24.5 C
Dar es Salaam
Saturday, April 20, 2024

Contact us: [email protected]

NMB yazindua kampeni kuhamasisha Bima

Na Mwandishi Wetu, Mtanzania Digital

Benki ya NMB imezindua kampeni maalum yenye lengo la kutoa hamasa na elimu juu ya umuhimu kwa Bima kwa Watanzania.

Kampeni hiyo iliyoitwa “Umebima? Siyo ngumu kihivyo” imezinduliwa Machi 8, 2022 katika Soka la Karume na kuhudhuriwa na makampuni kumi ya Bima ambayo unaweza kupata Bima zao kupitia matawi ya NMB kote nchini.

Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Afisa Mkuu wa Wateja Binafsi na Biashara wa benki ya NMB, Filbert Mponzi amesema kuwa licha ya umuhimu wake kwa maisha ya Watanzania na katika shuguli za kila siku, bado muitikio wa watu kukata Bima umekuwa mdogo sana.

“Pamoja na elimu kutolewa bado idadi ya watu wanaoweka bima ni ndogo sana, ambapo ni asilimia 15 tu ya watanzania ndio wanaotumia huduma za Bima, idadi hii bado ni ndogo sana,” amesema Mponzi na kuongeza kuwa;

“Lengo la Benki ya NMB kupitia kampeni hii ni kueneza elimu na hamasa juu ya uwekaji wa Bima ili idadi hii ya Watanzania wenye bima iongezeke kutoka 15% mpaka 50% ya Watanzania ifikapo mwaka 2030.

“Kwa sababu za Kijiografia, tunatambua kuwa makampuni haya ya Bima hayajafikia maeneo yote nchini lakini kwa kuwa Benki ya NMB imetapakaa nchi nzima na ina matawi katika wilaya zote nchini, tumeona ni vyema kushirikiana na makampuni haya kuuza Bima hizi katika kila tawi la benki yetu. Hivyo ukifika katika tawi lolote la NMB hapa nchini utaweza kununua bima yeyote uitakayo, iwe bima ya Afya, Maisha, chombo au yeyote ile,” alisisitiza Mponzi.

Mponzi amesema kuwa pamoja na huduma ya kukatiwa Bima, yeyote atakayefika katika tawi la NMB ataelimishwa na kueleweshwa juu ya huduma za Bima na umuhimu wake.

Mkuu wa Idara ya Bima wa Benki ya NMB, Martine Massawe alisema kuwa kampeni hiyo haijazinduliwa Dar es Salaam tu, bali na katika mikoa mbalimbali nchini huku lengo likiwa kufika katika mikoa yote ya Tanzania kueneza elimu hiyo muhimu ya Bima.

“Leo tunazindua katika soko la Karume hapa Dar es Salaam lakini pia mikoa kadhaa inafanya uzinduzi na tutasogea katika kila mikoa ili kuhakikisha elimu hii ya bima ambayo ni ya muhimu sana inawafikia watanzania wengi zaidi na kupitia benki ya NMB wengi wao waweze kujipatia huduma mbalimbali za Bima,” amesema Massawe

“Matawi yetu yote 226 yatatoa huduma ya kuuza Bima lakini pia tutakuwa na vituo maalum vya kutoa elimu na kuuza Bima katika maeneo mbalimbali, kama kwenye masoko kama la Kariakoo, Mwenge na kwingineko nchini kote,”ameongeza.

Uzinduzi huo pia ulihudhuriwa na Kaimu Mkurugenzi wa Mipango, tafiti na maendeleo ya masoko wa Tume ya usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA), Zakaria Muyengi na wahanga wa moto uliyoteketeza soko la Karume lakini kwa kupitia bima walizokata na kampuni ya Reliance insurance kupitia benki ya NMB walilipwa hasara yao na sasa wanaendelea vyema na biashara zao.

Katika huduma ya bima, NMB inashirikiana na kampuni ya Sanlam Life, UAP, Shirika la Bima la Taifa (NIC), kampuni ya Jubilee Insurance, kampuni ya Jubilee Life, kampuni ya Metropolitan Life, kampuni ya Britam Insurance, na Shirika la Bima Zanzibar (ZIC).

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles