23.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, September 28, 2021

Joe Hart ni wakati wa kusoma alama za nyakati

Badi Mchomolo

KWENYE soka kila mchezaji ana wakati wake, hivyo ni vizuri kuutambua wakati huo na kuutumia kabla ya kubadilika kutokana na umri pamoja na ushindani uliopo kwa kipindi husika.

Hakuna kipindi kizuri ambacho timu ya taifa ya England ilikuwa inajivunia kwenye safu ya kulinda lango kama ilivyokuwa msimu wa 2011/2012, baada ya kipa wao Joe Hart kuonesha ubora wake akiwa na kikosi cha Manchester Cityb ambacho kilichukua ubingwa wa Ligi Kuu England ikiwa mchezaji huyo ana miaka mitano tangu ajiunge akitokea klabu ya Shrewsbury Town.

Mlinda mlango huyo alipewa kila sifa kama inavyojulikana England wanavyoweza kuwapandisha thamani wachezaji wa nchi hiyo. Aliendelea kuonesha ubora wake na kuisaidia klabu hiyo kutwaa jumla ya mataji mawili ya Ligi Kuu England, Kombe la Ligi mara mbili na FA mara moja.

Wakati wake ulianza kupotea kwenye michuano ya Kombe la Euro mwaka 2016 huko nchini Ufaransa ambapo Ureno walifanikiwa kuwa mabingwa.

Hart hakuweza kuonesha kile ambacho alikuwa anakionesha akiwa na klabu ya Manchester United ingawa ndani ya timu ya taifa England ndio kipa namba moja.

England walijikuta wakiyaaga mashindano hayo katika hatua ya 16 bora baada ya kupoteza kwa mabao 2-1 dhidi ya Iceland, lakini lawama nyingi zilikwenda kwa kipa huyo namba moja ambapo alionekana kufungwa mabao ya kizembe. Alitajwa kuwa mmoja kati ya makipa waliofanya makosa makubwa kwenye michuano hiyo.

Kurudi kwenye viwanja vya Etihad, kocha wa timu ya Manchester City, Pep Guardiola hakuona mabadiliko ya kipa huyo, aliendelea kufanya yale aliyokuwa akiyafanya nchini Ufaransa kwenye michuano ya Euro, hivyo kocha huyo hakuwa na muda tena kumtengeneza.

Kocha huyo anaamini ubora wa timu unaanzia kwenye safu ya ulinzi kama alivyofanya akiwa ndani ya klabu ya Barcelona na Bayern Munich na kupata mafanikio makubwa. Mlinda mlango wa Guardiola lazima awe na uwezo wa kutumia miguu vizuri, lakini Hart hakuwa na vigezo hivyo na ndio maana Guardiola hakuweza kumuamini kwenye kikosi chake cha kwanza japokuwa kocha huyo alidai wawili hao wapo kwenye maelewano mazuri ndani na nje ya uwanja. Nafasi yake ikachukuliwa na mlinda mlango kutoka nchini Chile, Claudio Bravo.

Ujio wa kipa huyo uliufanya uongozi wa Manchester City kumtoa Hart kwa mkopo na kumpeleka katika klabu ya Torino na baadae kumpeleka West Ham na mwisho wa siku akauzwa moja kwa moja katika klabu ya Burnley.

Ilikuwa maumivu makubwa kwa mchezaji huyo kuondoka Manchester City kwa namna hiyo ikiwa aliandika historia ya kutwaa taji la Ligi Kuu mara mbili mfululizo pamoja na tuzo ya mlinda mlango bora Ligi ya England.

Lakini kitendo cha kuachwa na kocha huyo huku akiwa ameipa mafanikio makubwa klabu hiyo anadai kuliichanganya akili yake na ndio maana hadi sasa hajaweza kuwa kwenye ubora wake kwenye kikosi cha timu ya taifa pamoja na kazi ya klabu.

Kwa umri wake wakati ule anajiunga na klabu ya Torino na West Ham kwa mkopo haukuwa wakati sahihi, Man City wangeweza kumuuza moja kwa moja na sio kumtoa kwa mkopo akiamini ipo siku anaweza kurudi kikosini, lakini akaja kuuzwa baadae baada ya kuona hana namba tena.

Kwa sasa anakipiga katika klabu ya Burnley tangu kiangazi mwaka 2018, lakini hayupo kwenye kikosi cha kwanza kama enzi anatamba akiwa na Manchester City.

Tangu amejiunga na Burnley hadi sasa amekaa langoni mara 19 kwenye michuano ya Ligi Kuu nchini England, hii inaonesha jinsi gani wakati unavyo muacha. Umri wake wa miaka 33 ni kawaida kwa walinda mlango kuwa kwenye ubora wao.

Makipa wamekuwa tofauti na wachezaji wengine, wao wanaweza kuwa bora miaka yao inapozidi kuwa mikubwa, miongoni mwa walinda milango ambao wanaendelea kufanya vizuri wakiwa na umri mkubwa ni pamoja na Gianluigi Buffon, ambaye ni kipa wa timu ya Juventus na ana miaka 42.

Ikiwa ni misimu miwili kwa Hart ndani ya klabu ya Burnley, lakini ni mlinda mlango namba mbili huku namba moja ikiwa chini ya Nick Pope mwenye umri wa miaka 28, ambaye amekuwa hapo tangu mwaka 2016.

Hata kwenye kikosi cha timu ya taifa Hart hana nafasi tena kwenye kikosi cha kwanza huku mara ya mwisho akidaka mwaka 2017 na nafasi yake inachukuliwa na Pope.

Dalili za kuendelea kuwa mchezaji wa Burnley zinaonekana kufikia mwisho ambapo klabu hiyo ipo kwenye mipango ya kuachana naye na anahusishwa kuwindwa na klabu zinazoshiriki Ligi Kuu nchini Marekani. Huu ni wakati wake wa kusoma alama za nyakati, kila kitu kina mwisho wake, Marekani kunaweza kumfaa zaidi.

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

66,457FansLike
158,460FollowersFollow
519,000SubscribersSubscribe

Latest Articles