24.7 C
Dar es Salaam
Monday, November 18, 2024

Contact us: [email protected]

Nigeria, DRC kuongoza kuwa na watu masikini duniani 2050

JOSEPH HIZA NA MTANDAO

KASI ya ukuaji wa idadi ya watu katika baadhi ya mataifa masikini barani Afrika inaweza kukwamisha maendeleo yanayoelekea kufikiwa ya upunguzaji umasikini duniani na uimarishaji wa huduma ya afya, ripoti ya Taasisi ya Bill & Melinda Gates inaonya.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo mpya iliyozinduliwa hivi majuzi, idadi ya watu barani Afrika inakua kwa kasi ambapo kufikia mwaka 2050 itakuwa imeongezeka maradufu ya ilivyo sasa.

Katika ongezeko hilo, asilimia 40 ya watu masikini kabisa duniani wanahofiwa watakuwa wakitokea katika mataifa mawili tu ya bara hili; Nigeria na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).

Kwa sasa, barani Afrika wanaishi watu bilioni 1.3 na miaka 32 ijayo, idadi hii itaongezeka maradufu zaidi.

Na iwapo ukuaji wa kiuchumi hautakwenda sambamba na ongezeko hilo la idadi ya watu, basi kitakachotokea ni ongezeko la umasikini.

Wasiwasi huo umeufanya mfuko huo wa mwanzilishi wa Kampuni ya Microsoft, Bill Gates, kufanya utafiti wa namna ya kukabiliana na kitisho kijacho.

Yaliyogunduliwa na utafiti huo uliopewa jina la ‘Walindamlango 2018’ ni kwamba ifikapo mwaka 2050, asilimia 40 ya watu walio masikini zaidi duniani watakuwa wanaishi kwenye mataifa mawili tu: Nigeria na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo DRC), ilisema.

Hivi sasa, Nigeria inakaliwa na watu milioni 190, ambapo kwa wastani mwanamke mmoja huzaa watoto watano, na hilo lina matokeo yake, kwa mujibu wa Farouk Jega, Mkurugenzi wa Wakfu wa Bill na Melinda Gates nchini Nigeria:

“Tayari hali ni mbaya hapa Nigeria. Umasikini wa kutupwa unazalisha hali ya ukosefu wa usalama, machafuko, uhalifu. Lakini Serikali ya Nigeria inajaribu kukabiliana na ongezeko hili la kupindukia la idadi ya watu.”

Wizara ya Afya anapigia kampeni njia za kisasa za uzazi wa mpango. Lakini ni asilimia 10 ya wanawake wanaotumia njia hizo, ambayo ni idadi ndogo. Gharama pia ni kubwa, hasa kwa wanawake na familia za kimasikini,” anasema Jega.

Anasema vijana wa Kiafrika wanaongezeka kwa wingi huku kukizidi kuwa na watu wachache wenye uwezo wa kuhimili mazingira ya kiuchumi na kiafya huku wakishindwa kujikita katika kupanga na kuwekeza kwa ajili ya wakati ujao.

Hilo linakuja huku mwasisi mwenza huyo wa Bill and Melinda Gates Foundation (BMGF), Bill Gates, akitoa wito kwa Serikali ya Nigeria kuongeza juhudi za kuwekeza katika maendeleo ya binadamu kwa vile yatawezesha nchi kuelekea kufanikisha Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDG) 2030 yaliyowekwa na Umoja wa Mataifa.

Aidha, Juni mwaka huu, Taasisi ya Brookings Institution iliripoti kwamba Nigeria imeipiku India kama taifa lenye idadi kubwa ya watu maskini zaidi duniani kwa watu wake milioni 87 wanaishi katika umasikini uliokithiri.

Kadhalika, Machi mwaka huu, Shirika la Kimataifa la Fedha (IMF) lilisema Wanigeria wanazidi kuwa masikini kutokana na ukosefu wa mageuzi ya kutosha na fanisi ya kiuchumi.

Hata hivyo, ripoti ya BMGF ilifichua kwamba mwelekeo wa demographia unaonesha watu bilioni moja wameweza kujinasua kutoka umaskini kipindi cha miaka 20 iliyopita.

Lakini, iliongeza kuwa mlipuko wa idadi ya watu, hasa Afrika, unatoa changamoto ya anguko la idadi ya watu walio katika umasikini uliokithiri duniani na inaweza kuanza kuongezeka zaidi.

Kama ilivyo kwenye mataifa mengine mengi ya Afrika, jukumu la mwanamke nchini Nigeria ni lile lile la kuzaa, kulea watoto na kuhudumia nyumba.

Serikali ya Nigeria inapambana kubadili mtazamo huu kwa kushirikiana na asasi za kijamii, viongozi wa kidini na kimila, anasema Faouk Jega, ambaye anaona kuwa kuna aina fulani ya mafanikio kwenye ushirikiano huu.

Angalau sasa raia wako tayari kujadili faida na hasara za kuwa na watoto wengi na ile mila kwamba mwenye watoto wengi anakuwa amejijengea uhakika wa kuwa na watu wa kumuangalia afikapo umri wa uzeeni.

Hata hivyo, mkurugenzi huyo wa BMGF nchini Nigeria, anakiri kuwa: “Panahitajika juhudi kubwa zaidi kubadili imani na mitazamo ya watu.”

Njia moja nzuri kabisa kuwezesha hili, ni kutoa elimu zaidi kwa wanawake na kuwapatia vyanzo vya kujipatia kipato, anaamini Farouk Jega, kwani changamoto hizi zapaswa kugeuzwa kuwa fursa. Hata hivyo, hadi sasa idadi ya vizazi haijashuka.

Taasisi ya Gates inaona kwamba kutoa elimu ya afya na kuwekeza kwenye elimu ya vijana kutatatua tatizo hili kwa ufanisi zaidi.

“Ikiwa kila mwanamke barani Afrika angekuwa na uwezo wa kuamua idadi ya watoto awatakao, basi idadi ya watu barani humu ingepungua kwa asilimia 30”, unaandika wakfu huo.

Alisa Kaps wa Taasisi ya Idadi ya Watu na Maendeleo ya mjini Berlin, Ujerumani, anasema ifikapo mwaka 2050, Nigeria itakuwa na watu zaidi ya milioni 400 na DRC Kongo itakuwa na idadi mara mbili ya ilionao sasa, lakini kwenye mataifa yote mawili, hakuna uhakika ikiwa kutakuwa na chakula cha kutosha wala miundombinu ya kiafya ya kuwahudumia watu hao.

“Ongezeko hili la idadi ya watu kwa Kongo na Nigeria ni kubwa mno kwa nchi na halilingani na uwezo wa kuwahudumia. Kawaida, ukuaji wa uchumi unatakiwa kwenda sambamba na ukuaji wa watu, lakini uchumi na ustawi hauwezi kukua kwa kasi moja na watu,” anasema Kaps.

Frederick Okwayo wa Shirika la Idadi ya Watu la Umoja wa Mataifa (UNFPA) mjini Johannesburg, Afrika Kusini, anasema katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, shughuli za maendeleo zimekwazwa na vita vya mara kwa mara.

“Hali inazidi kuwa ngumu kwa sababu ya miundombinu mibaya, lakini tunajaribu kufika kwenye makambi ya wakimbizi na kuwasaidia watu, ukiwamo ushauri wa mambo ya familia,” anasema Okwayo.

Anasema kwenye suala hili la uzazi, lililo muhimu kwa mataifa takribani yote ya Afrika ni ulazima wa wanaume kushiriki kwa kuuona umuhimu wa kuwa na familia ndogo. Serikali pia zinapaswa kuwa madhubuti kwenye kuongoza mageuzi na kuyasaidia mashirika ya misaada.

Anasema kuwa kwenye jukumu la serikali, panakuja suala la tofauti za kiitikadi. Bado kuna viongozi barani Afrika ambao hawaamini kabisa suala la kuzuia uzazi.

Ripoti hiyo inakuja huku hivi karibuni Rais John Magufuli wa Tanzania akinukuliwa akiwashauri wanawake kuacha kutumia njia za kuzuia kizazi, kwani taifa hilo lina uhitaji wa watu wengi zaidi.

Aidha, takwimu za Umoja wa Mataifa zimeonesha kwamba Afrika itajumuisha nusu ya ukuaji wa idadi ya watu wote duniani kati ya mwaka 2015 bna 2050, huku idadi yake ya watu ikitarajia kukuwa maradufu mwaka 2050 na ongezeko lingine maradufu mwaka 2100.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles