NA MANENO SELANYIKA, DAR ES SALAAM
TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Kinondoni, imempandisha kizimbani Ofisa wa Idara ya Uhamiaji, Magreth Prosper (33) kwa tuhuma za kupokea rushwa kutoka kwa raia wa China, Lizhi Ping.
Ofisa huyo ambaye ni mkazi wa Kitunda, Dar es Salaam, anadaiwa aliomba Sh milioni 12.6 na shtaka la pili anadaiwa kuomba na kupokea Sh 63,000 kutoka kwa Ping.
Mbele ya Hakimu Obadia Bwegoge, Mwendesha Mashtaka wa Takukuru, Faraja Sambala, alidai mtuhumiwa alipokea fedha hizo kwa nyakati tofauti.
Katika shtaka la kwanza, inadaiwa alifanya kosa hilo Januari 26 mwaka huu, wakati kosa la pili alilitenda Januari 24 mwaka huu.
“Mtuhumiwa unadaiwa kumshawishi Ping akupe kiasi hicho cha fedha uweze kumrudishia paspoti zake 10 za kusafiria ulizozichukua kwa ajili ya ukaguzi.
“Mbali na hilo, pia ulizidi kumshawishi akupatie fedha kwa sababu aliegesha gari kando ya ofisi za Manispaa ya Kinondoni kitu ambacho ni kinyume cha sheria,” alidai mwendesha mashtaka.
Mtuhumiwa alikana kutenda shtaka hilo na upelelezi unaendeleana kesi iliahirishwa hadi Februari 24 mwaka huu huku mtuhumiwa akiwa ameachiwa baada ya kutimiza masharti ya dhamana.
Katika hatua nyingine, mahakama hiyo imeahirisha kesi inayowakabili watuhumiwa watano wanaodaiwa kumlawiti mwenzao (jina tunalo) mwenye umri wa miaka 23, walipokuwa katika mahabusu Kituo cha Polisi cha Urafiki hadi Februari 15.
Tukio hilo lilitokea Januari 8 mwaka huu ambapo watuhumiwa hao walielezwa kuwa ni Jafari Ally (27), Yusuph Salum (17), Moshi Mikendo (18), Ally Said (18) na Ibrahim Hamis (25).
Mbele ya Hakimu Is – Haq Kuppa, Wakili wa Serikali, Faustine Sylivester, alidai upelelezi wa kesi hiyo haujakamilika.