31.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, December 11, 2024

Contact us: [email protected]

OKWI AISHIKA PABAYA SIMBA

Na Mohammed Kassara

KIWANGO kilichoonyeshwa juzi na mshambuliaji wa kimatiafa wa Uganda ‘Cranes’ , Emmanuel Okwi katika mchezo wa fainali za Mataifa Afrika (Afcon), dhidi ya Jamhuri ya Kidemokrasia Kongo (DRC), kimezidi kuiweka timu yake ya Simba kwenye wakati mgumu wa kumshawishi kuongeza mkataba mwingine ili kusalia  Msimbazi.

Okwi katika mchezo huo alionesha kiwango cha juu na kuisadia Cranes kuibuka na ushindi wa mabao 2-0 huku mshambuliaji huyo akifunga bao moja.

Ushindi huo uliifanya Uganda kujikusanyika pointi tatu na kuongoza msimamo wa Kundi A, ikiwaacha wenyeji Misri inayolingana nayo kwa pointi katika nafasi ya pili, kutokana na wastani mzuri wa mabao ya kufunga, huku Zimbabwe ikikamata mkia ikiwa haijaambulia pointi yoyote.

Katika mchezo huo, Okwi aliifunga bao la pili la Cranes kwa kichwa dakika ya 48, huku jingine likiwekwa kambani na mshambuliaji wa KCCA,  Patrick Kaddu  dakika ya 14.

Mbali ya kuchangia ushindi huo, Okwi  pia alitangazwa mchezaji bora wa mchezo huo, mara baada ya pambano hilo kumalizika.

Makali ya Okwi akiwa na Cranes  yanazidi kuiweka Simba mahali magumu zaidi, baada ya nyota  huyo kumaliza mkataba wa kuitumikia klabu hiyo na huku kukiwa na taarifa za kutakiwa na klabu mbali mbali za nje ya Tanzania.

Ni wazi amewaweka Wekundu hao katika mtego wa kuhakikisha kwanza inaweka dau kubwa mezani ili kumshawishi  kusalia viunga vya Kariakoo.

Kinyume na hivyo inaweza kete na miamba ya Afrika Kusini, timu ya Kaizer Chiefs ambayo pia inahusishwa kumwania mshambuliaji huyo wa zamani wa SC Villa ya Uganda.

Kaizer Chiefs imekuwa ikivutiwa na kiwango cha staa huyo tangu msimu uliopita lakini kikwazo kilikuwa mkataba wake na Simba.

Moto aliouwasha katika mchezo dhidi ya DRC ni wazi utamfanya azidi kufuatiliwa na miamba hiyo lakini pia klabu nyingine za ndani na nje ya Afrika ambazo kipindi hiki ambacho mawakala wao wapo nchini Misri kuifuatilia Afcon  kwa lengo la kunyakuwa wachezaji wakali.

Okwi anasifika kwa umakini wake linapokuja suala la mkataba, kwani hii si mara ya kwanza kuihenyesha Simba kabla ya kufikia makubaliano na kuanguka saini.

Msimamo wake huo umekuwa ukimwezesha kuvuna fedha za kutosha kila anaposaini mkataba mpya.

Tangu alipotua kwa mara ya kwanza Simba mwaka 2009, Okwi amekuwa mchezaji muhimu wa kikosi hicho, akikisaidia kutwaa mataji matatu ya Ligi Kuu  Bara, ikiwemo mara mbili mfululizo msimu wa 2017-2018 na 2018-2019.

Pia aliiwezesha Simba kufika robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu uliopita.

Okwi alimaliza mfungaji bora wa Ligi Kuu  Tanzania Bara msimu wa 2017/2018, baada ya kupachika mabao 20, lakini msimu uliopita alimaliza akifunga mabao 15.

Mshambuliaji Meddie Kagere ambaye pia anakipiga Simba ndiye aliyekuwa kinara wa ufungaji baada ya kupachika mabao 23.

Mpaka sasa Simba imefanisha usajili wa wachezaji wawili pekee katika  eneo la ushambuliaji, Mbrazil, Wilker Henrique da Silva, kutoka klabu ya Bragantino inayoshiriki  Ligi Daraja la Nne nchini kwao, pia ikiwaongeza mikataba washambuliaji, Kagere na John Bocco.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
592,000SubscribersSubscribe

Latest Articles