Na VERONICA ROMWALD – DAR ES SALAAM
INAWEZEKANA wewe ni miongoni mwa watu wanaopenda kuongeza chumvi kwenye chakula pindi kinapokuwa kimetayarishwa mezani tayari kwa kuliwa.
Watu wengi hasa walaji wa nyama choma na chipsi hupendelea kuongeza chumvi mezani kwa madai kwamba chakula hakijakolea ladha ile wanayoihitaji.
Wataalamu wanaeleza kuwa chumvi ni kiungo muhimu katika chakula kwani licha ya kuongeza ladha ina ‘utajiri’ mkubwa wa madini ya sodium chloride ambayo huhitajika mno mwilini.
Wanataja faida za chumvi kuwa ni pamoja na kuweka sawa hali ya maji mwilini (fluid balance), husaidia katika kuweka sawa mtiririko wa mapigo ya moyo (heart rhythm) pia husaidia katika kutanuka na kusinyaa kwa kisuli (contract and relaxation of muscles).
Lakini wanasema ili mtu apate faida hizo ndani ya mwili wake chumvi inapaswa kupikwa jikoni na kuiva pamoja na chakula na si kuongeza mezani.
Wanasema kitendo cha kuongeza chumvi mezani (mbichi) ni cha hatari na kwamba husababisha mtu kupata magonjwa mbalimbali hasa shinikizo la juu la damu katika maisha yake.
Anasema uwezekano wa mtu kupata shinikizo la juu la damu kutokana na ulaji mbovu wa vyakula hasa vilivyoandaliwa kwa kutumia mafuta mengi ni mkubwa.
“Chipsi hupikwa kwa kutumia mafuta mengi na kawaida watu wanapokula huweka chumvi nyingi pamoja na wale wanaokula nyama choma hutumia chumvi nyingi, ulaji huo si mzuri na si salama kiafya.
Anasema tafiti zinaonesha watu weusi (Waafrika) tunapenda zaidi kutumia chumvi nyingi tofauti na watu wa mabara mengine.
“Mbaya zaidi inaonekana miili yetu ina inapokea haraka mno ile chumvi inayoingia mwilini ikilinganishwa na wenzetu weupe, hivyo kutusababishia madhara,” anasema.
Anasema mtindo wa maisha wa sasa unachangia kwa kiwango kikubwa watu kupata magonjwa ya moyo kuliko mtindo wa maisha wa kale.
“Wengi leo hii hatufanyi mazoezi, muda mwingi tunakaa maofisini, tunatumia usafiri wa bodaboda na magari kutoka sehemu moja kwenda nyingine, matumizi ya sigara na pombe ni ya kiwango kikubwa na ulaji wetu si mzuri kwa ujumla, mambo haya yanachochea kuongezeka kwa magonjwa ya moyo hasa shinikizo la juu la damu,” anasema.
Wengi hufa kimya kimya
Anasema hivi sasa ulimwenguni magonjwa ya moyo ndiyo yanayongoza kusababisha vifo vya watu wengi.
“Wakati mwingine mtu anaweza asigundue kama shinikizo lake la damu lipo juu, inawezekana kabisa asione hata dalili yoyote, haumwi kichwa wala miguu,” anasema.
Anaongeza; “Wengi huja hospitalini wakiwa tayari moyo haufanyi kazi sawa sawa au figo zimeharibika, tunapowapima tunagundua kuwa wana shinikizo la juu la damu, ndiyo maana ugonjwa huu unaitwa ‘silent killer’ kwa sababu unakula taratibu ndani ya mwili wako.
Tafiti
Daktari huyo anasema tafiti zinaonesha kuwa zaidi ya theluthi moja ya vifo vyote duniani hutokana na magonjwa yanayohusishwa moja kwa moja na moyo.
Anasema kati ya hiyo theluthi moja magonjwa ya moyo zaidi ya asilimia 50 yanatokana na shinikizo la juu la damu (hypertension).
“Katika miaka ya nyuma tatizo lilikuwa zaidi katika nchi zilizoendelea lakini katika miaka ya hivi karibuni kulingana na tafiti mbalimbali zinazoendelea kufanyika inaonekana tatizo lipo zaidi katika nchi zinazoendelea.
