Self Takaza, Iringa
TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) mkoani Singida, imempandisha kizimbani Ofisa Mifugo wa Halmashauri ya Mkalama kwa kupokea rushwa ya Sh 20,000 ili atoe kibali cha kuuzia nyama.
Mtumishi huyo John Yako (32) ambaye ni Ofisa Mifugo daraja la pili, alipandishwa kizimbani mbele ya Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Wilaya ya Iramba, Sydney Nindi.
Mwanasheria wa Takukuru Mkoani Singida, Mzalendo Widege, akisoma mashitaka alidai Mei 28, 2020 Yako aliomba rushwa ya Sh 20,000 kwa Ramadhani Shumbi kinyume na sheria ya Kuzuia na kupambana na Rushwa kifungu 15(1)na (2)namba 11 ya mwaka 2007.
Widege alidai katika shtaka la pili, mtuhumiwa huyo anadaiwa kuwa Mei 30, 2020 katika Kata ya Ibaga wilayani Mkalama Mkoa wa Singida, alikamatwa na Maofisa wa Takukuru kwa kupokea Sh 20,000 ili amsamehe Ramadhani Shumbi kutolipa kibali cha kuuza nyama.
Mtuhumiwa alikana mashtaka hayo na Hakimu, Nindi aliahirisha kesi hiyo hadi Juni 16 mwaka huu ambapo kesi hiyo itaanza kusikiliza hoja za awali. Mtuhumiwa yuko nje kwa dhamana ya Sh 1,000,000.