28.7 C
Dar es Salaam
Sunday, November 28, 2021

Uboreshaji daftari la wapigakura wapiga hodi Pwani

Gustaphu Haule  – Pwani

TUME ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imeanza kutoa mafunzo ya uboreshaji wa daftari la kudumu la wapigakura kwa maofisa waandikishaji wa Mkoa wa Pwani walioteuliwa kusimamia kazi hiyo.

Mafunzo hayo yameanza kutolewa jana ofisi za Mkuu wa Mkoa wa Pwani mjini Kibaha yakiwajumuisha maofisa waandikishaji, maofisa waandikishaji wasaidizi, maofisa uchaguzi na maofisa Tehama wa halmashauri za mkoa.

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo, Mjumbe wa NEC, Jaji mstaafu Mary Longway, alisema uboreshaji huo unafanyika kwa mujibu wa sheria ya uchaguzi.

Jaji Longway alisema mafunzo hayo yanatolewa kwa awamu tatu na kwamba awamu ya kwanza ni kwa ngazi ya mkoa, jimbo na baadae ngazi ya kata, huku lengo kubwa ni kuhakikisha kila mwananchi anajiandikisha.

“Zoezi la uboreshaji wa daftari la kudumu la wapigakura ni endelevu kwakuwa tayari limepita mikoa mingi na sasa tuko Pwani, kwahiyo tume imejipanga vizuri kuhakikisha kila Mtanzania anapata fursa ya kujiandikisha,” alisema Jaji Longway.

Kwa upande wake, Mratibu wa Uandikishaji Mkoa wa Pwani, Gerald Mbosoli, alisema baada ya kumaliza mafunzo hayo kwa maofisa waandikishaji, hatua itakayofuata ni kuingia katika mitaa kuendesha uandikishaji huo.

Mbosoli alisema uandikishaji wa daftari la kudumu la wapigakura utaanza rasmi Februari 14 na kumalizika Februari 20 na kwamba tume imetoa siku saba kuendesha zoezi hilo.

Aidha Mbosoli aliwataka wananchi wa Mkoa wa Pwani kujitokeza kujiandikisha kwakuwa hatua hiyo ni maandalizi ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba na asiyejiandikisha atakuwa amekosa haki na fursa ya kumchagua kiongozi anayemtaka.

Hata hivyo, awali kabla ya mafunzo hayo kufunguliwa, washiriki walikula kiapo namba sita na saba vilivyohusu kutojihusisha na chama cha siasa, utii na uaminifu kilichoendeshwa na Hakimu wa Mahakama ya Wilaya ya Kibaha, Joyce Mushi.

- Advertisement -
bestbettingafrica

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

66,457FansLike
167,206FollowersFollow
526,000SubscribersSubscribe
- Advertisement -
10Bet

Latest Articles