Anasema inaonekana shinikizo la juu damu ni namba moja kwa kusababisha magonjwa ya moyo katika nchi zilizopo Kusini mwa Jangwa la Sahara, Tanzania ikiwamo.
“Tafiti moja kubwa iliyofanywa katika nchi 23 barani Afrika ilionesha katika nchi zote hizo, shinikizo la damu linashika namba moja kwa kusababisha moyo kushindwa kufanya kazi na vifo vya ghafla,” anasema.
Anasema katika nchi hizo zilizofanyiwa utafiti huo (Tanzania ikiwamo) ilionekana asilimia 86 ya magonjwa yote ya moyo hutokana na shinikizo la damu.
Hali ilivyo JKCI
Daktari huyo ambaye pia ni Mkuu wa Idara ya Utafiti na Mafunzo wa JKCI anasema tafiti zilizofanywa na taasisi hizo zinaonesha tatizo ni kubwa katika jamii.
“JKCI tumewahi kufanya tafiti miaka mitatu iliyopita, ambazo zilihusisha jamii moja kwa moja na wagonjwa waliolazwa wodini, tumebaini tatizo ni kubwa.
“Kwenye tafiti zilizohusisha jamii asilimia kati ya 42 hadi 56 ya watu tuliowapima walikuwa na shinikizo la juu la damu,” anasema.
Anaongeza; “Asilimia 35 hadi 47 ya wagonjwa waliokuwa wamelazwa wodini ambao mioyo yao ilikuwa ime-fail (imeshindwa kusukuma damu sawa sawa), tulibaini kisababishi kikuu ni shinikizo la juu la damu.
Vijana hatarini
Anasema wakati katika nchi zilizoendelea tatizo hilo likijulikana kama ni ugonjwa wa watu wazima hali ni tofauti katika nchi zinazoendelea kwani linawakumba zaidi vijana.
“Katika nchi zilizoendelea watu wanaokutwa na shinikizo la juu la damu ni wale wenye umri wa kuanzia miaka 50 na kuendelea, lakini katika nchi zinazoendelea hasa kusini mwa jangwa la sahara wanaokutwa na tatizo hilo ni wale wenye umri wa kuanzia miaka 35 hadi 45, ambao kimsingi ni umri wa uzalishaji,” anasema.
Je, watoto nao wanaugua
Anasema watoto nao hupata shinikizo la juu damu lakini mara nyingi hali hiyo hutokea iwapo wamepata maradhi mbalimbali ikiwamo saratani.
“Tatizo hili limegawanywa katika makundi mawili kuna ‘primary hypertension’ na ‘secondary hypertension’. Tunaposema ‘secondary hypertension tunamaanisha kwamba kunakuwa na kisababishi kingine ambacho kinasababisha mtu kupata shinikizo la juu la damu.
“Kwa mfano saratani au mvurugiko wa homoni kwenye damu na mara nyingi hii ndiyo ambayo huwakumba watoto na kusababisha kupata shinikizo la juu la damu,” anasema na kuongeza:
“Lakini tunaposema ‘primary hypertension’ mara nyingi huwakumba zaidi watu wazima, yaani hapa tunampima mgonjwa lakini tunakuta hakuna tatizo lolote ambalo limesababisha wao kupata shinikizo la juu la damu. Asilimia 95 ya pressure zote ni primary hypertension.”
Anasema hata hivyo watoto ni nadra mno kupata tatizo hilo na kwamba kwa mwaka huwa wanawapokea watoto watano wenye shinikizo la juu la damu ikilinganishwa na watu wazima 400 hadi 500 ambao hufika katika taasisi hiyo wakisumbuliwa na shinikizo la juu la damu.
Matibabu
Anasema si rahisi kutibu shinikizo la juu la damu kwani mgonjwa hulazimika kutumia dawa siku zote za maisha yake tangu anapogundulika kuwa na tatizo hilo.
“Matibabu ya shinikizo la damu pamoja na kuwa yanajulikana na dawa zimethibitishwa kisayansi lakini ni miongoni mwa magonjwa ambayo hayatibiwi kisahihi, hii ni changamoto,” anasema.
Anasema changamoto hiyo ipo zaidi katika nchi zinazoendelea ambapo tafiti zinaonesha asilimia 18 ya watu wenye tatizo hilo katika nchi zinazoendelea ndiyo ambao hutumia dawa ikilinganishwa na asilimia 87 katika nchi zilizoendelea.
“Na katika hao asilimia 18 waliopo kwenye dawa ni asilimia sita tu ndiyo ambao wameweza ku-contral pressure zao, hawa wanazingatia matibabu yao.
“Katika nchi zilizoendelea watu hugundulika mapema na kuanza tiba lakini nchi zinazoendelea ni tofauti wengi huja hali ikiwa mbaya, hivyo kuna mambo mawili hapa, moja ni watu kuchelewa hospitalini na watu kutozingatia matibabu na masharti ya chakula wanayopewa na watalaamu,” anasema.
Wengi hawamudu gharama
Daktari huyo anasema gharama za kutibu tatizo hilo ni kubwa iwapo mtu hana bima yoyote.
“Nimesema awali kwamba mtu mwenye ugonjwa huu analazimika kumeza dawa kila siku tangu alipokutwa na tatizo, kwa kuwa matibabu ni ghali, changamoto tunayoona ni baadhi ya wagonjwa wetu ambao hawana bima wanafika mahali wanashindwa kugharimia matibabu yao,” anasema.
Anasema matibabu yenyewe hutegemeana na idadi ya dawa ambazo mgonjwa huandikiwa kulingana na kiwango cha shinikizo la damu alichonacho.
“Mgonjwa hupewa dawa kulingana na kiwango cha ‘presha yake, kuna ambao hutakiwa kutumia kidonge kimoja au viwili kwa siku, ikiwa juu hulazimika kutumia vidonge vitatu, vinne au hata vitano kwa siku ili kuiweka sawa.
“Sasa unaweza kukuta kidonge kimoja ni Sh 200 na kama hicho hakimsaidii anaweza kuandikiwa kidonge kimoja cha Sh 1,000, akitakiwa kumeza hicho cha Sh 200 kwa siku maana yake anahitaji kuwa na Sh 60,000 kwa mwezi apate dozi kamili, wengi wanashindwa kumudu gharama hizo,” anasema.
Anasema kutokana na hali hiyo wanakuwa hawatumii dozi kama inavyopaswa jambo ambalo ni la hatari.
“Kwa kawaida hakuna kikomo cha matumizi ya dawa, huu ni ugonjwa wa kudumu, kila siku mtu anapaswa kutumia dawa ingawa anaweza kufika mahali akapunguziwa dozi na daktari wake iwapo presha yake inakuwa imeshuka na hapo ndipo zile gharama za matibabu nazo zinapungua,” anafafanua.
Elimu ni ndogo
Daktari huyo anasema jamii bado haina uwelewa wa kutosha juu ya tatizo hilo.
“Wengi hawana mwamko wa kuchunguza afya zao, ndiyo maana wanaletwa hospitalini wakiwa shinikizo la damu limefika 200 na zaidi na tayari wamepata madhara makubwa,” anasema.
Madhara
Anasema wapo ambao hufikishwa hospitalini macho yakiwa hayaoni, moyo hausukumi damu sawa sawa, wana kiharusi au figo hazifanyi kazi sawa sawa.
“Na wale wanaokuwa hawatumii dawa inavyotakiwa wapo kwenye hatari ya kupata madhara haya katika siku za usoni,” anabainisha.
Kuhusu shinikizo la chini la damu
Daktari huyo anasema tatizo hili haliwapati watu wengi ikilinganishwa na shinikizo la juu la damu.
“Kwa mwezi hapa JKCI tunaweza kupokea watu 10 wanaosumbuliwa na shinikizo la chini la damu kuliko wale wenye shinikizo la juu ambao wanaweza kufikia zaidi ya 200, watu wenye shinikizo la chini la damu matibabu yao ni rahisi mara nyingi wakitundikiwa dripu ya maji hurejea katika hali ya kawaida,” anasema.
Kuhusu maadhimisho
Anasema kutokana na hali hiyo, Shirika la Afya Duniani (WHO) ilichagua Mei 17, kila mwaka kuwa Siku ya Mapigo ya Moyo Duniani.
“WHO ilitenga siku hii ili kuelimisha jamii kuhusu madhara ya shinikizo la damu na watu wapate fursa ya kuchunguza afya zao ili wale wanaogundulika waanze kupata matibabu mapema,” anasema.