NA ZAITUNI KIBWANA
KOCHA Mkuu wa Azam FC, Joseph Omog, ametaka mechi mbili za majaribio kabla ya timu yake haijapambana na Yanga kwenye mechi ya Ngao ya Jamii.
Azam na Yanga zinatarajia kukutana Septemba 13, katika Uwanja wa Taifa kwenye mechi hiyo, inayoashiria kuanza kwa msimu mpya wa ligi.
Omog ambaye kwa sasa amerudi Dar es Salaam, baada ya kuondolewa kwenye michuano ya Kombe la Kagame alisema mechi hizo zitamsaidia kukiweka sawa kikosi chake.
“Alisema timu yake imepata uzoefu katika michuano ya Kombe la Kagame, ila anataka mechi nyingine mbili kwa ajili ya kujiweka sawa,” alisema.
Alisema kikosi chake kitaanza mazoezi rasmi kuanzia leo, baada ya mapumziko aliyotoa kwa wachezaji wake mara baada ya kurejea Dar es Salaam.
“Mechi hizo siwezi kusema nataka kucheza na nani, ila nataka timu yoyote itakayoweza kukipima kikosi changu kabla ya mechi yetu na Yanga,” alisema.