25.1 C
Dar es Salaam
Tuesday, December 10, 2024

Contact us: [email protected]

DIT kuanzisha Shahada ya Miji endelevu

Na Mwandishi Wetu, Mtanzania Digital

Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam (DIT) inaandaa mtaala mpya wa shahada ya kwanza ya Miji Endelevu ya Kisasa na Teknolojia shirikishi (Bachelor Degree Programme in Sustainable Smart City Allied Technologies NTA Level 7 and 8)
ili uendane na mahitaji yaliyopo.

Mtaala huo umewasilishwa leo kwa wadau kwa ajili ya kupitia kutoa maoni na mapendekezo ili kuuboresha kwa hatua zaidi.

Akifungua warsha hiyo iliyofanyika kwenye Ukumbi wa mikutano wa DIT jijini DaresSalaam leo Alhamisi Septemba 22, 2022 Mkuu wa Taasisi hiyo, Prof. Preksedis Marco Ndomba amesema, DIT ni Taasisi kongwe na sasa imedhamiria kuwa kiongozi katika kutoa mafunzo yanayotatua changamoto za jamii barani Afrika.

“Dhamira yetu kuwa kiongozi hasa katika kutoa mafunzo yatakayotatua matatizo ya jamii Afrika na hii tutaifanikisha kupitia dhana yetu ya kutoa mafunzo ya ufundi viwandani tunaamini wahitimu wetu watakuwa na uwezo wa kuzalisha bidhaa zinazokubaliwa kwenye soko lakini zinazotatua changamoto za jamii,” amesema Prof. Ndomba.

Aidha, amesisitiza kuwa DIT kupitia dhana ya mafunzo viwandani inalenga kuwa chachu ya kuendeleza viwanda na ndio sababu ya kuboresha maudhui ya masomo pamoja na namna ya kufundisha kwa kuwa lengo letu ni kuisaidia jamii kwa kuhakikisha wanakuwa na ujuzi yakinifu pamoja na ubunifu katika nyanja zote.

Prof. Ndomba amewataka wadau walioshiriki kwenye warsha hiyo kutoa maoni yao kwa kuzingatia weledi kwa kuwa maoni yao ni muhimu na yatasaidia kuboresha mtaala huo wa program ya pekee inayolenga kuzalisha wataalam ambao watahitajika kwa siku za usoni.

“Niwaalike kwa dhati kabisa kutoa maoni yenu kwa kuzingatia weledi na utaalam wa kila mmoja, toeni mawazo bila woga kwa kuwa hii ni programu ya pekee lengo ni kuzalisha vijana watakaohitajika baadae badala ya kuanza kutafuta utaalam kama huo nje ya nchi……. hivyo tukae hapa tukijua tunaandaa kitu kizuri kitakachosaidia wote,” amesema Prof. Ndomba.

Kwa pande wake Mkuu wa Idara ya Mawasiliano ya Angani, Dk.Petro Pesha amesema, DIT kupitia wataalam wake imeona changamoto zilizopo kwenye miji mingi, moja ya changamoto hizo ni msongamano wa magari, mipango miji kutokuwa nzuri, uhifadhi wa taka pamoja na uhalifu hivyo wakahamasika kuandaa programu ambayo itasaidia kuandaa wataalam ambao watasaidia kutatua changamoto hizo.

“Miji yetu inakumbwa na changamoto mbalimbali kwa hiyo changamoto hizi zinahitaji utatuzi wa kitaalam, sasa huwezi kuzitatua kama huna utaalam au wataalam katika hayo maeneo hivyo mtaala huu utasaidia katika kupata hawa wataalam,” amesema Dk. Pesha.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
592,000SubscribersSubscribe

Latest Articles