23.2 C
Dar es Salaam
Sunday, March 26, 2023

Contact us: [email protected]

Nyama inayouzwa kwenye ndoo si salama-Bodi

Na Aziza Masoud-Dar es SalaamBODI ya Nyama Tanzania imetoa tahadhari kwa wananchi na kuwataka kuacha kula nyama  inayouzwa ikiwa imewekwa kwenye ndoo au kupangwa kwenye meza za mabucha kwa sababu  si salama kwa afya.

Vilevile imewataka wauza nyama kwenye mabucha kuacha kukata nyama kwa kutumia magogo kwa vile    wanahatarisha usalama wa walaji.

Akizungumza na waandishi wa habari   Dar es Salaam jana, Ofisa Nyama wa Bodi hiyo, Edgar Mbio, alisema  nyama hiyo na ile inayokaa buchani zaidi ya saa nne.

Mbio alisema kwa utaalamu nyama kama hiyo inakosa sifa ya kuwa na ubora unaofaa kwa matumizi ya binadamu.

“Biashara ya mifugo hufanyika machinjioni na buchani, hatutegemei kuona kinyume na hapo.

“Watu wanaonunua nyama kwenye meza… ndoo hizi ndizo zinazoleta madhara kwa sababu hazijakaguliwa, pia wale wanaonunua nyama ambayo imeshinda inanig’inia buchani nayo inakuwa imeshapoteza ubora kwa kuwa kwa kawaida nyama inapaswa kuhifadhiwa si zadi ya saa nane,” alisema Mbio.

Alisema wapo pia ambao hununua nyama katika  bucha  ambayo wanatumia vibao kukatia navyo si salama kwa sababu muuzaji anapokata anaacha ubora wa kitoweo hicho kwenye kibao.

Alisema mtu yeyote anayekula nyama iliyochinjwa na kuhifahiwa holela lazima apate madhara  kwa kuwa inakuwa si bora na salama hivyo haifai kwa matumizi ya binadamu.

Ofisa huyo alisema bodi ya nyama inaamini nyama bora na salama inaanzia kwa mfugaji kwa kufauta kanuni za ufugaji bora  zinazofuata taratibu ikiwamo kuuza  ng’ombe wa umri  chini ya miaka kumi.

Awali, Kaimu Msajili wa Bodi hiyo,  Imani Sichalwe aliwataka wananchi kuongeza kasi ya kula  nyama ili kufikia kilo 50 kwa mwaka  kwa kila mmoja.

Mbio alisema hicho  ndicho kiwango kilichopendekezwa na Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO).

Alisema takwimu zinaonyesha kila mwananchi nchini kwa kwa sasa anakula kilo 15 tu ya nyama  kwa mwaka hivyo   kuwa  na tofauti ya kiko 35  kwa kila mlaji.

“Tunakula nyama kwa kiwango cha chini ikilinganishwa  na  mahitaji yanayopaswa  ndani ya miili yetu.

“Pamoja na hali ya uzalishaji wa nyama nchini kuwa juu lakini bado watu hawali nyama,” alisema Sichalwe.

Alisema uchunguzi uliofanywa na bodi umebaini hali hiyo inatokana na bidhaa hiyo kuuzwa kwa bei ghali ambayo kwa wastani huuzwa kuanzia Sh 6,000 hadi Sh 15,000 kwa kilo moja.

Alisema ili kuboresha ulaji wa nyama bodi  imeanza kuhamasisha utumiaji wa mizani za digitali ambao utamuwezesha mlaji kununua kulingana na uwezo.

“Hii mizani itawaisaidia wananchi ambao wanahitaji kula nyama lakini  hawana fedha za kununua  kwa bei ya kiwango cha mizani iliyopo sasa.

“Mfano mwenye bucha akiwa na mzani wa digitali anaweza kumuuzia mlaji nyama hata ya Sh 500, tunaamini tutaongeza idadi ya walaji kwa njia hii,” alisema Sichalwe.

Alisema  kwa mujibu wa bajeti ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi,   Tanzania ni nchi ya pili  ikifuatiwa na Ethiopiakwa mifugo mingi.

Kwa sasa nchi  ina   ng’ombe wapatao  milioni 30.5, mbuzi milioni 18.8, kondoo milioni 5.3, kuku wa asili milioni 38.2, kuku wa kisasa milioni 36.6, nguruwe milioni 1.9  na punda 595,160.

Alisema bajeti hiyo imeonyesha pia  uzalishaji nyama nchini   mwaka 2017/18  ulikuwa  tani 679,992  za nyama ya ng’ombe, mbuzi, kondoo na nguruwe.

“Kati ya  tani 2,608.93 za nyama, tani 1,030.78 ni za ng’ombe, tani 1,248.14 mbuzi, kondoo tani 50.00 na punda tani 280.00 ziliuzwa nje ya nchi,” alisema Sichalwe.

Alisema   tani 1,224.55 za nyama  ikiwamo nguruwe tani 506.05, ng’ombe tani 711.03 na kondoo tani 7.47 ziliingizwa ndani ya nchini.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
211,184FollowersFollow
564,000SubscribersSubscribe

Latest Articles