29.2 C
Dar es Salaam
Monday, November 25, 2024

Contact us: [email protected]

‘Ni kazi ngumu kuwadhibiti watumiaji dawa za kulevya’  

Watumiaji wa dawa za kulevya wakijidunga sindanoNA TUNU NASSOR, ALIYEKUWA PWANI

ONGEZEKO la vijana wanaotumia dawa za kulevya nchini limezidi kuleta changamoto kubwa katika jamii kutokana na kukithiri kwa vitendo vya uhalifu.

Waathirika hao huiba vitu mbalimbali vikiwamo vyombo, nguo zilizoanikwa kwenye kamba na kuziuza kwa bei rahisi ili wapate fedha za kununulia dawa za kulevya.

Changamoto hii inawakumba zaidi kundi la vijana wenye umri kati ya miaka 20 na 35.

Kwa kuliona hilo, serikali ya awamu ya nne iliyokuwa ikiongozwa na Rais Mstaafu, Jakaya Kikwete, ilitoa wito kuanzishwa kwa vituo vya kuwasaidia waathirika wa dawa za kulevya kila mkoa.

Kituo cha Filbeth Bayi Drugs Rehabilitation kilianzishwa Julai 13, 2013 kikiwa na lengo la kutoa msaada kwa wakazi wa Mkoa wa Pwani, waliothirika na dawa hizo.

Mratibu wa kituo hicho, Felix Swai, anaeleza namna walivyoanzisha kituo hicho kwa kusema kuwa mkurugenzi wa kituo hicho, Filbert Bayi ndiye aliyetoa nyumba, vyakula na mahitaji muhimu kwa ajili ya waathirika.

Anasema walitafuta mwalimu ambaye alikuwa na uzoefu wa kuongea lugha za kijiweni na kuweza kuishi nao.

“Baada ya kuanzishwa kwa kituo hiki tulianza kupokea waathirika wengi kutoka kwa wazazi na jamaa na tunakaa nao kwa miezi minne.

“Wanafundishwa namna ya kuacha dawa hizi, pia hufundishwa kazi za ujasiliamali kama kutengeneza sabuni, dawa za chooni, kulima bustani za mboga, ufugaji wa kuku na wanajifunza masomo ya kompyuta,” anasema Swai.

Anasema wanajivunia kuwasaidia vijana zaidi ya 40 waliokuwa wameathirika na sasa wanajitegemea.

“Waliosoma kompyuta wameweza kufungua ‘internet café’ ambazo zinawasaidia kuwaingizia kipato na kuendesha maisha yao,” anasema.

“Vijana wawili waliweza kurudi shule na kurudia mitihani huku mwingine akijiunga na mafunzo ya ufundi stadi,” anasema.

Pamoja na mafanikio hayo, Swai anataja changamoto wanazoikumbana nazo kuwa ni pamoja na miundombinu finyu hasa majengo ya kumudu kupokea waathirika wengi zaidi, ambapo lililopo sasa linauwezo wa kuchukua watu 20 tu.

“Kundi kubwa la wasichana pia wamejiingiza katika jambo hili, kwa kuwa hatuna miundombinu ya kutosha, hatuwezi kuwachukua kwa sababu hatuna pa kuwaweka,” anasema.

Anasema baadhi ya waathirika hao wengine wanaishi na virus vya Ukimwi, maradhi waliyoyapata baada ya kuchangia sindano za kujidunga.

“Upatikanaji wa maji safi na salama nao ni changamoto, hasa ukizingatia kuwa wagonjwa hao hutumia maji mengi ili kuipoza miili baada ya kuacha dawa za kulevya,” anasema.

Anaongeza kuwa jengo hilo linahitaji kuwekewa uzio kwa kuwa wengine hutoroka kutokana na kuzidiwa na hamu ya unga hivyo uliopo ni rahisi kuuruka.

Anasema ni kazi ngumu kuwadhibiti bila ya kuwa na uzio katika eneo wanaloishi

Swai anasema usaidizi kutoka kwa wadau mbalimbali ikiwamo serikali ni mdogo hivyo kulazimika kuchukua wagonjwa wachache.

“Kwa kuwa lengo letu ni kuwasaidia wengi zaidi waliopo Mkoa wa Pwani na kwingineko, jitihada zaidi zinahitajika ili kuwafikia.

“Jamii ijitolee kuwasaidia watu hawa ili waweze kurudi katika hali zao za kawaida kwa kuwapeleka katika vituo vya tiba,” anasema Swai.

Anasema ikiwa serikali za mitaa na vijiji vitaitisha vikao vya wananchi na kuwachangia gharama za matibabu na vyakula kwa waathirika, ingesaidia kupunguza wimbi la watu hawa mitaani.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles