24.8 C
Dar es Salaam
Thursday, September 21, 2023

Contact us: [email protected]

Ujio wa mwenyekiti mpya na harufu ya mabadiliko CCM

Rais John Pombe Magufuli.
Rais John Pombe Magufuli.

NA MASYAGA MATINYI,

BAADA ya kumalizika Uchaguzi Mkuu Oktoba mwaka jana, kumekuwapo matukio kadhaa ya kisiasa nchini, lakini Jumamosi wiki hii mjini Dodoma kuna tukio la aina yake ambalo kila Mtanzania mwenye kujitambua bila kujali itikadi yake, ataelekeza macho na masikio huko.

Uchaguzi wa Oktoba ulitupa Rais mpya na Mkutano Mkuu maalumu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), ambacho ni chama tawala, utashuhudia Mwenyekiti mpya akikabidhiwa kiti.

Mwenyekiti wa sasa wa CCM, Rais (mstaafu), Jakaya Kikwete, atakabidhi uenyekiti kwa Rais John Magufuli, kwa mujibu wa utamaduni uliozoeleka ndani ya chama hicho, lakini si kwa mujibu wa Katiba. Kama ingekuwa kwa mujibu wa Katiba, basi ingesubiriwa 2017.

Ingawaje tayari CCM kupitia msemaji wake, Christopher ole Sendeka, imesema Mwenyekiti ajaye lazima achaguliwe kwa kupata kura zisizopungua asilimia 50 ya kura zote, ukweli unabaki kuwa hakuna mwanachama anayetarajiwa kuwa Mwenyekiti mpya zaidi ya Rais Magufuli.

Tukio la Jumamosi litatoa fursa ya kipekee kwa CCM kujipanga upya kama ikidhamiria na kurejesha imani kwa wananchi hasa walio wanyonge, ambao kimbilio lao linapaswa kuwa chama hicho.

Si jambo la siri au kubahatisha kukiri kuwa imani waliyokuwa nayo Watanzania wakati chama hicho kinaasisiwa na Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere pamoja na waasisi wengine, imepotea kabisa.

Katika miongo kadhaa iliyopita, tumeshuhudia chama kilichojinasibu kama cha wakulima na wafanyakazi, kikigeuka na kuwa pango la mafisadi, matajiri, wapokeaji na watoa rushwa, matapeli na wajanja wengine.

Kama si kazi kubwa aliyoifanya Katibu Mkuu, Abdulrahman Kinana, kuzunguka nchi nzima kukifufua chama, pengine hii leo tungekuwa tunazungumza lugha nyingine.

CCM ilijisahau kabisa, ililewa madaraka, ambapo ziara za Kinana ziliibua mambo mengi ya ovyo, ikiwamo kuwaibua hadharani mawaziri na watendaji mizigo.

Zamani sifa ya kuwa kiongozi ndani ya CCM ilikuwa uadilifu, upendo, nia ya dhati ya kuwatumikia wananchi, uzalendo na mema mengineyo, lakini miaka ya karibuni sifa kuu imegeuka na kuwa fedha, kama huna fedha basi ukae pembeni.

Mwalimu Nyerere aliwahi kusema; ‘Rushwa ni adui wa haki,’ hivyo kutokana na kukithiri kwa vitendo vya rushwa ndani ya CCM, haki ikatoweka. Ni nguvu ya pesa tu.

Ndio sababu katika mchakato wa kupata wagombea wa nafasi mbalimbali ndani ya chama hicho mwaka jana (2015), ilibidi Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa (Takukuru), ifanye kazi usiku na mchana baada ya kuwapo vilio kutoka kila kona ya Tanzania.

Wahenga walisema; ‘dalili ya mvua ni mawingu’, mabadiliko yanayotarajiwa kufanyika Jumamosi, yana viashiria vya kutosha kuonyesha CCM inaenda kuzaliwa upya, ingawaje wanaotarajiwa kufanya mabadiliko hayo si malaika, ni binadamu kama wote tulivyo, hivyo mapungufu ya hapa na pale hayatakosekana.

Tangu Rais Magufuli aingie Ikulu mwishoni mwa mwaka jana, ameonyesha uthubutu wa hali ya juu katika kukabiliana na maovu ndani ya Serikali, jitihada ambazo bila shaka yoyote zitahamia CCM.

Kutokana na ukweli huo, tetesi za hofu miongoni mwa wahafidhina ndani ya chama hicho zimezagaa, kwa sababu ile CCM ambayo baadhi waliigeuza kama kampuni binafsi, sasa inaelekea kuzikwa na kuzaliwa upya.

Wana-CCM na Watanzania wengine hawatarajii tena kuona chama kikiendelea na utaratibu hatari kabisa wa ‘kiimla’, ambapo tulianza kushuhudia watu wakirithishana madaraka bila aibu kuanzia ngazi ya chipukizi hadi Taifa.

