25.4 C
Dar es Salaam
Monday, November 18, 2024

Contact us: [email protected]

OBAMA AFURAHISHWA MAENDELEO YA KISIASA KENYA

SIAYA, KENYA


RAIS wa zamani wa Marekani, Barack Obama, amefurahishwa na maendeleo ya kisiasa yaliyopatikana nchini hapa, hasa baada ya Rais Uhuru Kenyatta na Kiongozi wa Upinzani, Raila Odinga kuweka tofauti zao pembeni ili kuijenga nchi.

Obama alieleza hayo wakati akizindua mradi wa kijamii huko Kogelo, Kaunti ya Siaya, ambako ndiko anakotoka baba yake, marehemu Mzee Hussein Obama.

Hata hivyo, Obama alisema kazi ngumu ingali bado mbeleni kuhakikisha jamii zinapatiwa fursa sawa kwa ajili ya nchi kukua na kustawi.

“Kuna maendeleo mazuri katika nchi hii ya ajabu. Pamoja na nyakati ngumu na tishio zinazojitokeza kila uchaguzi unapofanyika, sasa tuna rais na kiongozi mkuu wa upinzani walioahidi kujenga madaraja na kutoa kauli maalumu za kufanya kazi pamoja,” alisema.

Aliongeza kuwa pamoja na Kenya kuibuka kama nchi inayojiamini na kujitegemea, kuna mengi ya kufanya kushughulikia changamoto zilizobakia.

Alizitaja changamoto hizo kuwa ni pamoja na kung’oa mizizi ya rushwa, kugeuza ukabila kuwa ushirika na kuzichukulia tofauti za kijamii kama nguvu.

Obama alikuwa akizungumza wakati wa uzinduzi wa Kituo cha Rasilimali cha Sauti Kuu kilichoanzishwa na dada yake, Auma Obama ili kusaidia kuwaelimisha wakazi kuhusu kutumia vyema vipaji vyao.

Aidha alirudia kauli yake ya mwaka 2015 aliyoitoa kwenye Uwanja wa Kasarani jijini Nairobi wakati alipozuru hapa akiwa rais, akisema maendeleo nchini Kenya huhesabiwa pale Wakenya wachache wanaposafiri nje au hata kuhamia ng’ambo ili kupata elimu nzuri.

Mtazamo huo hasi alisema haukubaliki kwani vijana zaidi wanaweza kuwa na fursa nzuri kimaendeleo wakiwa hapa iwapo tu kutakuwa na sera nzuri kwa ajili yao.

Akiwa amevalia suruali rangi ya kijivu, miwani ya jua na shati jeupe la mikono iliyokunjwa, Obama aliwasili katika Kijiji cha Kogelo na msafara wa walinzi na magari ya kidiplomasia saa mbili na nusu asubuhi.

Alikuwa ametokea Uwanja wa Ndege wa Kimataifa Kisumu na kwenda moja kwa moja katika nyumba ya bibi yake, Sarah Obama.

Umati uliojazana kando ya barabara ulizuiwa kusonga mbele wakati magari yakielekea Kituo cha Sauti Kuu.

Baada ya kuzindua kituo hicho na kutembelea makazi yake ya asili ya Alego Nyang’oma katika Kaunti ya Siaya, Obama alielekea Afrika Kusini alikotarajia kutoa mhadhara wa 16 wa kila mwaka wa Nelson Mandela jijini Johannesburg.

Kabla ya kuwasili hapa juzi na kukutana na Rais Kenyatta Ikulu jijini Nairobi kisha na Raila katika Hoteli ya Villa Kempensiki, Obama alikuwa Tanzania kwa mapumziko ya siku nane akiwa na mkewe Michelle na binti zake Malia na Sasha.

Hata hivyo, kitendo cha Obama kutoambatana na familia yake katika ziara ya Kenya kumezua mjadala miongoni mwa Wakenya katika mitandao ya jamii.

Obama aliyetua Kenya juzi bila shamrashamra zilizoshuhudiwa mwaka 2015 wakati akiwa bado rais, pia hakuwa tayari kufuatiliwa na vyombo vya habari alipokuwa Tanzania.

Baada ya kutua kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta, alienda Ikulu jijini Nairobi kukutana na Rais Kenyatta kabla ya kuonana na Odinga katika Hoteli ya Villa Kempensiki, ambako wanahabari nako hawakuruhusiwa.

Wakati Wakenya wakijiuliza sababu za kutoonekana kwa Michelle na binti zake alioandamana nao kwenda Serengeti, alionekana akijiachia kwenye tamasha la muziki la Beyonce na Jay-Z jijini Paris, Ufaransa juzi. Alionekana akiwa na binti yake Sasha (17).

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles