LONDON -UINGEREZA
SASA ni wazi kwamba nyota ya Boris Johnson anayewania kiti cha Uwaziri Mkuu wa Uingereza imezidi kung’ara baada ya kuungwa mkono na mmoja wa wapinzani wake.
Kampeni za Boris sasa zimepata nguvu mpya baada ya kuungwa mkono na mmoja wa wapinzani wake Matt Hancock ambaye ni Waziri wa Afya.
Katika raundi ya kwanza ya mchujo Boris aliongoza dhidi ya wagombea 10 wa nafasi hiyo kwa kupata kura 144.
Jana Hancock alisema Meya huyo wa zamani wa jiji la London anayepigia upatu hatua ya kuachana na Umoja wa Ulaya, ndiye mgombea bora wa kukiunganisha chama na anaweza kutimiza ajenda hiyo.
Hatua ya Waziri Hancock imekuja baada ya Boris kukataa kushiriki katika mdahalo wa telesheni pamoja na wapinzani wake watano waliobaki jumapili.
Chama cha Conservative kinamfatuta atakayerithi nafasi ya kukiongoza chama iliyoachwa wazi na Theresa May mwanzoni mwa mwezi huu baada ya mpango wake wa Brexit alioufikia na viongozi wa Ulaya kushindwa kuungwa mkono bungeni mjini London.