27.9 C
Dar es Salaam
Thursday, March 28, 2024

Contact us: [email protected]

Watendaji kilimo wapewa zigo la kutafuta masoko ya uhakika

Na Mwanishi wetu, Dodoma

WAZIRI wa Kilimo, Japhet Hasunga, amewaagiza watendaji wakuu wa wizara yake na taasisi zake kusimamia kikamilifu uzalishaji wa mazao na upatikanaji wa masoko ya uhakika.

Alitoa kauli hiyo juzi alipofanya kikao kazi cha menejimenti iliyohusisha wakurugenzi wa wizara, bodi za mazao na wakala zilizo chini ya wizara hiyo jijini Dodoma kujadili utekelezaji wa kazi za wizara.

Hasunga alisema katika kipindi cha miaka mitano ya Serikali ya awamu ya tano, Wizara ya Kilimo imefanikiwa kuimarisha uzalishaji wa mazao hususan ya chakula hali iliyopelekea nchi kuwa na utoshelevu wa chakula katika kipindi chote.

“ Wizara ya Kilimo imefanya  mengi ya manufaa kwa kusimamia wakulima kuzalisha mazao mengi ya chakula na biashara hali iliyopelekea uchumi wa nchi kuimarika “ alisema Hasunga

Katika kikao hicho cha mwisho katika mwaka mwa fedha 2019/20, Hasunga  alisema watendaji wa wizara na taasisi zake watapimwa kwa  kuongeza uzalishaji  mazao ya kilimo, idadi ya ajira zitakazozalishwa kwenye mnyororo wa thamani wa zao,mchango wa zao katika upatikanaji wa fedha za kigeni na idadi ya wakulima na kiasi cha ekari wanachozalisha.

Alisema bodi za mazao zitapimwa kwa mashamba bora ya mfano waliyonayo, idadi ya viwanda vinavyochakata mazao ya Kilimo na idadi ya masoko  kwa mazao ya wakulima. 

Alizieleza bodi za mazao na taasisi zote kuhakikisha zinaweka utaratibu mzuri wa kuepusha kero za wakulima kuhusu upatikanaji wa mbegu bora, pembejeo, viuatilifu na masoko ili wanufaike na kazi za Kilimo .

“Rais John Magufuli ameagiza wizara ya Kilimo kuhakikisha inaondoa kero zote za wakulima kwa kuzitatua haraka katika ngazi zote ili asiwepo mtu atakayekuwa kikwazo kwa wakulima nchini” alisema Hasunga.

Katika kikao kazi hicho Waziri huyo wa alisema Serikali haitopanga bei za mazao ya pamba, mahindi mpunga au ufuta bali itahakikisha wakulima wanapata bei nzuri ya soko.

Kwa upande wake Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo, Gerald Kusaya, alisema watumishi na watendaji wa wizara wataendelea kutekeleza majukumu yao kwa weledi na ubunifu ili wakulima nchini wanufaike.

Alisema ataendelea kusimamia na kufuatilia utendaji kazi wa watendaji wakuu na taasisi zake ili malengo ya Serikali na maagizo yote yapatiwe utekelezaji ili uzalishaji na tija kwa mazao ya wakulima nchini uongezeke.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles