24.7 C
Dar es Salaam
Saturday, April 13, 2024

Contact us: [email protected]

Nyerere na udhaifu wa viongozi nchini

yeye-001

Na Markus Mpangala,

LEO kitabu chetu kinaitwa ‘Uongozi Wetu na Hatima ya Tanzania’ kilichoandikwa na Rais wa Awamu ya Kwanza, Julisu Nyerere na kuchapishwa na Kampuni ya Mkuki na Nyota ya jijini Dar es Salaam. Kimepewa nambari ISBN 978-9987-753-42-0.

Kitabu hiki kimebadilishwa kabisa muundo na kumwezesha msomaji kukibeba kwenye mfuko wa suruali (kwa wanaume) au kiganjani kama simu. Ni maboresho makubwa.

Zipo kurasa 90 zilizogawanywa katika maeneo 25 yanayoelezea sakata zima la uongozi wetu chini ya Chama Cha Mapinduzi (CCM). Nyerere anaelezea Ripoti ya Jaji Nyalali, Dodoma (1992), Kikao cha Halimashauri Kuu Butiama mwaka 1993 na matukio mengine yaliyofanikisha uandikwaji wa kitabu hicho.

Maudhui yake ni; nafasi ya Zanzibar kwenye Jumuiya ya Kiislamu (OIC), Kurejeshwa kwa serikali ya Tanganyika (kampeni ya kundi la G55), Muundo wa Muungano (idadi ya serikali), uamuzi wa vipindi vya urais na mikakati ya siri ya kumwongezea muda wa kubaki madarakani, nafasi ya makamu wa pili wa rais (mgombea mwenza), mfumo wa vyama vingi vya siasa nchini na mengineyo.

Mwalimu Nyerere ameelezea ripoti ya Jaji Nyalali kuhusiana na mabadiliko ya kisiasa kutoka kwenye chama kimoja kwenda chama kingine. Nyerere kama Baba wa Taifa anaonyesha umahiri wa kuwoangoza wanasiasa na viongozi wa taasisi mbalimbali namna ya kuwa thabiti kwenye mambo mazito. Mathalani, Nyerere alijidhihirisha kukubaliana na pendekezo la Watanzania wachache kutaka vyama vingi vya siasa huku wengi wakipinga.

Anasema; “Lakini Kamati ikapendekeza kwamba kutokana na historia ya nchi yetu itafaa chama kikiteua mgombea mwenza wake kutoka upande wa pili wa Muungano; katiba iseme hivyo. Watu wengi, mimi nikiwa miongoni mwao waliona kuwa mapendekezo haya ni mazuri. Lakini tukawa tukisikia minong’ono kwamba ‘Wazanzibari’ hawapendi pendekezo hil la kupata Makamu wa Rais kwa njia ya kuwa mgombea mwenzi,” (uk.8).

Nyerere anadhihirisha kuwa alikuwa jabali na kiongozi madhubuti pale anaposema kuwa haikuwa jambo zuri kwa wananchi wa Zanzibar peke yao kumchagua makamu wa rais (kulingana na utaratibu wa awali).

Nyerere anatukumbusha kikao cha faragha cha Desemba mwaka 1992. Anatueleza kuwa Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM iliketi kuzungumzia masuala mbalimbali ambapo aliombwa kuhudhuria.  Anasema Rais Mwinyi alikubaliana na vipindi vya urais vitamkwe kwenye katiba, lakini palikuwa na jaribio la kumwongezea muda Rais Mwinyi.

“Rais alieleza kuwa walikuwa wamekubaliana kwamba vipindi vya kuwa Rais ni lazima vitamkwe, lakini walikuwa hawajafikia uamuzi viwe vipindi vingapi. Awali baadhi ya viongozi wa chama walikuwa wameanza kampeni za kutaka Rais Mwinyi aongezewe vipindi vya muda wa kuwa Rais. Nilipotambua hivyo nilikuwa nimekwenda mara moja kwa Rais na kumsihi azizime kampeni hizo; na viongozi wahusika nilitafuta nafasi nao nikawaomba wasilifufue jambo hili. Nikadhani tumeelewana hivyo. Kwahiyo nilishtuka niliposikia kuwa kumbe suala hilo la vipindi vya urais bado linazungumzwa, na ati bado uamuzi wa vipindi vingapi haujafikiwa!” (uk.9).

Anaendelea, “Suala hili lilikwishakuamuliwa zamani na sasa ni sehemu ya Katiba yetu. Uamuzi huo inafaa uheshimiwe. Rais Mwinyi ndiye Rais wa kwanza kuchaguliwa kwa mujibu wa katiba hiyo. Yeye alisema kuwa vipindi viwili havitoshi, na akataka viwe vitatu; Rais wa pili atasema vipindi vitatu havitoshi na atataka viwe vinne na kadhalika mpaka tufikie Ngwazi wa Tanzania (uk.10).

Ni kwa vipi Nyerere aliyestaafu alisumbuliwa mara kwa mara kutoa ufananuzi au kukabiliana na joto la kisiasa ndani ya chama na serikali? Ni wazi kuwa CCM na wanachama wake walitakiwa kuwa imara bila Mwalimu Nyerere.

Lilikuwa jambo lenye busara kumtegemea Nyerere kutoa mwongozo wa hekima, lakini lilikuwa jambo la hasara kumtegemea kupitiliza. Kwamba CCM na viongozi wa serikali walitakiwa kufahamu kuwa upo wakati ambao hatutakuwa naye.

Kitabu hiki kina mawaidha mengi yenye elimu katika uongozi wa taasisi mbalimbali, mamlaka za uteuzi, misingi na mwelekeo wa kampuni ama vyama vya siasa. Ni kitabu kinachofaa kwa wataalamu wa sayansi ya siasa na wapenzi wa vitabu ili kujipatia historia yakinifu.

0787 558 448

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles