Na THERESIA GASPER-DAR ES SALAAM
SIMBA imeendeleza vurugu zake katika usajili wa msimu ujao wa Ligi Kuu Tanzania Bara, baada ya kufanikiwa kuwasajili beki, Erasto Nyoni na kipa Said Mohamed, huku Yanga ikifanikiwa kumsainisha mkataba mpya kiungo wake, Thaban Kamusoko.
Nyoni ambaye ni beki wa kulia amemaliza mkataba wake wa kuitumikia Azam FC kama ilivyo kwa Nduda ambaye mkataba wake wa kuichezea Mtibwa Sugar ulimalizika msimu uliopita wa Ligi Kuu Tanzania Bara.
Wekundu hao wa Msimbazi, Simba, walikamilisha usajili wa mikataba ya miaka miwili kwa nyota hao ambao pia wanaichezea timu ya Taifa ‘Taifa Stars’ jana baada ya pande zinazohusika kufikia mwafaka.
Nyoni amekuwa akisifika kutokana na uwezo wake mkubwa wa kucheza namba zaidi ya moja na usajili wake unachukuliwa kama tahadhari endapo beki Shomari Kapombe aliyejiunga pia na timu hiyo akitokea Azam FC hatapona kwa wakati majeraha yanayomsumbua.
Kwa upande wa Mohammed, anakuwa kipa wa tatu kusajiliwa na Wekundu hao msimu huu baada ya klabu hiyo awali kuwanasa, Aishi Manula kutoka Azam na Emmanuel Mseja aliyesajiliwa akitokea Mbao FC.
Usajili wa makipa hao watatu una maana makipa, Daniel Agyei na Manyika Peter muda wao wa kuondoka katika klabu hiyo umewadia.
Wakati huo huo, mvutano wa muda mrefu kati ya Yanga na Kamusoko hatimaye umemalizika baada ya kiungo huyo wa kimataifa wa Zimbabwe kusaini mkataba mwingine wa miaka miwili.
Wakati huo huo, Singida United imeendelea kufanya yake baada ya jana kufanikiwa kumsajili kipa, Ally Mustapha ‘Barthez’ ambaye amemaliza mkataba wa kuitumikia Yanga.
Mwenyekiti wa Singida United, Festo Sanga, alisema klabu hiyo imemsajili kipa huyo ikiamini ataisaidia timu hiyo kufikisha malengo ya kufanya vizuri katika Ligi Kuu Tanzania Bara msimu ujao.
“Tumeingia mkataba wa miaka miwili na Barthez, kwani tumeona ana uwezo mzuri wa kuisaidia timu yetu ikafikia malengo ya kufanya vizuri katikia ligi kuu msimu ujao,” alisema.