Na VERONICA ROMWALD – DAR ES SALAAM
TAASISI ya Saratani Ocean Road (ORCI), imeongeza idadi ya aina za saratani ambazo watatoa huduma ya uchunguzi wa awali, lengo likiwa kuongeza nguvu ya mapambano dhidi ya magonjwa hayo.
Hayo yalielezwa jana hospitalini hapo na Mkurugenzi wa Mipango, Daudi Maneno, alipozungumza wakati wa ufunguzi wa semina ya siku moja kwa waandishi wa habari kuelekea maadhimisho ya Siku ya Saratani Duniani.
“Tuna jukumu la kuhakikisha tunatoa huduma za kinga na tiba na kutoa elimu kwa umma ya kujikinga na magonjwa haya, na kuendesha programu za mafunzo kwa wataalamu na kufanya tafiti mbalimbali.
“Katika kutekeleza suala hilo, tumekuwa tukifanya uchunguzi wa awali kwa magonjwa ya saratani, awali tulikuwa tunafanya uchunguzi wa awali kwa saratani ya matiti, kizazi na tezidume.
“Lakini hivi karibuni tumeona kuna kasi ya ongezeko la wagonjwa wa saratani nyingine pia, hivyo tukaamua kuongeza huduma za uchunguzi wa awali,” alisema.
Alitaja huduma za uchunguzi wa awali zilizoongezwa kuwa ni uchunguzi wa awali wa saratani ya ngozi, hasa kwa wenye ulemavu wa ngozi, saratani ya kibofu cha mkojo, saratani ya ngozi, koo na homa ya ini ambayo isipogundulika mapema na kutibiwa huweza kusababisha saratani ya ini.
Alisema eneo jingine ambalo Serikali imewekeza ni upande wa tiba ambapo sasa wamepata mashine ya LINAC inayotibu kisasa zaidi magonjwa hayo katika mfumo wa 3D.
“Matokeo ya tiba kwa mashine hizi ni bora zaidi kuliko mashine ambazo tulikuwa tunazitumia hapo awali, tumeweza kupunguza muda wa mgonjwa kusubiri matibabu kutoka wiki sita hadi chini ya wiki nne,” alisema.
Alifafanua kwamba hapo awali mwaka 2015 wagonjwa walikuwa wanasubiria hadi wiki 12 kufanyiwa matibabu na hivyo kusababisha msongamano mkubwa.
“Haya ni mafanikio makubwa kwetu, kuweza kuendelea kupunguza muda wa wagonjwa kusubiri huduma,” alisema.
Naye Mkurugenzi wa Huduma za Kinga ORCI, Dk. Crispin Kahesa, alisema kufuatia maboresho mbalimbali yaliyofanywa na Serikali hospitalini hapo, idadi ya wagonjwa wanaopewa rufaa kwenda nje imepungua kutoka 146 hadi 44 kufikia mwaka jana.
“Changamoto tuliyonayo sasa ni kuendelea kuhamasisha jamii kujikinga dhidi ya magonjwa haya kwani Shirika la Afya Duniani (WHO) linaonya ikiwa hatua hazitachukuliwa idadi ya wanaougua itazidi kuongezeka kutoka watu milioni 18.1 hadi milioni 24 ifikapo 2035, duniani.
“Inakadiriwa takribani watu milioni 43.8 duniani wanaishi na saratani, kila mwaka inakadiriwa watu milioni 9.6 duniani hufariki kwa magonjwa haya, hapa nchini kila mwaka tunagundua wagonjwa wapatao 52,000 wa saratani,” alibainisha.
Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Saratani ORCI, Maguha Stephano, alisema maadhinisho ya Siku ya Saratani hufanyika Februari 4 kila mwaka.
“Hupewa kaulimbiu kwa kipindi cha miaka mitatu mitatu, kwa mwaka 2019 hadi 2021 inasema ‘Mimi Ninaweza, Nitapiga Vita Saratani’. Katika kuiadhimisha tunafanya uchunguzi wa awali bila malipo, tunawasihi wananchi wajitokeze,” alisema.