NA SAADA SALIM, DAR ES SALAAM
KOCHA mpya wa Simba, Joseph Omog, amesaini mkataba wa miaka miwili kukinoa kikosi hicho na kuahidi kurudisha heshima ndani ya klabu hiyo kwa kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara.
Omog aliwasili Dar es Salaam juzi usiku na kupokewa na Katibu mkuu wa klabu hiyo, Patric Kahemele ambaye aliwahi kufanya naye kazi wakati akiwa Azam FC.
Uongozi wa timu hiyo ulimtambulisha kocha huyo jana katika hafla iliyohudhuriwa pia na Rais wa klabu hiyo, Evans Aveva, Mwenyekiti wa Kamati ya Ufundi, Collin Frisch, Katibu Patrick Kahemele, Ofisa Habari, Haji Manara.
Akizungumza katika utambulisho huo, Omog alisema atahakikisha anatumia vema kipindi hiki cha usajili kwa kupendekeza wachezaji watakaosaidia timu kupata ushindi na kufanikiwa kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara msimu ujao.
Alisema baada ya kufanya mazungumzo na kukubaliana kuja kukinoa kikosi cha timu hiyo, alitumiwa ripoti iliyoachwa na kocha aliyepita ambapo aliangalia mahitaji na kuridhika nayo.
“Simba walinishirikisha kwa kila jambo hasa hili suala la usajili, walinitumia ripoti yao nikaona muda huu uliobakia tutashirikiana katika usajili ili kuendelea kuboresha zaidi kikosi cha timu yetu,” alisema Omog.
Alisema anafurahi kurejea kwa mara nyingi katika ardhi ya Tanzania na kuhakikisha timu yake inapata ushindi kwa kila mechi za ligi huku akilenga kupata ubingwa wa timu hiyo.
Alisema anafahamu wachezaji wa Tanzania pamoja na soka lake na anaamini atafanya vizuri akiwa na kikosi cha Simba kama alivyokuwa Azam aliyoipa ubingwa msimu wa 2013/14.
Tangu kuondoka kwa kocha Dylan Kerr Januari mwaka huu, Simba imekuwa haina kocha mkuu hivyo timu hiyo ilikuwa chini ya kocha msaidizi, Jackson Mayanja ambaye atafanya kazi na Omog.
Katika baadhi ya rekodi zake, Omog amewahi kuipa ubingwa wa Kombe la Shirikisho Afrika Leopard FC ya Kongo Brazzaville mwaka 2014, pia ni kocha wa kiwango cha juu cha ufundishaji soka na maozezi ya viungo aliyehitimu vizuri mafunzo yake katika Chuo cha Vijana na Michezo mjini Younde, Cameroon.
Alikwenda kujiendeleza kielimu nchini Ujerumani na kwa pamoja na Pierre Njili na Martin Ndtoungou, walipata stashahada za ukocha na leseni za UEFA daraja la B mwaka 1987.
Mwaka 2001 aliteuliwa kuwa msaidizi wa kocha Mjerumani, Winfried Schafer katika timu ya taifa ya Cameroon, chini ya nahodha, Samuel Eto’o kutokana na kujua kwake lugha ya Kijerumani.
Mwaka 2003 aliteuliwa kuwa kocha mkuu wa timu ya taifa baada kuondoka kwa Winfried Schafer, lakini akafukuzwa mwaka 2010 kutokana na matokeo mabaya na kushindwa kuiwezesha Cameroon kufuzu Fainali za Mataifa ya Afrika.
Akaamua kutoka nje ya nchi na mwaka 2011 alijiunga na AC Leopard ya Kongo, ambayo aliiwezesha kutwaa ubingwa wa Kombe la Shirikisho.