Mwenyekiti mpya atakapokuwa anafanya mabadiliko ambayo bila shaka yoyote yatakuwa machungu kwa baadhi ya wanachama, asonge mbele, apuuze kelele.

Anapaswa kurejea kisa cha Mwalimu Nyerere kuhusu vijana waliokuwa wanakwenda kuchumbia katika kilima fulani, ambapo kabla ya kuanza safari walikuwa wakikutana na ajuza mmoja, ambaye aliwapa onyo la nini kitawakuta katika safari hiyo

Ajuza huyo aliwaambia kuwa watu wa kule kilimani wana tabia ya kuzomea na kutisha kwa kelele nyingi sana, lakini kijana anayekwenda kuchumbia hapaswi kamwe kutikiswa na kelele hizo na kugeuka nyuma, kwa sababu akigeuka atakuwa jiwe.

Pamoja na onyo hilo, vijana wengi walijaribu kumfikia binti, lakini hawakuweza, waligeuka nyuma na kuwa mawe, lakini mwisho wa siku aliibuka kijana mmoja ambaye pamoja na kelele nyingi, kamwe hakugeuka na ndiye alimpata binti na kumuoa.

Watanzania wanataka kumuona binti safi (CCM), hivyo Mwenyekiti mtarajiwa kabla ya kumpata binti, kelele zitakuwa nyingi sana, kamwe usigeuke nyuma. Watangulizi wako inawezekana walimtamani sana binti huyo, lakini walishindwa kuhimili kelele za huyo, huyo huyo, mpige huyo, mchinje huyo. Wakageuka nyuma. Usigeuke.

Tena kelele zipo zinasikika kweli; huyo huyo dikteta, huyo huyo hashauriki, huyo huyo mbabe, huyo huyo haambiliki, huyo huyo katunyang’anya pesa, huyo huyo anavunja Katiba na nyinginezo nyingi.

Unakabidhiwa chama huku kukiwa na makovu mabichi kabisa yatokanayo na purukushani za Uchaguzi Mkuu uliopita, maana yake bado baadhi ya wana-CCM wamenuna, wamesusa na wengine wamezira.

Hali si shwari, kwani kuna aliyewania kuteuliwa kupeperusha bendera katika uchaguzi uliopita, lakini hakufanikiwa, yeye ameweka bayana kabisa kuwa baada ya vikao vya Halmashauri Kuu kumalizika Ijumaa (Julai 22), atarejea nyumbani, kwa sababu eti haoni sababu ya kushiriki Mkutano Mkuu. Ndio hali ilivyo CCM.

Ni wengi ndani ya chama ambao kwa dhati kabisa wanaamini hawakutendewa haki kwenye hatua za mchujo mwaka jana, hawa CCM inabaki kuwa adui kwao na ni miongoni mwa viongozi, hivyo chama hakipo salama, unaweza kukiona salama kwa nje, lakini ndani hali si shwari.

Ni ukweli usiopingika kuwa, uelewa wa mwenyekiti mtarajiwa kuhusu utendaji wa kila siku ndani ya chama pamoja na taratibu na tamaduni nyingine ni mdogo kutokana na historia yake kiutendaji, lakini siku zote dhamira ya kweli hushinda.

Hakuna popote katika historia ya Rais Magufuli ambapo aliwahi kukitumikia chama tofauti na ilivyo kwa Mwenyekiti anayestaafu Kikwete, ambaye wakati anakabidhiwa uenyekiti tayari alikuwa anakijua chama ipasavyo.

Hata tukirejea ushuhuda wako wakati wa kampeni, ulikiri kuwa hukujua kama ndani ya chama kuna wanafiki, mchana mnacheka na kula ugali pamoja, usiku wanakwenda upande wa pili.

Hivyo ufahamu kuwa unakwenda kuongoza chama kilichosheheni wanafiki na kazi ya kusafisha wanafiki si ndogo, inahitaji utulivu wa hali ya juu pamoja na busara, vinginevyo unaweza kujikuta unamwaga pumba pamoja na mchele safi jalalani.

Kama hazina kubwa ya viongozi wakiwamo wastaafu utaitumia vizuri, uwezekano wa kutetereka kwenye kiti cha uenyekiti ni mdogo sana na mwelekeo wa uongozi wako utaonekana katika sekretarieti mpya inayosubiriwa.

Wenye hekima waliwahi kusema; ‘Vijana wana nguvu ya kukimbia kwa kasi kubwa, lakini wazee hawawezi kukimbia, ila wanaijua njia’. Waonyeshe wanaodai hushauriki kuwa unashaurika, na unafanyia kazi ushauri, hasa ushauri wa wazee, ili usije potea njia, wakakucheka.

0755961538

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,690FollowersFollow
574,000SubscribersSubscribe

Latest Articles