Renatha Kipaka – Bukoba
WANAFUNZI 18 wa sekondari katika Halmashauri ya Bukoba mkoani Kagera, wamepata mimba katika kipindi cha mwaka 2019.
Kutokana na hali hiyo, Ofisa Elimu Sekondari wa halmashauri hiyo, Chacha Mengewa ametaka masomo ya dini yapewe nafasi ili kujenga maadili.
Mengewa alitoa kauli hiyo jana wakati alipokuwa anajibu maswali yaliyoulizwa na baadhi ya madiwani kuhusu wingi wa mimba mashuleni.
“Ili kutokomeza mimba mashuleni, wazazi na walezi kwa kushirikiana na Serikali kuanzia ngazi za vijiji wanatakiwa kuwaelimisha watoto wa kike kwa kuwapa uwazi na kuwaambia madhara yanayotokana na ubebaji mimba katika umri mdogo,” alisema Mengewa.
Alisema vipindi vya dini katika shule vipewe kipaumbele ili kuwasaidia kuogopa, maana mtoto wa kike akipata mimba mfumo wake wa maisha huwa unaishia hapo hasa akiwa anatokana na familia isiyo na uwezo wa kumwendeleza kielimu.
“Niseme tu ili kuepuka vishawishi hivyo kuwepo na utaratibu wa kuwapa kazi wanafunzi wa kike ili wawe na muda mchache wa kupumzika, nayo inaweza kusaidia,” alisema Mengewa.
Naye Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo, Murushidi Ngeze ambaye ni diwani wa Kata ya Rukoma kupitia CCM, alisema ili kutokomeza mimba za kabla ya wakati Jamii ishiriki kikamilifu ili kuondoa jambo hilo.
Wazazi waondoe mzizi huu kwa kuwajengea mfumo mzuri wa dini watoto kuanzia majumbani hadi shuleni huko wanakoshinda ili wawe na hofu ya Mungu.
“Hembu tujiulize mtoto anapobeba mimba, mfano yuko kidato cha pili, maisha yake yanakuwa vipi, maana kwanza anakuwa ni mdogo kiasi kwamba mtoto anamzaa mtoto na mwisho wa siku anakuwa amepoteza mwelekeo wa maisha yake,” alisema Ngeze.
Alisema jambo hili niwatake watu wa elimu msingi na sekondari kuainisha jambo hilo ili liletwe kwenye kamati maalumu kutafuta ufumbuzi wa kuondoa mimba mashuleni, isiwe wimbo wa kila wakati.