24.1 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

Wakulima wa mradi wa kilimo himilivu cha mtama waingiza bilioni 13.5

Na Mwandishi Wetu, Dodoma

Wakulima 22,000 waliopo kwenye Mradi wa Kilimo Himilivu cha Mtama (CSA), kutoka wilaya sita za mkoa wa Dodoma, wamefanikiwa kuingiza Sh bilioni 13.5 kwa msimu wa mwaka 2020 hadi 2021.

Aidha, Shirika la Mpango wa Chakula Duniani (WFP) kwa kushirikiana na FarmAfrika wamewahakikishia wakulima hao masoko ya uhakika ndani na nje ya nchi.

Hayo yamesemwa na Mkuu wa Ofisi Ndogo ya WFP, Neema Sitta wakati akizungumza na waandishi wa habari kwenye ofisi zao zilizopo hapa jijini Dodoma.

Amesema mradi huo wa CSA unatekelezwa katika vijiji zaidi ya 200 vilivyopo kwenye wilaya sita za Bahi, Chamwino, Mpwapwa, Kongwa, Chemba na Kondoa ambapo kwa msimu wa mwaka 2020 hadi 2021 wamefanikiwa kuuza zaidi ya tani 28,000 za mtama, zenye thamani ya Sh bilioni 13.5.

Sitta amesema mradi huo unaofadhiliwa na Shirika la Maendeleo ya Ireland (IrishAid) na kusimamiwa na kutekelezwa WFP Kwa kushirikiana na FarmAfrika kwa Sh bilioni 1.7.

“Mradi wa CSA ambao umefikia wakulima 22,000 na kunufaisha zaidi ya watu 100,000 umeweza kuwaingizia wakulima zaidi ya Sh.bilioni 13.5 baada ya kuzalisha zaidi ya tani 28,000. Matarajio yetu ni kuona wakulima wa mtama wanaongeza uzalishaji kwa msimu mpya, ili kujipatia kipato cha uhakika,” ameeleza.

Mkuu huyo wa ofisi ndogo ameeleza sababu ya wao kujikita katika kilimo cha mtama ni kutokana na zao hilo kukubali ardhi na mazingira ya Dodoma, pamoja na uhakika wa soko.

“Zao la mtama lina vitamin nyingi ambazo zinafaida kwa mwili wa binadamu, hivyo mkakati wetu wa siku zijazo ni kuongeza uzalishaji,” ameeleza.

Ameongeza soko la zao la mtama mweupe lipo nchini Sudani Kusini,Burundi na wateja wengine wanatoka kwenye Kiwanda cha Bia Tanzania (TBL) na kampuni nyingine za ndani.

Sitta amesema ufanisi wa mradi huo ambao unatekelezwa na FarmAfrika umetokana na mafunzo ambayo wakulima wamepatiwa pamoja na kuwaunganisha na masoko ya ndani na nje.

Amesema wakati mradi huo unaanza walikuta wakulima wanavuna gunia tatu kwa hekari ila kwa sasa wanavuna gunia 10 kwa hekari moja hiyo hiyo kutokana na mafunzo na elimu wanayopewa.

Alieleza WFP na FarmAfrika wameweza kuunganisha wakulima na soko moja kwa moja na kuondoa madalali waliokuwa wanachangia kushusha bei ya zao.

Alifafanu kwa sasa bei ya zao la mtama kilo moja inaunzwa hadi Sh 550 kutoka Sh 250 ya awali hivyo kuongeza kipato kwa wakulima na kuhamasisha kilimo hicho.

Sitta alisema kilimo cha mtama ambacho kinalimwa mkoa wa Dodoma kinazingatia mfumo wa kilimo hai jambo ambalo linachangia kuwepo na uhakika wa soko kote duniani.

Amesema ushiriki wao kwenye kilimo ni kuhakikisha mkulima ananufaika na kilimo lakini ardhi inakuwa endelevu kwa vizazi vijavyo.

Kwa upande wake Meneja Mradi wa CSA, kutoka FarmAfrika Tanzania, Grace Changanyika amesema mradi huo umekuwa na mafanikio makubwa kwa wakulima jambo ambalo linawarahisishia kufikisha ujumbe wao kama watekelezaji wa mradi.

Changanyika amesema mafanikio waliyoyapata wakulima 22,000 kupata zaidi ya Sh bilioni 13.5 yamevutia wakulima wengi kutaka kuingia kwenye mradi.

“Kilimo hiki kimebadilisha maisha ya wakulima kiuchumi, kijamii na maendeleo, ukilinganisha na kipindi cha nyuma kabla ya mradi,” amesema.

Naye Mkulima Patrick Mbeho wa kijiji cha Mkola wilayani Bahi, amesema mradi huo umefanya mapinduzi makubwa kwenye maisha yake kwa kipindi cha muda mfupi.

Mbeho ambaye ana zaidi ya hekari 20 za mtama, amesema ameweza kupata mavuno mara tatu ya yale ambayo akiyapata katika miaka ya nyuma kwenye eneo lenye ukuba uleule, pia uhakika wa soko.

“Kwangu haya ni mapinduzi ya kiuchumi, kijamii na maendeleo kwani nilikuwa napata Sh. milioni mbili kwa shamba la hekari 20 ila kwa sasa napata hadi Sh. milioni sita, nimefanikiwa kujenga nyumba ya biashara, mashine ya kupembulia mtama na mengine mengi,” amesema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles