Na Ruth Mnkeni, Dar es Salaam
BENKI ya NMB imeorodhesha kiasi cha Sh bilioni 41.4 ilichokipata kutokana na mauzo ya hatifungani ya NMB yenye uhai wa miaka mitatu mpaka siku ya kukomaa.
Akizungumza jana jijini Dar es Salaam wakati wa kuorodhesha hatifungani hizo iliyoashiriwa na upigaji wa kengele Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Dk. Adelhelm Meru, aliipongeza benki hiyo kwa kuorodhesha hatifungani kwenye soko la hisa kuwa ni ya kizalendo na kuwataka wawekezaji katika sekta binafsi kushiriki.
“Hatifungani hii inatarajiwa kuleta maendeleo katika soko la mitaji na inafungua njia kwa mashirika mengine binafsi, mashirika ya Serikali na mamlaka za manispaa kutafuta njia mpya za kukuza mitaji na uwezeshaji,” alisema Dk. Meru.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa NMB, Ineke Bussemaker, alisema hatifungani hiyo ya miaka mitatu si tu imeleta msisimko chanya kwenye soko la mitaji bali hata katika soko la hisa, NMB inakuwa benki ya kwanza kupata kiwango zaidi ya mara mbili ya kiwango walichoomba awali.
Ineke aliongeza kuwa mwitikio chanya kwenye hatifungani ya NMB unatoa somo kuwa kuna umuhimu wa benki mbalimbali kuchangia kwa kiwango kikubwa katika kuendeleza masoko ya mitaji na kupigania elimu ya fedha kwa jamii.
Alisema hatifungani ya NMB ilipata mwitikio chanya kutoka kwa wawekezaji na kupita kiwango kilichopangwa awali kwa asilimia 107.
Alisema benki hiyo ilipata maombi 1,811 yenye thamani ya Sh bilioni 41.4 huku maombi mengi yakirundikana wiki ya mwisho kabla ya kufunga upokeaji wa maombi.