28.7 C
Dar es Salaam
Monday, October 25, 2021

KESI MAUAJI BARLOW SHAHIDI: NILISHANGAA KUSIMAMIA UPEKUZI WAKATI SI KIONGOZI

Na MASYENENE DAMIAN -MWANZA


KESI ya mauaji ya kukusudia ya aliyekuwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, marehemu Liberatus Barlow, inayomkabili Muganyizi Michael na wenzake sita, imeendelea kusikilizwa jana katika Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Mwanza kwa mashahidi wawili wa upande wa mashtaka kutoa ushahidi wao.

Mashahidi hao, namba 13 na 14 walitoa ushahidi wao mbele ya Jaji  Sirilius Matupa, anayesikiliza shauri hilo namba 192 la mwaka 2014.

Akiongozwa na Wakili wa Serikali, Revina  Tibilengwa kutoa ushahidi wake, shahidi namba 13, Mohamed Shabani alidai Novemba 3, 2012 aliamshwa saa 12 asubuhi na watu waliojitambulisha kwake kuwa ni askari polisi.

Baada ya kuamka, aliwakuta askari watatu nje ya nyumba yake wakiwa na silaha wakamweleza  kuna jirani yake wanamshuku, hivyo wanahitaji kumfanyia upekuzi, lakini yeye awe shuhuda.

Baada ya ushahidi wake, shahidi huyo aliulizwa maswali na mawakili wa upande wa utetezi ambao walihoji kwanini shahidi huyo  aliitwa kuwa shuhuda wa upekuzi, wakati yeye siyo mwenyekiti wala mjumbe wa uongozi wa mtaa huo na ndipo alipojibu kuwa hata yeye alishangazwa na kitendo hicho.

Mahojiano kati ya wakili wa utetezi, Allanus Bubezi na shahidi yalikuwa hivi.

Wakili: Wewe pale siyo mwenyekiti wa mtaa na kulingana na hati ya upekuzi ni wewe peke yako ndiyo ulishuhudia, je uliambiwa kulikuwa na ugumu wa kumpata mwenyekiti?

 

Shahidi: Hapo hata mimi nilishanga,niliitikia wito kwa kuwa niliamshwa.

Wakili: Unafahamu kwamba hii ni fomu ya polisi na ulilazimishwa kusaini?

Shahidi: Mimi nilifuata maagizo kama nilivyoelekezwa.

 

Wakili: Unaishi pale tangu 2002.

Shahidi: Ndiyo

Wakili: Kutoka nyumbani kwako na kwa jirani yako (mtuhumiwa) siyo mbali?

Shahidi: Siyo mbali sana.

 

Wakili: Unawezaje kuishi miaka yote hiyo bila kuwafahamu jirani zako?

 

Shahidi: Ninachojali ni mihangaiko yangu.

 

Wakili: Je nikisema una wafahamu jirani zako ila unaiongopea mahakama nitakuwa nimekosea?

Shahidi: Ndiyo utakuwa unakosea.

Shahidi huyo alimaliza kutoa ushahidi wake muda wa saa sita mchana na kutoa nafasi kwa shahidi namba 14, Ikombe Pius mkazi wa Nyashana jijini Mwanza.

Pius alitoa ushahidi wake, ambapo alitumia muda wa dakika 34 kabla ya mahakama kwenda mapumziko ya muda wa saa moja na kisha kuendelea tena mchana kwa mawakili wa upande wa utetezi kuuliza maswali mbalimbali kwa shahidi huyo.

Awali akiongozwa na Wakili wa Serikali, Ajuaye Bilishanga, shahidi huyo aliieleza mahakama kuwa Novemba 3, 2012 saa 12:30 mchana, akiwa  eneo lake la kazi stendi ya mabasi ya Tanganyika, alipigiwa simu na mkewe akimweleza nyumbani kuna askari wengi na raia wamejaa, wanasema redio Call na ufunguo wa gari vimedumbukizwa kwenye shimo la choo chake.

Wakili: Baada ya kupata taarifa hizo ulifanya nini?

Shahidi: Nilimjibu mke wangu wasubiri nije.

Wakili: Ulipofika nyumbani ulikuta nini?

Shahidi: Nilikuta watu wengi,kiongozi wa askari anaitwa Konyo akajitambulisha na kuonesha kitambulisho chake.

Wakili: Baada ya kujitambulisha ulielezwa nini?

Shahidi: Nimfuate balozi.

Wakili: Baadaye ikawaje?

Shahidi: Konyo akaniuliza unawatambua hawa (watuhumiwa wawili waliokuwa wamekalishwa chini wamefungwa pingu mkononi), nikasema siwatambui.

Wakili: Baadaye ikawaje?

Shahidi: Akasema  hawa watu ndiyo waliomuua kamanda wetu wa polisi, wakachukua ufunguo wake wa gari na redio call wakaja kudumbukiza kwenye shimo la choo chako, tunaomba tubomoe tutoe hivyo vitu.

Kesi hiyo, inatajwa tena leo kwa ajili ya kusikilizwa ambapo mashahidi wa upande wa mashtaka wataaendelea kutoa ushahidi wao.

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

66,457FansLike
163,099FollowersFollow
522,000SubscribersSubscribe

Latest Articles