23.1 C
Dar es Salaam
Monday, September 25, 2023

Contact us: [email protected]

Ulimwengu anusurika kifo kwa ajali ya gari

ULIMWENGUNa Veronica Romwald, Dar es Salaam

MWANAHABARI nguli, Jenerali Ulimwengu, juzi usiku alinusurika kufa kwa ajali ya gari iliyotokea katikati ya makutano ya Barabara ya Ali Hassan Mwinyi na Kenyatta.

Akizungumza na MTANZANIA Jumamosi jana, Ofisa Uhusiano wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), John Stephen, alisema Ulimwengu alipokelewa hospitalini hapo saa nane usiku.

“Aliletwa hospitalini usiku wa saa nane ya kuamkia leo (jana) na kupelekwa moja kwa moja kitengo chetu cha wagonjwa wa dharura (emergence) ambako alipatiwa huduma ya kwanza,” alisema Stephen.

Alisema baadaye Ulimwengu alihamishiwa Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Mishipa ya Fahamu (MOI) kwa ajili ya vipimo zaidi.

Ofisa Uhusiano wa MOI, Patrick Mvungi, alisema Ulimwengu alifikishwa katika taasisi hiyo saa 11 alfajiri.

Alisema miongoni mwa watu waliomtembelea kumjulia hali ni pamoja na Balozi Juma Mwapachu na Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Vicent Mashinji.

Mke wa Ulimwengu, Josephine aliliambia gazeti hili nje ya wodi aliyolazwa mumewe kuwa daktari anayemtibia amemtaka kupumzika kwa muda mrefu.

“Namshukuru Mungu hali yake si mbaya kama mnavyomuona ila haruhusiwi kuongea kwa sasa, hapa mmemkuta kaamka kwa sababu nampatia chakula, daktari ameshauri kwamba anahitaji muda mwingi wa kupumzika,” alisema Josephine.

Wakati huo huo, Mvungi alisema Mbunge wa Ukerewe (Chadema), Joseph Mkundi ambaye amelazwa katika taasisi hiyo baada ya kupata ajali ya gari iliyosababisha kuvunjika mkono amefanyiwa upasuaji na sasa afya yake inazidi kuimarika.

“Mbali na Mkundi, Mbunge wa Malindi (CUF), Ally Salehe ambaye naye alilazwa kwa matibabu ameruhusiwa kurudi nyumbani kwake baada ya afya yake kuimarika,” alisema Mvungi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,718FollowersFollow
574,000SubscribersSubscribe

Latest Articles