26.4 C
Dar es Salaam
Tuesday, November 26, 2024

Contact us: [email protected]

ODINGA APITISHWA KUMKABILI UHURU KENYATTA

Na Mwandishi Wetu-Nairobi, Kenya


 

BAADA ya minong’ono ya muda mrefu, ikiwamo uwezekano wa kutokea mpasuko tangu mwishoni mwa mwaka jana, hatimaye Muungano Mkuu wa Vyama vya Upinzani nchini Kenya (NASA), umemteua aliyekuwa Waziri Mkuu, Raila Odinga kuwa mgombea wake wa urais katika Uchaguzi Mkuu utakaofanyika Agosti 8.

Mbali ya Odinga, mgombea mwenza atakuwa Makamu wa Rais wa zamani, Kalonzo Musyoka, ambaye ni kiongozi wa Chama cha Wiper Democratic Movement huku Kiongozi wa Chama cha Amani National Congress (ANC), Musalia Mudavadi akitarajia kuwa Waziri Mkuu Mratibu wa Shughuli za Serikali.

Wengine ni Kiongozi wa Ford Kenya, Moses Wetangula, ambaye atakuwa Naibu Waziri Mkuu wa Masuala ya Uchumi huku Kiongozi wa Chama cha Mashinani (CCM), Isaac Ruto akitarajia kuwa Waziri Mkuu atakayesimamia utawala na huduma za jamii.

Uteuzi huo wa Odinga na wenzake umekuja baada ya kikao cha siku mbili cha Jumanne na Jumatano wiki hii, ambacho pamoja na mambo mengine, kimekubaliana juu ya muundo huo wa uongozi serikalini, iwapo watashinda Uchaguzi Mkuu unaotarajia kuwa wenye ushindani mkali na kihistoria.

Odinga sasa atakabiliana na Rais Uhuru Kenyatta atakayetetea kiti chake kupitia chama tawala cha Jubilee kwa muhula wa pili.

Katika sherehe zilizofanyika Uwanja wa Uhuru Park jijini Nairobi jana, viongozi hao watano wa NASA walishirikiana bega kwa bega kuzungumzia umoja na mshikamano wa muungano wao.

Walisikika wakizungumza kwa mbwembwe nyingi na kutamba, kwamba huu ni mwaka wa kuikomboa Kenya kwa mara nyingine kutokana na kile walichodai imetawaliwa kwa misingi ya uongo na mabavu bila ya kufuatwa sera.

Akihutubia umati mara baada ya kutangazwa kuwa mgombea, Raila alisema: “Hii ni heshima kubwa, ambayo ndugu zangu wamenifanyia, kwa kuniweka nipeperushe bendera ya NASA. Tumekuwa na vikao ambavyo vimechukua siku nyingi. Kila kitu tumeandika, tumekubaliana ya kwanza Serikali tutakayoiunda, ambayo ni ya mseto. itakuwa Serikali ya mpito.”

Alisema atakuwa kama Joshua wa kwenye Biblia na kuvusha Wakenya hadi nchi ya ahadi.

“Sisi tuko kama timu yenye pembe tano (Pentagon), wamenipa utepe wa nahodha, hiyo inaniunganisha mimi nao na Wakenya wote, tutatembea pamoja bega kwa bega. Tunataka kuibadilisha Kenya na kutekeleza ndoto ya waanzilishi wa taifa letu,” alisema.

Alisema Serikali yake itajikita katika kumaliza umasikini, kuimarisha afya, kuboresha uchumi, kubuni ajira na kushusha gharama ya elimu na maisha.

Odinga pia ameahidi kuhakikisha walimu, madaktari na wafanyakazi wengine wanalipwa mishahara mizuri.

Kadhalika, ameahidi kuwa akishinda Serikali yake itamaliza tatizo la rushwa serikalini.

Naye Makamu wa Rais wa zamani, Musalia Mudavadi, akizungumza katika mkutano huo, alisema viongozi wote wakuu wa muungano huo wamekubaliana kumuunga mkono mgombea huyo mmoja.

“Tumekubali kwamba mpangilio huu wa uongozi ni mpangilio ambao tunataka ulinganishwe na Rasimu ya Bomas ambayo Wakenya walitaka, lakini haikuidhinishwa,” alifafanua.

Alisema mpango wao ni kuwa na wadhifa wa kinara wa mawaziri na wasaidizi wake, kama ilivyokuwa katika rasimu hiyo ya katiba.

Kutangazwa kwa Odinga kupeperusha bendera ya NASA katika uchaguzi wa rais, ni hatua iliyokuwa ikisubiriwa kwa hamu kubwa na pande zote za kisiasa, hasa kutokana na mivutano iliyokuwa ikiendelea katika muungano huo juu ya nani hasa anayestahili.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles