28.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, December 4, 2024

Contact us: [email protected]

NMB yadhamini Mkutano Mkuu wa Uchaguzi ALAT kwa Mil. 150

NA MWANDISHI WETU

BENKI ya NMB imedhamini Mkutano Mkuu Maalum wa Uchaguzi wa viongozi wa Jumuiya ya Tawala za Mitaa Tanzania (ALAT) kwa sh Mil. 150, huku ikijivunia makusanyo ya zaidi ya sh Trilioni 6 kupitia Mfumo wa Ukusanyaji Mapato ya Serikali Kielektroniki (GePG) katika kipindi cha miaka mitatu iliyoishia Julai 2021.

Mkutano Mkuu Maalum wa Uchaguzi ALAT Taifa umefanyika leo Septemba 27,kwenye Ukumbi wa Jakaya Kikwete jijini Dodoma , ukifunguliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, aliyeambatana na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, Spika wa Bunge Job Ndugai na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Ummy Mwalimu.

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mkutano huo, Afisa Mtendaji Mkuu wa Benki ya NMB (CEO), Ruth Zaipuna, amesema wanajivunia ushirikiano wao na ALAT, ambao umekuwa chachu ya kudhamini mara kwa mara mikutano yao hiyo na kuwa anaamini Jumuiya hiyo itauenzi uhusiano huo, huku wakiendelea kuifanya NMB kuwa benki namba moja katika Makusanyo ya Halmashauri zote nchini.

“Matarajio yetu ni kuendekeza uhusiano mwema kati ya ALAT na NMB, pamoja na ushirikiano mzuri na Halmashauri zote katika kukamilisha miradi mikubwa inayosimamiwa na Halmashauri zetu, lakinipia tumekuwa vinara wa makusanyo ya fedha za Serikali.

“Katika mwaka mmoja wa fedha uliopita (Julai 2020 Hadi Julai 2021), NMB ilikusanya Sh. Bilioni 343.9, wakati kwa miaka mitatu tumekusanya takribani Sh. Trilioni 6, huku tukiwa sehemu ya ufanikishaji wa miradi na uendelezaji wa mazao ya kimkakati kote nchini,” alisema CEO Zaipuna.

Akifungua Mkutano huo, Rais Samia aliipongeza NMB kwa kubeba dhamana kufanikisha Uchaguzi wa ALAT Taifa, huku akiwataka Wajumbe kuchagua viongozi sahihi, ili kuitendea haki kaulimbiu ya mkutano huo isemayo ‘Chagua Viongozi Bora kwa Maendeleo Endelevu,’ kwani ALAT imara ndio Msingi mkuu wa maendeleo endelevu yanayochakatwa na Serikali yake.

Rais Samia akaenda mbali kwa kuwataka viongozi wateule wa uchaguzi huo kuisimamia ALAT kufanya kazi kwa kufuata sheria, haki na uadilifu, kwani anawategemea viongozi wa kada hiyo katika kusimamia makusanyo na matumizi ya fedha za miradi ya Halmashauri na kuwasisitiza wajiepushe na ubaadhirifu.

“Fanyieni kazi vipaumbele muhimu ambavyo ni pamoja na kutenda haki, kufanya kazi kidijitali, ushirikiano baina ya mameya, wenyeviti wa halmashauri, Wakurugenzi na wakuu wa Wilaya, ili kumaliza tatizo la ubaadhirifu na ufujaji wa fedha. Kahakikisheni thamani ya pesa kwa miradi mnayosimamia utekelezaji wake inaonekana,” alisisitiza Rais Samia.

Mkutano Mkuu Maalum wa Uchaguzi wa ALAT Taifa, ambao awali ilikuwa ufanyike Aprili mwaka huu na kusogezwa mbele hadi Septemba – kupisha maombolezo ya msiba wa aliyekuwa Rais wa Tanzania, Dk. John Magufuli, umetumika kuchagua Mwenyekiti, Makamu Mwenyekiti na Wajumbe 16 wa Kamati ya Utendaji kupitia Kanda 6 za Jumuiya hiyo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
592,000SubscribersSubscribe

Latest Articles