Na Mwandishi Wetu, Same
Mkuu wa Wilaya ya Same mkoa wa Kilimanjaro, Rosemary Senyamule amepokea vifaa mbalimbali vya kusaidia miundombinu ya elimu kutoka Benki ya NMB katika Shule tano za halmashauri hiyo vyenye thamani ya Sh milioni 25.
Akizungumza wakati wa hafla iliyofanyika katika Shule ya Sekondari Kwakoko, Rosemary alisema NMB imekua ikisaidia huduma za jamii ikiwemo kuboresha miundombinu ya elimu nchini ambayo inachangia kuweka mazingira mazuri ya kujifunzia.
Alisema dhamira ya serikali ni kuhakikisha wanafunzi wote wa Shule za Msingi na Sekondari wilayani humo wanakua na mazingira rafiki ya kujifunzia na kuhimiza uongozi wa Shule zilizopata meza na viti kuvitunza ili vitumike kwa muda mrefu zaidi.
“Serikali inatambua michango ya mara kwa mara ambayo NMB mmekua mkitoa kwa jamii nchi nzima,imekua ikigusa na kusaidia maisha ya wanufaika kwa kiwango kikubwa naamini mtaendelea kuchangia hata maeneo mengine,”alisema Senyamule
Wakati huo huo alitaka benki hiyo kuona umuhimu wa kufungua tawi lingine kwenye ukanda wa milimani hasa vijiji vinavyojishughulisha na kilimo ili kuhakikisha wananchi wa maeneo hayo wanakua na utamaduni wa kuhifadhi fedha zao benki.
Alisema maeneo hayo yana vikundi visivyo rasmi ambavyo wenyeviti wake wamekua na utamaduni wa kutunza fedha ndani ya nyumbani zao badala ya benki na kumekua na malalamiko ya upotevu wa fedha za wana vikundi jambo ambalo halipaswi kuendelea kufumbiwa macho.
Awali Meneja wa NMB Kanda ya Kaskazini, Aikansia Muro alisema benki hiyo imetoa meza na viti 180 pamoja na mabati 192 kwaajili ya Shule za Sekondari Kwakoko, Bemko, Chauka, Vumari na Shule ya Msingi Mwenge.
“Changamoto za sekta ya elimu kwa NMB ni jambo la kipaumbele, hii ni kutokana na ukweli kwamba elimu ndio ufunguo wa maisha na kichocheo kikuu cha maendeleo ya wananchi hapa nchini,tunatambua juhudi za serikali za kusimamia elimu kwa nguvu zote kwa kuboresha utoaji wa huduma mijini na vijijini,” alisema Aikansia
Alisema licha ya benki hiyo kupokea maombi mengi ya kuchangia miradi ya jamii imejikita zaidi katika maeneo ya elimu, afya na misaada ya hali na mali katika nyakati ngumu za majanga.