JUMATANO iliyopita, David Cameron alijiuzulu rasmi Uwaziri Mkuu wa Uingereza.
Nilifuatilia kwa karibu siasa za Uingereza zilivyokuwa tangu matokeo ya kura ya maoni ya Uingereza kujitoa kutoka Jumuiya ya Ulaya (EU).
Nilimfuatilia kwa karibu zaidi David Cameron, hasa kutaka kuona mwenendo wake utakavyokuwa baada ya Uingereza kupiga kura ya kujitoa EU na hatima yake kama Waziri Mkuu.
Kama nilivyotarajia, baada tu ya matokeo ya ile kura ya maoni kutangazwa, David Cameron alitangaza kujiuzulu nafasi yake ya Uwaziri Mkuu, kwani aliamini kwamba Uingereza ilihitaji nahodha mwingine ambaye ataweza kuiongoza na kuivusha katika kipindi cha kujitoa kutoka Jumuiya ya Ulaya.
Wakati Cameron akiyatangaza hayo, ilijulikana kwamba Waziri Mkuu mpya wa Uingereza angepatikana Septemba mwaka huu, kutokana na kutakiwa kuwepo kwa uchaguzi ndani ya chama cha Conservative, ambacho ndicho chama tawala kwa sasa.
Kikatiba, kiongozi wa chama kitakachoshinda Uchaguzi Mkuu ndiye anayekuwa Waziri Mkuu wa Uingereza. Kutokana na hilo, kwa kuwa chama cha Conservative bado kinaendelea kuwa madarakani hadi uchaguzi mwingine ufanyike nchini humo, ilibidi kuanza kwa uchaguzi ndani ya chama ili atakayeshinda kuwa kiongozi achukue nafasi ya Uwaziri Mkuu.
Ndani ya wiki tatu, mambo yamekwenda mbio sana. Mara baada ya Cameron kutangaza kujiuzulu, walianza kujitokeza wanachama wa Conservative kutangaza kugombea nafasi ya uongozi wa chama. Wengi walidhani kwamba Boris Johnson, Meya wa zamani wa London ambaye aliongoza kampeni ya Uingereza kujitoa EU, angegombea nafasi hiyo na pengine kuja kuwa Waziri Mkuu. Hata hivyo, hakugombea.
Theresa May na Andrea Leadsom ndio waliobaki kwenye kinyang’anyiro hicho na bado kila mtu alijua kwamba kiongozi atachaguliwa Septemba.
Hata hivyo, baada ya kutoa kauli tata na kuandamwa na vyombo vya habari, Leadsom aliamua kujitoa kwenye kinyang’anyiro cha kugombea uongozi wa chama cha Conservative na hivyo kumuacha Theresa May akiwa mgombea pekee.
Hiyo ilitokea Jumatatu ya wiki iliyopita na siku hiyo hiyo Cameron akatangaza kwamba ataachia rasmi madaraka siku mbili baadaye, ili Theresa May achukue nafasi ya uongozi wa chama na Uwaziri Mkuu wa Uingereza.
Siku mbili baadaye, Cameron alikwenda kwenye Bunge lao kama kawaida, akajibu maswali kama kawaida na alionekana mwenye furaha kubwa, hasa pale alipoeleza kwamba ratiba yake ya siku ilikuwa tupu kabisa siku hiyo, kwani zaidi ya kwenda kuonana na Malkia baadaye kwa ajili ya kujiuzulu rasmi, hakuwa na lingine la kufanya. Waliomsikiliza walicheka, naye pia alicheka. Na kile kicheko kilikuwa cha kweli, si cha kinafiki.
Saa chache baadaye Cameron na familia yake walitoka kwa mara ya mwisho kwenye makazi yao ya miaka sita iliyopita – 10 Downing Street. Alizungumza na wanahabari, kisha alipanda Range Rover kuelekea kwa Malkia na kisha kwenye makazi yake mapya.
Naomba tu niseme kwamba wapo wengi wanaomshutumu David Cameron kwa uongozi mbovu, wakiwemo Waingereza wenyewe. Hata hivyo, katika wiki tatu za mwisho za Cameron kuwa Waziri Mkuu, naomba nizungumzie upande wa pili niliojifunza kutoka kwake na ambao ninatamani viongozi wetu wa Afrika wajifunze.
Nilipokuwa nikifuatilia nyendo za David Cameron katika wiki tatu za mwisho za uongozi wake, nilitamani sana kuona kiongozi mmojawapo wa Afrika, ambaye ameruhusu kura ya maoni ya jambo muhimu katika nchi kujiuzulu baada ya tamanio lake kushindwa.
Nilipokuwa nikimfuatilia David Cameron, nilitamani sana kuona kiongozi mmojawapo wa Afrika akiachia kabisa madaraka baada ya kugundua kwamba hakutakiwa kusubiri kwa miezi mingine miwili ili kumpata mrithi wake, kwani alikuwa amekwishapatikana.
Nilipokuwa nikimfuatilia David Cameron, nilitamani sana kuona kiongozi mmojawapo wa Afrika akifurahi kuachia madaraka na kutoa hotuba ya mwisho bila kutoa vijembe vya kuwabeza wapinzani wake, bali kufurahia matunda ya kweli yaliyopatikana katika kipindi cha uongozi wake.
Nilipokuwa nikimfuatilia David Cameron, nilitamani sana kuona kiongozi mmojawapo wa Afrika akiwa na amani na furaha ya kweli, huku akishiriki kubeba mizigo yake na kisha kujumuika na rafiki zake jioni akipata kahawa huku akiwa ndani ya mavazi ya kawaida kabisa.
Nilipokuwa nikimfuatilia David Cameron, nilijifunza jambo kubwa ambalo nilitamani sana kuona viongozi wetu wa Afrika wakijifunza pia.