RUTH MNKENI NA TUNU NASSOR, DAR ES SALAAM
ZOEZI la uwekaji wa alama ya X katika nyumba zilizojengwa mabondeni jana liliendelea, huku nyumba zaidi ya 3,000 zilizojengwa katika Bonde la Mto Msimbazi ziliwekewa X tayari kwa ajili ya kubomolewa.
Tangu kuanza kwa zoezi hilo la uwekaji wa alama hiyo katika nyumba zilizojengwa kando ya mto na kwenye hifadhi ya bahari, zaidi ya nyumba 5,000 zimeshawekewa X.
Kutokana na idadi hiyo huwenda nyumba zaidi ya 8,000 zikakumbwa na bomoabomoa inayotarajiwa kuanza leo katika maeneo mbalimbali jijini Dar es Salaam, baada ya kipindi cha wiki mbili kilichotolewa na Serikali kumalizika jana.
Akizungumza baada ya kumaliza zoezi hilo kwa Ofisa Mazingira Mwandamizi wa Baraza la Hifadhi ya Mazingira (NEMC), Arnold Kusiraga, alisema katika zoezi hilo wamefanikiwa kuweka alama ya X katika nyumba zaidi ya 3,000 kwa siku ya jana pekee.
Alisema tangu walipoanza wamefanikiwa kuzifikia nyumba takribani 5,500 ambazo zote zitaanza kubomolewa leo.
“Inavyoonekana nyumba zitakazovunjwa zitakuwa nyingi tofauti na makadirio ya kwanza kwani kwa sasa tumefanya kazi kama robo tu lakini nyumba ni nyingi na maeneo yaliyobaki bado ni mengi,”alisema Kusiraga.
Aliyataja maeneo ambayo wamefanikiwa kuwekwa alama ya X kuwa ni Jangwani, Kigogo Mbuyuni, Kigogo Sambusa, Mapera, Dampo na Buguruni Alhamza.
Hata hivyo alisema zoezi la kubomoa nyumba linaendelea leo katika maeneo ya Bonde la Mkwajuni hadi Daraja la Salender ambapo matingatinga yatakayobomoa yatakuwa matatu had manane.
Alisema zoezi la kuweka alama ya X litaendelea kwa siku ya leo kwa kuweka alama hizo kwenye maeneo ya Buguruni Kwamnyamani hadi Segerea.
Alisema maeneo mengine yatakayoathiriwa na bomobomoa hiyo ni wale waliojenga kandokando ya mito ambapo aliitaja baadhi ya mito hiyo kuwa ni Mto Msimbazi, Mzinga, Kizinga, Mto Ng’ombe, Tegeta, Mbezi, Mpiji, Mineva na Nyakasangwe.
Ulinzi waimarishwa
Kutokana na vurugu zilizotokea juzi wakati wa kuanza kwa zoezi hilo la kuweka X katika nyumba hizo za mabondeni, Jeshi la Polisi limelazimika kuimarisha ulinzi na kuwalinda maofisa hao wa NEMC pamoja na wale wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kuweza kuendelea na zoezi hilo.
Wakati wa zoezi hilo jana Jeshi la Polisi pamoja na wafanyakazi wa NEMC walilazimika kutembea kwa miguu kutoka Jangwani kuelekea Buguruni Alhamza kwenda na kurudi kutokana na kuwa maeneo hayo hakuna barabara za kupita magari kwa sababu ya ubovu wa miundombinu.
Polisi hao walionekana kupita kila kona huku wakiwa na mabomu ya machozi pamoja na bunduki hali ambayo ilisababisha wananchi kuanza kuzungumza maneno ya kejeli dhidi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Wakati zoezi hilo linaendelea wapo baadhi ya askari waliokuwa wakizunguka maeneo ya Kigogo Mbuyuni, ili kuhakikisha kwamba wananchi hawafanyi vurugu zozote kama kuchoma matairi na kufunga barabara.