Na Mwandishi Wetu, Mtanzania Digital
WIKI moja kabla ya kufanyika kwa Mbio za Hisani za NMB Marathon ‘Mwendo wa Upendo,’ Benki ya NMB inayoandaa mbio hizo imetangaza wadhamini zaidi ya 20, ambao wameeleza siri ya uamuzi wa kukubali kudhamini kuwa ni kuguswa na wazo chanya la benki hiyo kuwakomboa kinamama nchini.
NMB Marathon 2022, zinazolenga kukusanya kiasi cha Sh milioni 600 za kusaidia matibabu ya kinamama wenye tatizo la Fistula wanaotibiwa kwenye Hospitali ya CCBRT, zitafanyika Oktoba 1, kwenye viwanja vya Leaders Club, Mgeni Rasmi akitarajiwa kuwa Waziri Mkuu Kassim Majaliwa.
Akizungumza wakati wa utambulisho huo jijini Dar es Salaam jana, Afisa Mkuu wa Fedha wa NMB, Juma Kimori, aliwashukuru wadhamini hao kwa kusapoti mbio hizo na kurahisisha lengo lengo la kukusanya Sh milioni 600 mwaka huu, hivyo kutoa nafasi mapato ya miaka miwili ijayo ya mbio hizo kuyaelekeza katika maeneo mengine yenye uhitaji.
“Mwaka jana wakati tukizindua NMB Marathon tuliweka lengo la kukusanya Sh bilioni 1 katika kipindi cha miaka minne, mwitikio mkubwa ukatuwezesha kukusanya Sh milioni 400 badala ya 250 tulizotarajia. Ndipo tulipoona umuhimu wa kupata milioni 600 mwaka huu, ili kukamilisha bilioni 1.
“Tunawashukuru wadhamini wetu waliogawanyika katika kategori zaidi ya tano, zikiwemo za Executive, Gold, Bronze na Media Partner kwa kujitokeza kutusapoti kama tulivyowaomba wakati tukizindua mbio hizi mwaka huu, na kutoa michango yao katika kufanikisha mchakato huu wa kusaidia kinamama wetu,” alisema Kimori.
Aliwataja Wadhamini Wakuu wa kuwa ni Sanlam Life Insurance na UAP Insurance (Executive), huku Jubilee General Insurance (ikiwa kategori ya Gold). Wadhamini wa kundi la Bronze ni pamoja na Alliance Life Assurance, Britam Insurance Tanzania, Reliance Insurance na ARiS Risk and Insurance Solutions.
Wengine wa kundi hilo ni pamoja na Jubilee Life Insurance na Metropolitan Life Insurance, huku Toyota, TBL, Strategis, Serena Hotel, Azam, na Johari Rotana Hotel wakiwa ni miongoni mwa wadhamini wengineo.
Katika kategori ya vyombo vya habari washirika, Kimori aliitaja EFM Radio, TV E, Mwananchi Communications Limited, IPP Media na Almasi Productions, orodha iliyokamilishwa na Kampuni za SGA Security Tanzania, Gelato na Grano Coffee.
Kwa nyakati tofauti katika utambulisho huo, wadhamini hao waliipongeza NMB kwa wazo chanya la kulikomboa kundi la kinamama wanaoshindwa kujitibu Fistula kutokana na gharama kubwa na kwamba kujitokeza kwao kuunga mkono jambo hilo, ni uthibitisho kwamba afya ya mama ni kipaumbele muhimu kwa jamii.
Afisa Mtendaji Mkuu wa Sanlam, Julius Magabe, aliishukuru NMB kwa kuwashirikisha katika suala hilo la tiba kwa kinamama wenye Fistula na kwamba kwao hiyo ni nafasi muhimu na adhimu ya kusapoti wanawake, huku akieleza kwamba watakuwa bega kwa began a NMB katika jambo lolote la kijamii.
Naye Mariam Hussein, ambaye ni Mkuu wa Kitengo cha Mauzo wa Kampuni ya Bima ya UAP, alisema amani na kuboresha maisha ya kila mtu ni kati ya vipaumbele vya UAP na kwamba hiyo ndio siri ya uharaka wao katika kudhamini NMB Marathon, ambayo hawataishia kudhamini tu, bali watakimbia mbio hizo.