Na THERESIA GASPER-DAR ES SALAAM
KOCHA Msaidizi wa Yanga, Shadrack Nsajigwa, amesema makosa madogo waliyofanya ndiyo yaliwagharimu na kujikuta wakipoteza mchezo dhidi ya wapinzani wao, Simba.
Yanga juzi ililala bao 1-0 kutoka kwa Simba katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara uliopigwa Uwanja wa Taifa Dar es Salaam.
Akizungumza baada ya mchezo huo kumalizika, Nsajigwa, aliyataja makosa hayo kuwa ni pamoja na kadi nyekundu aliyolimwa beki wa timu hiyo, Hassan Kessy.
“Kupoteza mchezo ni moja ya matokeo, hivyo kwa sasa tunaangalia tulikosea wapi na kusonga mbele kwa kuangalia michezo inayotukabili mbele yetu,” alisema.
Akizungumzia uamuzi wake uliolalamikiwa na mashabiki wa timu hiyo wa kumtoa kiungo, Papy Tshishimbi na winga Emmanuel Martin, alisema alifanya hivyo baada ya kubaini alikuwa amechoka na kudai hali hiyo ilitokana na mchezaji huyo kutoka kwenye majeraha.
“Tumeona makosa yaliyojitokeza hivyo kwa sasa tunaenda kuyafanyia kazi kabla ya kuelekea katika mechi zinazotukabili mbele yetu,” alisema.
Yanga kwa sasa inashika nafasi ya tatu katika msimamo wa ligi kuu, ikiwa imejikusanyia pointi 48, baada ya kucheza michezo 24, ikishinda 13, sare tisa na kupoteza miwili.