Na Shermarx Ngahemera
KAMPUNI ya Taifa ya Uwekezaji (NICOL) ya wazalendo imepitia majaribu makubwa na sasa imeanza kupata faida baada ya kupata uongozi mpya na imeanza kutoa gawio kwa wanahisa wake baada ya miaka takriban zaidi ya 10 ya sintofahamu na vuta nikuvute.
NICOL ni kampuni ya kizalendo ilianzishwa kwa ushirikiano wa karibu baina ya Serikali na vyombo vyake, pamoja na viongozi mbalimbali, wabunge na wananchi ili kuhamasisha uwekezaji kwa wazalendo na hivyo kupata tokea mwanzo mwitikio mkubwa kutoka kwa watu wengi kununua hisa.
Hadi sasa NICOL ni kampuni pekee ya kizalendo yenye uzito mkubwa wa uwekezaji na mtaji mkubwa kushinda makampuni yote ya kizalendo (collective investment scheme).
Pamoja na changamoto nyingi za awali za kiuongozi hali ya kampuni sasa imeimarika baada ya wanahisa kuweka uongozi mpya madarakani na faida kupatikana na kampuni kuanza kutoa gawio kwa wanahisa wake.
Nilipomwuliza Dk Gideon Kaunda, Mwenyekiti wa NICOL katika mahojiano mahsusi ofisini kwake alisema kwa kujiamini kuwa mambo ni shwari na hiyo inathibitishwa na kampuni hiyo kushinda kesi zote 43 za kupandikiza zilizokuwa zimetengenezwa na utawala king’ang’anizi uliopita ambao ulijitahidi kuhujumu kampuni hiyo kwa mengi ili usitoke madarakani.
Anasema masahibu ya hujuma kwa kampuni ya NICOL yameainishwa vilivyo katika Ripoti yake ya mwaka 2016 ambayo inalaani uongozi uliopita kwa kukosa weledi na uzalendo kwenye mambo mengi.
Anasema kampuni ya NICOL pamoja na kuhujumiwa na kuwa kimya kwa miaka 13 bila kutoa gawio imeweza kufanya kazi na kupata faida na sasa mtaji wake ni zaidi ya shilingi bilioni 100 na inatafuta mahala pazuri pa kuwekeza kwa kupanua wigo wake.
Anasema tokea awe kiongozi wa NICOL ameweka juhudi yake zaidi kwenye utawala bora na uwekezaji wenye tija ambao sasa matunda yake yameanza kuonekana.
“Tumeweza kutayarisha na kufanya mahesabu ya Kampuni kutokea 2009 na kwa mwaka 2016 na hivyo kuweza kufanya mkutano tarehe 2 Disemba mwaka jana (2017 ) ambapo wanahisa 600 walihudhuria Mkutano Mkuu wa Mwaka ingawa uongozi uliotangulia uliweka pingamizi la mkutano huo usifanyike lakini Mahakama ilitupilia mbali kutokana na kukosa sababu ya msingi .”
Kutaka kurudi DSE
Dk Kaunda anasema lengo la kwanza ni kurudi kwenye soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE) ambako kampuni iliwahi kusimamishwa mwaka 2011 kufuatia Menejimenti ya NICOL kushindwa kufuata masharti ya lazima ya kuendelea kuweko kwenye Orodha ya DSE (Continuing Listing Obligations ) kwa kufanya kwa kificho maamuzi mengi muhimu ya uwekezaji yakiwemo manunuzi na mauzo bila kuishirikisha DSE na bodi ya Wakurugenzi wa NICOL na hivyo kuwa batili.
Matendo hayo ni kinyume cha taratibu na kanuni za miongozo ya Soko la DSE na hivyo Kampuni kupoteza fedha nyingi kutokana na kukosa kuzingatia mwenendo sahihi wa uendeshaji kampuni ya umma (plc) kama NICOL na hivyo kutumbukia katika lindi la madeni kwa wakati fulani yalifikia kiasi cha shilingi bilioni 11.5 ingawa kwa sasa madeni hayo yamelipwa na uongozi mpya.
Anasema mambo ni moto moto kwa bodi mpya.
Bodi mpya chini ya Dk Kaunda anasaidiwa na wajumbe Joyce N. Nyanza na Mhandisi Ladislaus Salema na Mwanasheria Benjamin Mwakagamba.
“Kazi yetu ya kwanza ilikuwa ni kuinusuru kampuni kutokana na matishio mbalimbali ya kisheria na kiutawala kitu ambacho kampuni imefanikiwa kwa kushinda kesi zote 43 mahakamani , imelipa madeni na hakuna kesi iliyobakia na sasa mambo ni shwari na hivyo tumeanza kutoa gawio kwa wanahisa wetu,” anaeleza Dk Kaunda.
Ripoti hiyo ya mwaka 2016 yenye kurasa 80 imeeleza kwa marefu na mapana mwenendo wa Uongozi uliopita na ubadhirifu uliofanyika na mwishowe mahakama kuutupilia mbali nje ya kampuni.
Matendo ya uongozi uliopita ulifedhehesha sana mwenendo wa NICOL na kitendo cha Mahakama Kuu kufukuza na kupiga marafuku wale wote waliohujumu NICOL ni matendo yaliyopongezwa na wote wapenda maendeleo ya haki kwenye Mkutano Mkuu mwaka jana.
Mwaka jana NICOL imedai kupata faida ya shilingi bilioni 8.67/- baada ya kodi na kutoa gawio la shilingi 252/- kwa hisa kwa kampuni ambayo ilianza mwaka 2004 na wanachama wenye hisa 148 na mtaji wa shilingi milioni 140/- . Kampuni ina mtaji ulioidhinishwa wa shilingi Bilioni 200 na kugawanywa kwenye hisa bilioni 1.6 kwa bei ya shilingi 125 kwa kila hisa.
Mwenyekiti Kaunda anatoa ahadi ya kulipa gawio kila mwaka kuanzia sasa kwani biashara ni nzuri hasa wakati huu ambapo nchi ina mipango ya uchumi wa viwanda na hivyo kufungua milango ya uwekezaji mpya kwa marefu na mapana.
Anasema, Kampuni ina rasilimali za kutosha kwani ina hisa katika makampuni tisa makubwa zenye thamani isiyopungua shilingi bilioni 100/- wakati wana amana yao Benki Kuu ambayo iko hapo kuanzia mwaka 2011 na haijaguswa. Makampuni hayo yahaja yanayofanya shughuli zake katika Soko la Hisa la Dar es Salaam ni Benki za NMB, CRDB, Tanzania Breweries, Swissport, Simba Cement, Twiga Cement, Vodacom, TCC na DSE.
“Kampuni nayo iliwahi kuwekeza kwenye vitalu huko Mtwara na vimetengeneza faida na katika benki ya NMB Kampuni ina umiliki wa asilimia 6.6 na asilimia 3.3 hisa za DSE,” anafichua Mwenyekiti.
Anasema Dk Kaunda kuwa kimsingi ukiachia mambo ya hujuma zilizofanywa na uongozi uliopita uwekezaji wa NICOL ulikuwa mzuri na wa kimkakati kwani uwekezaji kwenye benki, vitalu, viwanda viwili vya kuchakata nyama ya ng’ombe na mbuzi na kiwanda cha kuchakata samaki vyote vilianza vizuri lakini uongozi uliokuwepo wakati huo ulivuruga na kuleta sintofahamu nyingi kwa vitendo vyake vilivyokosa uwazi, uaminifu kwenye masuala mbalimbali yanayohusu kampuni ya NICOL.
Dk Kaunda anasema mara nyingi vitendo viovu kama vilivyoonekana kwenye kesi 43 mbalimbali viliweza kuathiri na kutishia ustawi wa kampuni kutokana na kukithiri matendo ya kulana kisogo, kukosa uaminifu, ustadi na kukosa weledi wa kitaaluma wa uendeshaji mambo. Lakini hiyo ni historia kwa sasa na hivyo anawakaribisha watu wote kununua hisa za NICOL pale ambapo tangazo litakapotoka la kurudishwa tena Sokoni.
“Hali ya kifedha ni nzuri baada ya kulipa kodi ya Serikali pamoja na malimbikizo mbalimbali ya madeni na hivi sasa tuko tunafuatilia mambo ya uwekezaji ili tukirudishwa sokoni shughuli zianze kwa kwenda shoti.”
Anasema pamoja na Matatizo yote waliyopitia wanaendelea kuhakikisha mtaji wa NICOL unaimarika ili kuleta maendeleo na mafanikio makubwa kwa wanahisa katika siku za usoni.
Mwenyekiti anasema Kampuni imekatishwa tamaa na maamuzi mengine ya mikataba ya kitapeli ambayo yameifanya baadhi ya miradi kuchukuliwa na wapangaji wao na NICOL kubakia kama mchinjaji wa nyama badala ya kuwa mwuzaji wa nyama katika viwanda vyake anavyomiliki.
“Viwanda vya nyama vya Tanzania Meats Company (TMC) na East Africa Meat company vinauwezo wa kuchinja ng’ombe 300 na mbuzi 500 kwa siku na kuuzwa Irak na Vietnam lakini kasoro kubwa ni kuwa mauzo hayo yalifanyika kwa fedha tasilimu (cash) na hivyo hakuna taarifa rasmi ya hujuma hiyo kwani biashara inafanywa na kampuni tanzu ya Ako. Kwa vile Nicol ni kampuni ya Umma imeanzisha Ukaguzi wa kijinai (forensic audit) ili kuchunguza kwa kina mwenendo mzima wa uendeshaji wa kampuni na hasara zilizopatikana ili kutambua nafasi ya kila mhusika katika kusababisha hasara ya fedha na kuipaka matope kampuni kwa kuhisiwa kuwa na mwenendo mbaya wakati ni matendo ya watu binafsi na sio kampuni husika.
Hali hiyo inaonesha kipato cha NICOL ni kidogo wakati biashara ni nzuri na ya faida kubwa na kuiweka kampuni katika nafasi nzuri.
Lakini Mwenyekiti Kaunda anajulikana katika utendaji na usimamizi mzuri wa miradi kwani mwaka 1995 hadi 2000 aliweza kuanzisha na kuendesha ‘Alliance Air’ ambayo ilikuwa ina ndege zilizokodishwa na Air Tanzania na ilikuwa inaiingizia faida serikali kiasi cha Dola milioni 30 kwa mwaka.
Walipokuja Shirika la Ndege la Afrika ya Kusini (SAA) walipata hasara hadi walipoondolewa kwa kushindwa kujiendesha kibiashara.