LAGOS, NIGERIA
PRODYUZA maarufu nchini Nigeria, Babatunde Okungbowa ‘OJB Jezreel’, amefariki duniani baada ya kusumbuliwa na tatizo la figo kwa miaka mitatu.
Mtayarishaji huyo wa muziki nchini humo katika studio yake ya Silverpoint, alikuwa maarufu kutokana na kuwatoa wasanii wakubwa wanaofanya vizuri kwa sasa ndani na nje ya nchi hiyo akiwemo, Benjamin Njoku, Kehinde Ajose na Iyabo Aina.
Mwaka jana prodyuza huyo alikwenda nchini India kwa matibabu ya ugonjwa huo na mwezi ujao ilikuwa afanye sherehe ya kutimiza miaka 50.
Msemaji wa familia hiyo, aliweka wazi kwamba OJB alianza kuzidiwa wiki iliyopita ambapo aligundulika kwamba figo yake imeshindwa kufanya kazi na kukimbizwa katika hospitali ya mjini Lagos.
OJB amefariki huku akiacha wake zake watatu ambao ni Mabel, June na Korede pamoja na watoto wanane.