Na Aziza Masoud-Dar es Salaam
BODI ya Nyama Tanzania imetoa tahadhari kwa wananchi na kuwataka kuacha kula nyama inayouzwa ikiwa imewekwa kwenye ndoo au kupangwa kwenye meza za mabucha kwa sababu si salama kwa afya.
Vilevile imewataka wauza nyama kwenye mabucha kuacha kukata nyama kwa kutumia magogo kwa vile wanahatarisha usalama wa walaji.
Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Ofisa Nyama wa Bodi hiyo, Edgar Mbio, alisema nyama hiyo na ile inayokaa buchani zaidi ya saa nne.
Mbio alisema kwa utaalamu nyama kama hiyo inakosa sifa ya kuwa na ubora unaofaa kwa matumizi ya binadamu.
“Biashara ya mifugo hufanyika machinjioni na buchani, hatutegemei kuona kinyume na hapo.
“Watu wanaonunua nyama kwenye meza… ndoo hizi ndizo zinazoleta madhara kwa sababu hazijakaguliwa, pia wale wanaonunua nyama ambayo imeshinda inanig’inia buchani nayo inakuwa imeshapoteza ubora kwa kuwa kwa kawaida nyama inapaswa kuhifadhiwa si zadi ya saa nane,” alisema Mbio.
Alisema wapo pia ambao hununua nyama katika bucha ambayo wanatumia vibao kukatia navyo si salama kwa sababu muuzaji anapokata anaacha ubora wa kitoweo hicho kwenye kibao.
Alisema mtu yeyote anayekula nyama iliyochinjwa na kuhifahiwa holela lazima apate madhara kwa kuwa inakuwa si bora na salama hivyo haifai kwa matumizi ya binadamu.
Ofisa huyo alisema bodi ya nyama inaamini nyama bora na salama inaanzia kwa mfugaji kwa kufauta kanuni za ufugaji bora zinazofuata taratibu ikiwamo kuuza ng’ombe wa umri chini ya miaka kumi.
Awali, Kaimu Msajili wa Bodi hiyo, Imani Sichalwe aliwataka wananchi kuongeza kasi ya kula nyama ili kufikia kilo 50 kwa mwaka kwa kila mmoja.
Mbio alisema hicho ndicho kiwango kilichopendekezwa na Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO).
Alisema takwimu zinaonyesha kila mwananchi nchini kwa kwa sasa anakula kilo 15 tu ya nyama kwa mwaka hivyo kuwa na tofauti ya kiko 35 kwa kila mlaji.
“Tunakula nyama kwa kiwango cha chini ikilinganishwa na mahitaji yanayopaswa ndani ya miili yetu.
“Pamoja na hali ya uzalishaji wa nyama nchini kuwa juu lakini bado watu hawali nyama,” alisema Sichalwe.
Alisema uchunguzi uliofanywa na bodi umebaini hali hiyo inatokana na bidhaa hiyo kuuzwa kwa bei ghali ambayo kwa wastani huuzwa kuanzia Sh 6,000 hadi Sh 15,000 kwa kilo moja.
Alisema ili kuboresha ulaji wa nyama bodi imeanza kuhamasisha utumiaji wa mizani za digitali ambao utamuwezesha mlaji kununua kulingana na uwezo.
“Hii mizani itawaisaidia wananchi ambao wanahitaji kula nyama lakini hawana fedha za kununua kwa bei ya kiwango cha mizani iliyopo sasa.
“Mfano mwenye bucha akiwa na mzani wa digitali anaweza kumuuzia mlaji nyama hata ya Sh 500, tunaamini tutaongeza idadi ya walaji kwa njia hii,” alisema Sichalwe.
Alisema kwa mujibu wa bajeti ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Tanzania ni nchi ya pili ikifuatiwa na Ethiopiakwa mifugo mingi.
Kwa sasa nchi ina ng’ombe wapatao milioni 30.5, mbuzi milioni 18.8, kondoo milioni 5.3, kuku wa asili milioni 38.2, kuku wa kisasa milioni 36.6, nguruwe milioni 1.9 na punda 595,160.
Alisema bajeti hiyo imeonyesha pia uzalishaji nyama nchini mwaka 2017/18 ulikuwa tani 679,992 za nyama ya ng’ombe, mbuzi, kondoo na nguruwe.
“Kati ya tani 2,608.93 za nyama, tani 1,030.78 ni za ng’ombe, tani 1,248.14 mbuzi, kondoo tani 50.00 na punda tani 280.00 ziliuzwa nje ya nchi,” alisema Sichalwe.
Alisema tani 1,224.55 za nyama ikiwamo nguruwe tani 506.05, ng’ombe tani 711.03 na kondoo tani 7.47 ziliingizwa ndani ya nchini.