31.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

NMB yatoa vifaa vya Mil. 29/- Hospitali ya Amana, shule Ilala

Na Mwandishi Wetu, Mtanzania Digital

HOSPITALI ya Rufaa ya Amana na shule tatu za msingi za Buguruni Kisiwani, Kivule na Airwing zilizoko wilayani Ilala jijini Dar es Salaam, zimeingia katika orodha ya wanufaika wa Programu ya Uwajibikaji kwa Jamii (CSR 2022) ya Benki ya NMB, baada ya Ijumaa iliyopita kukabidhiwa misaada yenye thamani ya Sh milioni 29.

Meneja wa Kanda ya Dar es Salaam, Pwania na Zanzibar, Donatus Richard akimuonyesha Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Ng’wilabuzu Ludigija vifaa vilivyokabidhiwa na Benki ya NMB kwa Shule za Msingi za Airwing, Kivule na Buguruni Kisiwania ikiwa ni Mabati, Madawati pamoja na Kabati za kuhifadhia Dawa katika Hospitali ya Rufaa ya Amana vyote vikiwa na thamani ya Shilingi milioni 29.

Makabidhiano hayo yalifanyika Shule ya Msingi Buguruni Kisiwani, ambako Meneja wa NMB Kanda ya Dar es Salaam, Donatus Richard, alimkabidhi Mkuu wa Wilaya ya Ilala (DC), Ng’wilabuzu Ludigija, vifaa vyenye thamani hiyo, ambayo ni kati ya Sh. Bilioni 2.8 zilizotengwa na benki hiyo kusaidia Sekta za Elimu na Afya kwa mwaka 2022.

Wakati Hospitali ya Amana ikikabidhiwa masanduku ya kuhifadhia vifaa tiba vya wagonjwa waliolazwa ‘bed side rockers’ 30 zenye thamani ya Sh. Mil. 9.2, Shule ya Airwing ilikabidhiwa madawati 100 yenye thamani ya Sh. Mil. 10, huku Shule ya Buguruni Kisiwani ikikabidhiwa mabati 150 yenye thamani ya Sh. Mil.4.8.

Nayo Shule ya Msingi Kivule, ilikabidhiwa madawati 50 yenye thamani ya Sh milioni 5, hivyo kufanya jumla kuu ya thamani kufikia Sh milioni 29, ambako DC Ludigija aliishukuru benki hiyo na kusema anaamini misaada hiyo inaenda kuamsha ari ya kujisomea na kuboresha mazingira ya kufundishia, pamoja na kuhudumia wagonjwa.

Ludigija aliitaka Benki ya NMB kuendelea kuunga mkono jitihada za Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan, katika kunyanyua elimu na kuboresha miundombinu ya afya wilayani mwake, ambako uwingi wa shule na hospitali, umesababisha kuongezeka kwa wanafunzi na wagonjwa, hivyo kuongeza changamoto.

“Serikali tunawashukuruni kwa namna mnavyojitoa kutatua changamoto kwenye elimu na afya wilayani Ilala, ambako uhitaji ni mkubwa na bado nguvu ya Serikali haitoshi bila sapoti za wadau. Kwa hili mnadhihirisha ukweli kuwa; ‘Ninyi NMB ni Benki Baba Lao,’ mnaoongoza katika kutekeleza takwa la CSR,” alisema Ludigija.

Kwa upande wake, Donatus aliishukuru Manispaa ya Ilala pamoja na viongozi wa shule zilizokabidhiwa misaada hiyo kwa kuitazama NMB kama mshirika sahihi katika utatuzi wa changamoto, hivyo kuipelekea maombi yao na kwamba wao wanajisikia faraja kuwa wadau vinara katika kurejesha kwa jamii sehemu ya faida yao.

“Misaada hii tunaitoa chini ya mwamvuli wa CSR, programu ya kila mwaka, ambayo kwa mwaka huu wa 2022 tumetenga kiasi cha Sh bilioni 2.8 ambazo ni sawa na asilimia 1 ya faida yetu kwa mwaka uliopita, tukirejesha kwa jamii, ambayo ndio sehemu ya wateja wetu.

“Kwa sababu sehemu ya faida tunairudisha kwao, basi wito wetu wa Watanzania ni kutumia huduma zetu zilizotapakaa matawini kote nchini, ambako kuna mikopo ya riba nafuu kwa kada zote za wafanyakazi, wakulima, wafanyabiashara, wajasiriamali, wafugaji na wavuvi. NMB ndio suluhu ya changamoto za kifedha,” alisisitiza Donatus.

Akisoma risala ya shule kwa Mkuu wa Wilaya, Mwalimu Lilian Saguti wa Shule ya Buguruni Kisiwani, alisema shule hiyo iliyoanzishwa miaka 19 iliyopita (2003), kwa sasa ina wanafunzi 1169 na walimu 32, huku ikikabiliwa na changamoto za madawati, viti na meza za walimu, pamoja na vifaa vya michezo, ikiwemo viwanja.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles