Na – JOHANES RESPICHIUS – DAR ES SALAAM
IMEELEZWA kuwa Katiba haitoi haki na uhuru usiokuwa na ukomo hivyo mwenendo wa sasa wa kisiasa wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) wa kuchochea wananchi kwa makusudi kutotii maagizo halali ya vyombo vya dola na Serikali kwa kusingizia uhuru wa kikatiba ni kuikiuka.
Hayo yameelezwa jana na msemaji wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Christopher Ole Sendeka, katika mkutano wake na waandishi wa habari uliofanyikia ofisi ndogo za chama hicho zilizopo Lumumba.
Ole Sendeka ambaye aliutumia pia mkutano huo kutoa pole kwa askari wanne waliouawa katika shambulizi la kushtukiza juzi wakati wakibadilishana lindo katika Benki ya CRDB, Tawi la Mbande huko Temeke na pia kuelezea mafanikio ya Serikali ya awamu ya tano, alisema Chadema kinaitumia Katiba vibaya hivyo wananchi wanapaswa kukipuuza.
Alisema Chadema imekuwa ikitaja baadhi ya vifungu vilivyopo katika Katiba ili kuhalalisha matamko huku wakiacha vile vinavyowazuia kutekeleza matakwa yao ya kisiasa ambayo yana viashiria vya kuhatarisha amani na utulivu.
Alikitaja kitendo cha Chadema kutaka kufanya maandamano na mikutano nchi nzima siku ya Septemba mosi, mwaka huu kupinga kile ambacho imekuwa ikikitaja kuwa ni utawala wa mabavu wa Serikali iliyoko madarakani ni kuvunja sheria.
“Wanachotaka kufanya Chadema ni kuchochea wananchi kwa makusudi kutotii maagizo ya vyombo vya dola na Serikali, wanafanya visingizio mufilisi kwa madai kwamba Katiba inawapa uhuru wakati Katiba haitoi haki na uhuru usiokuwa na kikomo.
“Ibara ya 29 (5) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano inasema: Ili watu wote waweze kufaidi haki na uhuru vinavyotajwa na Katiba hii, kila mtu ana wajibu wa kutenda na kuendesha shughuli zake kwa namna ambayo haitaingilia haki na uhuru wa watu wengine au masilahi ya umma.
“Hivyo basi Chadema wakumbuke na kutilia maanani kuwa kila haki ina wajibu na hakuna haki au uhuru usiokuwa na ukomo, hususani pale inaposababisha kuingiliwa ama kukatizwa kwa haki au uhuru wa watu wengine na ibara ya 30 (1) na (2),” alisema Ole Sendeka.
Alisema ingawa sheria ya vyama vya siasa inaruhusu kufanyika kwa mikutano na maandamano na kifungu 11 kidogo cha kwanza A, kinatoa uhuru wa kufanya mkutano kwa nia ya kujitangaza na ya kutafuta wanachama lakini si kwa visingizio vya kuishtaki Serikali kwa wananchi.
“Pia kifungu cha 11 (6) kinaweka utaratibu ambao wote tunatakiwa kuandika barua ya kutoa taarifa polisi kuhusu kufanya mkutano na polisi wa eneo hilo wana uwezo wa kuuzuia kwa sababu ambazo wataziandika kwenye notisi.
“Tumeshuhudia vituko vinavyofanywa ikiwa ni pamoja na maazimio ya kutopeana mikono, kutohudhuria misiba, sherehe, kuziba midomo na vituko hivyo vilivyoanzishwa na vyama vinavyounda Ukawa ndivyo vinavyozidi kuasisi na kupandikiza mbegu ya chuki miongoni mwa Watanzania,” alisema Ole Sendeka.
Wakati huo huo, Ole Sendeka alimtaka Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema, Edward Lowassa, kukubaliana na kushindwa katika uchaguzi mkuu uliofanyika mwaka jana.
Lowassa ambaye alikuwa Waziri Mkuu wa kwanza wa Serikali ya awamu ya nne kabla ya kujiuzulu kwa kashfa ya Richmond, aliondoka CCM baada ya jina lake kutopitishwa kuwa mgombea urais na kujiunga na Chadema kilichompitisha kuwa mgombea wake wa nafasi hiyo lakini alishindwa na Rais wa sasa, Dk. John Magufuli.
“Lowassa alishindwa kukidhi vigezo ndani ya CCM na akashindwa kuwa rais wa nchi kwa sababu kura hazikutosha. Alisema atakibadilisha Chadema kutoka chama cha uharakati kuwa cha siasa, lakini yeye ndiye amebadilika kuwa mwanaharakati.
“Kama anaamini kuna kura yake iliyoibiwa alete ushahidi wa nakala moja ya kituo hicho kinachoonesha tofauti na matokeo ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC). Huu ni umaarufu unaotafutwa kwenye migongo na majeneza ya watu, CCM imepewa kibali cha kuongoza nchi na dhamana hii tutaitetea na kuilinda kwa nguvu zote na hakuna damu itakayomwagika kabla wachochezi hawajashughulikiwa vya kutosha,” alisema Ole Sendeka.
Aidha, msemaji huyo alisema CCM kimepokea kwa majonzi na masikitiko makubwa taarifa ya kushambuliwa na kuuawa kwa askari polisi waliokuwa wakitekeleza majukumu yao ya ulinzi katika Benki ya CRDB Tawi la Mbande.