33.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, November 26, 2024

Contact us: [email protected]

Ni janga

Ajali 2Ajali 1Na Waandishi Wetu, Dar na Kahama
WATU 38 wameripotiwa kupoteza maisha jana katika matukio ya ajali mawili tofauti yaliyotokea kwenye mikoa ya Mbeya na Shinyanga.
Taarifa zilizokusanywa na MTANZANIA Jumamosi kutoka Mbeya na Shinyanga, zilieleza kuwa tukio la kwanza lilitokea eneo la Uwanja wa Ndege, Kata ya Kiwira, wilayani Rungwe, mkoani Mbeya, ambako gari aina ya Toyota Hiace lenye namba za usajili T 290 ADU, lililokuwa kwenye kasi lilipinduka baada ya kushindwa kukata kona.
Tukio hilo lilithibitishwa na Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mbeya, Ahmed Msangi, ambaye alieleza kuwa ajali hiyo iligharimu maisha ya watu 19 na kujeruhi wawili ambao wamelazwa katika Hospitali ya Igogwe, iliyopo Wilaya ya Rungwe.
Kamanda Msangi alisema chanzo cha ajali hiyo ni mwendo kasi uliosababisha dereva wa gari hilo kushindwa kukata kona na kugonga gema ambalo liliisukuma gari hiyo kutumbukia mtoni.
“Tukio hilo limetokea leo (jana) saa 3:00 asubuhi baada ya Hiace yenye namba za usajili T 290 ADU iliyokuwa ikitokea jijini Mbeya kwenda Kiwira, ikiwa imebeba wafanyabiashara waliokuwa wanakwenda kwenye mnada huko Kiwira, wilayani Rungwe kushindwa kukata kona.
“19 walifariki pale pale na miili yao imehifadhiwa katika Hospitali ya Igogwe iliyopo Wilaya ya Rungwe, wakiwemo dereva na kondakta na walionusurika ni wawili ambao wamelazwa Hospitali ya Igogwe, wilayani Rungwe,” alisema Kamanda Msangi.
Aidha, Msangi alisema taarifa za awali za uchunguzi wa chanzo cha ajali hiyo zilieleza kuwa sababu ya dereva wa Hiace kuendesha gari kwa mwendo kasi ni kuwakimbia madereva wa magari ya abiria aina ya Coaster yanayofanya safari zake kwenye miji ya Mbeya, Kyela na Rungwe, waliokuwa wakimfukuza kwa kutumia gari ndogo baada ya kumuona kapakia abiria.
Alisema madereva wa magari hayo wako katika mgomo na wanawazuia madereva wa magari mengine kubeba abiria.
Naye mmoja wa mashuhuda wa ajali hiyo aliyekuwa kituo cha mabasi cha Nanenane ambako Hiace iliyopata ajali ilianzia safari yake, alilieleza gazeti hili kuwa mgomo wa madereva wa Coaster ni kupinga taratibu na sheria za usalama wa barabarani, na pia kupinga faini ya Sh 250,000 aliyolipishwa dereva mwenzao.
Katika tukio jingine, Mwandishi Paul Kayanda kutoka Kahama anaripoti kuwa watu 19 wanahofiwa kufa baada ya kufukiwa na kifusi cha udongo katika machimbo madogo ya dhahabu ya Kalole, yaliyopo Kijiji cha Lunguya, Halmashauri ya Msalala, mkoani wa Shinyanga.
Taarifa zilizopatikana kutoka eneo la tukio na kuthibitishwa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga, Justus Kamugisha, zilieleza kazi ya kufukua kifusi kilichowafukia watu hao inaendelea sambamba na kuhakiki idadi ya watu waliokuwa kwenye shimo hilo.
Akizungumzia ajali hiyo, Diwani wa Kata ya Lunguya, Benedictor Manywali, alisema idadi ya watu waliofukiwa inaweza kuwa kubwa zaidi kwa sababu duara lililotitia lilikuwa na watu wengi wanaojihusisha na uchimbaji wa madini.
Katika taarifa yake, Kamanda Kamugisha alisema tukio hilo limetokea Aprili 17, majira ya saa 8 usiku, baada ya eneo hilo kukumbwa na uteketeke uliosababishwa na maji ya mvua kubwa inayoendelea kunyesha eneo hilo.
“Mpaka sasa naweza kusema chanzo cha kuanguka kwa duara hilo ni mvua zinazonyesha, hivyo mashimo yameingiliwa na maji, sasa kwa sababu wanachimba chini kwa chini, lilititia na hivyo kwa kuwa tumeambiwa kulikuwa na watu basi tunadhani watu hao wamefunikwa na kufa.
“Nimeshatuma kikosi cha polisi kwenda kusaidia kuokoa, lakini ya idadi ya watu waliokufa tumeambiwa kuwa ni 19, ila hatuna uhakika tunaendelea nayo.”

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles