Na Editha Karlo,Kasulu
MGOMBEA ubunge Jimbo la Kasulu Mjini, Profesa Joyce Ndalichako (CCM), amewataka wananchi wa Wilaya ya Kasulu kumchagua kuwa mbunge wao ili aipaishe wilaya hiyo kwa maendeleo.
Amesema atafanya kazi kubwa ya kuhakikisha maendeleo yanakuja kwa kasi sambamba na kusimamia masuala muhimu ya wananchi.
Ndalichako aliyasema hayo juzi kwenye viwanja vya Umoja mjini Kasulu wakati wa uzinduzi wa kampeni zake za ubunge.
Aliwaomba wananchi kukichagua chama chake ili kiweze kushika dola. Alisema tahakiksiha anaendeleza ujenzi wa miundombinu ya barabara ya ndani ili kuwasaidia wananchi kusafirisha mazao yao.
“Mimi sikuwa mwanasiasa, nilipata ubunge wa kuteuliwa ila nina ifurahia, siasa ninaipenda, waomba wananchi wa Kasulu Mjini mnichague niwe mtumishi wenu niwaletee maendeleo,” alisema.
Alisema miaka mitano ijayo, ilani ya chama imeelekeza kuhakikisha wanapata tija katika mazao yao na vijiji vyote ambavyo havina umeme na maji vinapata huduma hiyo ili kufanikisha mpango wa Serikali ya CCM hadi kufikia mwaka 2025, Tanzania inakuwa nchi ya kuigwa barani Afrika.
“Mimi ni mwanamke mpambanaji,mnyenyekevu naweza kwenda popote nikajishusha na kuomba nikasikilizwa mkinichagua nitakuwa kinara wa kupambania maendeleo, nitapambana hadi kieleweke”alisema
“Wakati nikiwa mbunge wa kuteuliwa nimefanya mengi katika wilaya yetu,sekta za miundombinu ya elimu,kutoa mikopo kwa kina mama na vijana na kuboresha miundombinu ya barabara za ndani nipeni miaka mitano niwe mtumishi wenu mnitume jambo lolote nitafanya.
“Sasa nawaomba wana Kasulu wenzangu tumpe kura nyingi za ushindi wa kishindo Rais wetu John Magufuli na madiwani wote msinichanganyie rangi za madiwani, nawaombeni sana nipe madiwani wa chama cha mapinduzi ili jifanye nao kazi vizuri,”alisema
Mbunge mteule kundi la vijana (UVCCM), Sylivia Sigula aliwataka wananchi kuchagua mafiga matatu ambayo ni rais,mbunge na madiwani ili waweze kufanya kazi ya kuwaletea maendeleo wanaKasulu kwa kushirikiana.
“Nawaomba mumpe kura nyingi za kishindo Rais wetu John Magufuli pia mchague madiwani wote wa chama cha mapinduzi ili waweze kumsaidia mbunge kufanya kazi mkimchanganyia madiwani mtakuwa mmevunja miguu hataweza kutembea,pia ukinununua tochi mpya katika tochi hiyo ukaweka betri mbili na gunzi moja hiyo tochi itawaka kweli?mmenunua tochi iwekeni betri tatu ili iweze kuwaka vizuri”alisema.