Na Nora Damian, Mtanzania Digital
Wakati Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT) kikijipanga kuwa Chuo Kikuu cha Uchukuzi Rais Mstaafu Jakaya Kikwete amekitahadharisha kisitoke nje ya misingi ya kuanzishwa kwake.
Kikwete ameyasema hayo Novemba 15,2023 wakati wa mahafali ya 39 ya chuo hicho ambapo alikuwa mgeni rasmi.
Ametoa mfano kuwa mainjinia bado wanawahitaji watu wenye astashahada za awali, astashahada na stashahada katika shughuli zao hivyo ni muhimu chuo hicho kikaendelea kutoa wataalam wa ngazi hizo hata kama kinataka kuwa chuo kikuu.
“Mwenye ‘degree’ anafanya kazi kwa kushirikiana na hawa wa astashahada na stashahada, injinia mmoja anahitaji ‘techinician’ watano, hata yule mwenye MBA (Master of Business Administration) na BBA (Bachelor of Business Administration) anahitaji wenye certificate katika kufanya kazi.
“Fanyeni yote lakini kuongeza kwenye shahada kusiwafanye mpunguze kwenye astashahada, stashahada. Mkifanya hivyo mtakuwa mmeondoka kwenye madhumuni ya kuunda chuo hiki mwaka 1975,” amesema Kikwete.
Kuhusu kitabu cha historia ya chuo hicho, amesema kimeandikwa vizuri na kwamba kinasaidia kujua chuo kilipotoka, kilipo na kinakokwenda na kuwa faida kwa vizazi vya sasa na vijavyo.
Naibu Waziri wa Uchukuzi, David Kihenzile, amesema
Serikali imeendelea kuboresha miundombinu na mazingira ya kufundishia na kujifunzia katika chuo hicho ambapo ilikipatia fedha za kununua ndege mbili mpya za injini moja zitakazotumika kwa mafunzo ya urubani.
Aidha amesema Serikali imekipatia tena chuo hicho Sh bilioni moja kugharamia malipo ya awali ya ndege mpya moja yenye injini mbili itakayotumika kwa mafunzo ya urubani.
“Serikali itaendelea kutenga fedha za maendeleo kukiwezesha chuo hiki kutekeleza majukumu yake ipasavyo ili kuzalisha wataalam watakaoendana na kasi ya ongezeko la miundombinu ya uchukuzi hapa nchini,” amesema Kihenzile.
Awali Kaimu Mkuu wa chuo hicho, Dk. Zainab Mshana, amesema wanaendelea kuimarisha utoaji wa mafunzo kwa kuandaa mitaala mipya na kuboresha iliyopo na kuimarisha ubora wa mafunzo yanayotolewa.
“Chuo kimeandika andiko la ufadhili kutoka Serikali ya Jamhuri ya watu wa China ili kukipandisha hadhi kuwa chuo kikuu cha uchukuzi,” amesema Dk. Mshana.
Amesema pia wanakabiliwa na changamoto za uhaba wa wahadhiri, uchakavu wa miundombinu na vifaa vya kujifunzia na kufundishia na uhaba wa mabweni.
Katika mahafali hayo wahitimu 3,800 walitunukiwa astashahada ya awali, astashahada, stashahada, stashahada ya juu, shahada na shahada ya uzamili.