27.1 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

OMMY DIMPOZ TUMIA AKILI KUFIKIRI SIO VIDOLE

Na RAMADHANI MASENGA

MANENO yameponza wengi kuliko ukimya. Ukifanyiwa jambo ambalo sio sahihi na kukaa kimya, tafsiri zinaweza kuwa nyingi juu ya ukimya wako ila jua huwezi kupata athari kubwa kama ukiongea.

Rekodi zinaonesha wengi wanajutia maneno yao kuliko ukimya wao.  Unaweza kukaa kimya saa tatu na usimkere mtu. Ila ukiongea dakika kumi ni lazima kuna watu watakaofurahia maongezi yako na wengine watakuchukia kutokana na maneno yako.

Hii maana yake ni kwamba kukaa kimya kunaleta tokeo moja la kutochukiwa ila kuongea kunaleta matokea mawili. Ama kuchukiwa ama kupendwa.

Ommy Dimpoz kwa muda sasa amekuwa msanii zaidi wa mitandaoni kuliko redioni na kwenye runinga. Zamani tulizoea kusikia nyimbo zake zikitamba kwenye vipindi tofauti vya redio na runinga lakini siku hizi hali imebadilika.

Ni kama amesahau majukumu yake. Ni kama kakubali kuwa mpambe wa Ali Kiba. Ommy yuko zaidi katika mitandao kuliko muziki. Wakati wengine wakitamba katika mitandao kwa taarifa za kusisimua na kuleta burudani kwa wafuatiliaji wa mitandao hiyo, Ommy Dimpoz yuko busy kukera watu.

Wakati kile kinachoitwa disi kilichomo katika mistari ya Diamond katika wimbo wa Fresh Remix wa Fid Q  kikishika chati, wengi waliamini majibu ya Ali Kiba na wapambe wake yataegamea katika mashairi zaidi.

Toka enzi za kale, wasanii wamekuwa na tamaduni ya kudisiana kupitia mashairi na haijawahi kuwa ajabu. Ila wakati Ali Kiba akikwepa kumjibu Diamond katika wimbo na kwenda kumjibia Twitter, Ommy Dimpoz yeye akaenda mbali zaidi.

Bila kujua ama kupima kuwa ugomvi ule ulipaswa wapambane vijana na kuachana vijana, Dimpoz akakosa adabu na kumhusisha mama mzazi wa Diamond katika ugomvi ule.

Hapa hakuwa akimtusi Diamond na mama yake pekee. Ila ukweli ni kwamba alikuwa akiwakosea kina mama wote duniani na kujivua nguo mwenyewe hadharani.

Nani sasa atasema Dimpoz ana heshima na utu? Alichofanya Ommy Dimpoz  ni zaidi ya utoto. Ni zaidi ya ujinga. Ni upumbavu mkubwa kabisa. Katika nchi ya kistaarabu kama Tanzania, yenye kuheshimu maadili, huwezi kuhusisha ujinga wa ujana na kuwatusi wazee wetu.

Dimpoz hatakiwi kumuomba msamaha Diamond na mama yake tu. Anatakiwa ajue amewakosea kina mama wote duniani. Awaombe msamha. Pia ajikosoe kwa ujinga wake.

Kwa umri wake, mama wa Diamond ni mama yake pia. Alikunywa nini hata akili zikamruka na kufanya alilofanya?

Katika dunia ya muziki kuna mambo mengi unaweza kuyafanya ili kuchangamsha muziki wako. Miongoni mwa mambo hayo ni kumdisi msanii mwenzako.

Hiyo haipo katika Hip Hop ama Taarabu pekee. Hata Sikinde na Msondo Ngoma walikuwa na mchezo huo. Hata  malenga kina Shaaban Robert walifanya mambo haya.

Ujinga ni pale mtu unapodisiwa katika nyimbo badala ya kupambana na mhusika unahusisha wazazi. Hii haikubaliki.

Dimpoz ajitafakari sana. Wakati yeye akijikusanya na kuunda jeshi kwa Ali Kiba, Ali mwenzake anazidi kufanya makubwa katika muziki wake. Katika hiki kiitwacho bifu la Diamond na Ali Kiba, wote wanaojisogeza karibu hawafanyi lolote la maana zaidi ya wahusika kuzidi kujiimarisha kibiashara na kiumaarufu.

Katika bifu hili ukiwa karibu na Diamond ujue unamnadi na kumjenga zaidi Diamond na sio wewe. Ukiwa karibu na Kiba katika ugomvi huu jua unamsaidia zaidi kiba sio wewe.

Hivyo mafanikio wanayopata kutokana na huu ugomvi magirini, wewe huambulii chochote kwa sababu mwishoni majina ya hii miamba miwili ndiyo yatakayosimama.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles