FRANCIS GODWIN Na RAYMOND MINJA – IRINGA
SAA chache baada ya kuachiwa huru na Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Iringa, aliyekuwa Mwenyekiti wa Mtandao wa Wanafunzi Tanzania (TSNP), Abdul Nondo, ameeleza magumu aliyopitia wakati akitetea wanafunzi huku akiwa anaendelea na kesi yake ya kudaiwa kujiteka.
Hukumu hiyo ya kesi ya jinai namba 13 ya mwaka 2018 ilitolewa jana na Hakimu Mfawidhi, Liad Chemshana wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Iringa.
Katika kesi hiyo ilidaiwa kwamba Machi 7 mwaka huu akiwa Ubungo Dar es Salaam, Nondo alichapisha taarifa hizo akitumia simu ya kiganjani yenye No. 0659366125 kinyume cha Sheria ya Makosa ya Mtandao na kusambaza katika mitandao ya jamii.
KAULI NONDO
Akizungumza nje ya mahakama baada ya hukumu hiyo, Nondo alisema katika kipindi chote wakati anatetea haki za wanafunzi na kuendelea na kesi dhidi yake, alipita kwenye nyakati nzito katika maisha yake ila anamshukuru Mungu kwa vile Mahakama imetenda haki.
Alisema pamoja na hali hiyo, kamwe hatorudi nyuma katika mapambano ya kutetea haki za wanafunzi nchini kwa kupaza sauti mambo yanapopindishwa.
“Katika kipindi chote ambacho nilikuwa napitia mapito haya mazito iwapo ningekuwa sina msimamo ningekuwa nimerudi nyuma na kukata tamaa kukubali kila nilichoshinikizwa niseme niweze kuachiwa.
“… lakini sikuwa tayari kwa hilo nilimtanguliza Mungu ambaye leo (jana), ameweza kunipigania, namshukuru Mungu na Mahakama kwa kutenda haki.
“Pia naushukuru Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu (THRDC), muda wote wamekuwa nami, asanteni sana mawakili wangu, asanteni Watanzania wote sitorudi nyuma kuwa mtetezi wa wanyonge,” alisema Nondo.
Alisema amepita katika mapito mazito kwa ajili ya kupigania haki za wanafunzi na kamwe hataacha kuendeleza harakati za kupigania haki zao.
“Mungu ni mwema ametenda mema juu yangu na sitarudi nyuma, nawaombeni niwashukuru pia waandishi wa habari nchini hasa Iringa ambao muda wote mlifika kufuatilia kesi yangu naomba leo (jana) niishie hapa.
“Nitasema zaidi ila leo (jana) sipo vizuri nina furaha kubwa,” alisema Nondo huku akibubujikwa machozi
Mratibu wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu (THRDC), Onesmo ole Ngurumwa, alisema Mahakama imeweza kutenda haki na uamuzi uliotolewa na mahakama hauna hata chembe moja ya upendeleo .
Katika kasi hiyo, Nondo alikuwa akitetewa na mawakili wawili, Chance Luoga na Jebra Kambole ambao walieleza imani kubwa kwa mahakama kupitia hukumu hiyo.
Wakili Kambole alisema kuna uonevu mkubwa ambao polisi walionyesha kumtendea mteja wao ambao mahakama pia imeuona.
Hukumu hiyo ilichukua saa moja kusomwa huku askari wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU) wakiwa wametanda nje ya mahakama hiyo.
MAHAKAMA ILIVYOHUKUMU
Akisoma hukumu hiyo, Hakimu Chemshana alisema kwa mujibu wa ushahidi wa Nondo mahakamani hapo, alitekwa eneo la Ubungo Dar es Salaam na watekaji wakiwa katika gari walikuwa wakimhoji mshtakiwa kuwa nani yupo nyuma ya maandamano yaliyokuwa yamepangwa kufanyika ya kupinga mauaji ya mwanafunzi Akwilina Akwilini wa Chuo chaUsafirishaji (NIT).
Alisema kutokana na ushahidi uliotolewa na mshatakiwa pamoja na Jamhuri hapana shaka kuwa Nondo alikwenda polisi kama mlalamikaji ila polisi walimchukua kama mtuhumiwa .
“Mahakama hii imeptia ushahidi na majumuisho ya kesi hii na kujiridhisha bila shaka yoyote kuwa makosa mawili ni kueleza uongo na kurusha uongo mitandaoni ni jambo lisilo na ubishani ila ni nani aliyeeleza taarifa hizo na kurusha uongo.
“Swali la kujiuliza, je, jamhuri wameshindwa kueleza kuwa mshtakiwa alifikaje Mafinga?
“Pili Mahakama imekosa ushahidi kuhusu alifikaje Mafinga, tatu, hakuna ushahidi kutoka Jamhuri kuwa mshatikiwa alikuwa wapi wakati wa tukio.
“Hivyo mashahidi wa Jamhuri wametoa ushahidi wa hisia,” alisema Hakimu Chamshama
Hakimu alisema swali la nne ambalo halina majibu ni Jamhuri wameshindwa kuthibitisha uongo wa mshatikiwa kwa kila namna na hata kielelezo kilicholetwa na Jamhuri kinatia shaka… kwa mkanganyiko huu mahakama imejizuia kuyaamini maelezo yaliyoletwa mahakamani.
Alisema ujumbe uliotumwa kupitia simu ya Nondo uliosomeka ‘Am at risk!’ kwa maana nipo hatarini, haukueleza hatari ya nini na haujulikani ulitumwa na nani ambako upande wa Jamhuri ulishindwa kutolea ushahidi .
Hakimu Chemshama alisema mtu aliyepelekwa kutoa ushahidi kama mpenzi wa Nondo alisema aliwasiliana na Nondo ila hakusema Nondo yupi, wapi na ujumbe wa ‘Am At risk’ uliotumwa haukutumwa na mshtakiwa ingawa ulitumwa kwenye kundi la WhatsApp.
Alisema ushahidi wa shahidi wa tatu kama ulivyo hauonyeshi ni maagizo kutoka kwa mshtakiwa .
Hakimu alisema si jukumu la Mahakama kujua mshtakiwa alitekwa au hakutekwa, hilo ni jukumu la polisi hivyo mahakama imeamua Abdul Nondo aachiwe huru.
Aisema asiyeridhika na hukumu hiyo ana haki ya kukata rufaa mahakama ya juu.