33.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, November 26, 2024

Contact us: [email protected]

Nyalandu awaonya wanaokiuka sheria

nyalanduNA MWANDISHI WETU, BUSEGA
WAZIRI wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu, amesema atawachukulia hatua watendaji wa wizara yake wanaofanya kazi kwa kukiuka sheria za kazi.
Amesema kwamba, kama watumishi hao wanadhani hana mamlaka ya kuwachukulia hatua, wanatakiwa kujua uwezo huo anao kwa mujibu wa sheria.
Kutokana na hali hiyo, amewataka wananchi wakiwamo wafugaji, wamfikishie taarifa sahihi za watendaji wanaokiuka sheria kwa kuwatoza faini kinyume cha sheria ili aweze kuwachukulia hatua.
Nyalandu aliyasema hayo juzi mjini Lamadi, Wilaya ya Busega, Mkoa wa Simiyu alipokuwa akihutubia mkutano wa wafugaji kutoka mikoa mbalimbali nchini.
“Hakuna mtendaji wa wizara yangu aliye juu ya sheria, unyanyasaji na rushwa ni makosa ya jinai na kamwe sitakubali yawepo ndani ya taasisi za wizara ninayoiongoza.
“Lazima kila mtendaji afuate sheria na anayekiuka nina mamlaka ya kumuondoa wakati wowote na kama wanabisha waendelee tu.
Nyalandu aliyasema hayo baada ya wafugaji kumwambia kwamba wanaonewa na baadhi ya watendaji wa wizara yake wakiwamo wahifadhi na askari wa wanyamapori.
Naye Katibu Mkuu wa Chama cha Wafugaji Tanzania, Magembe Makoye, alisema matukio ya wafugaji kunyanyaswa yameshika kasi kwa kuwa hakuna hatua za kisheria zinazochukuliwa dhidi ya wanaokiuka sheria.
“Ng’ombe wanakamatwa, wanapigwa risasi ndani na nje ya hifadhi na watendaji wanajigamba hakuna wa kuwakataza. Kwa hiyo, tunaomba mheshimiwa waziri ulifanyie kazi suala hili,” alisema Makoye.
Naye Waziri wa Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi, Dk. Titus Kamani, amesema watendaji wa wizara yake wanaozuia mifugo isisafirishwe nje ya nchi wanahujumu uchumi wa Taifa.
“Ni uhujumu uchumi kwa mtumishi wa umma kuzuia mifugo isisafirishwe nje ya nchi wakati mhusika amefuata taratibu zote ikiwa ni pamoja na kumiliki vibali halali vya Serikali.
“Pamoja na kwamba ni kosa kuzuia mifugo isisafirishwe wakati kuna vibali maalumu, hata nyinyi mnaosafirisha mifugo kwa njia za panya acheni kwani na nyie mnakiuka sheria,” alisema Dk. Kamani alipokuwa akizungumza kwenye mkutano huo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles