Na Amina Omari-Tanga
MENEJA wa Mfuko wa Bima ya Afya wa Taida (NHIF), Mkoa wa Tanga, Ali Mwakababu, amesema moja ya changamoto inayowakabili ni udanganyifu kwenye kwenye fungu la wananchama wanaotakiwa kujiunga kwa vikundi (Kikoa).
Mwakababu alisema baadhi ya wananchi wamejiunga kupitia mfumo huo wakati wakiwa siyo wanakikundi.
Alisema kuwa fao hilo lilikuwa ni maalum kwa wajasiriamali lakini wanufaika wametumia fursa hiyo vibaya kwa kuwaingiza wanachama wasio stahiki .
“Tulilenga kuwasaidia watu wa hali ya chini waweze kunufaika na bima lakini wamekuwa wajanja kwa kusababisha mfuko kuingia gharama kubwa za kulipia matibabu yao,” alisema meneja huyo.
Alisema pia licha ya elimu inayoendelea kutolewa na NHIF kuhusu umuhimi wa bima ya afya, bado wananchi wanashindwa kutumia fursa hadi wakiwa wagonjwa.
Mwakababu alisema kuwa dhana ya kuwa na bima ya afya ni kwa ajili ikusaidie wakati ambapo unakabiliwa na magonjwa bila ya kuyumbisha kipato chako.
“Watanzania ni watu wajanja sana mtu anasubiri azidiwe na ugonjwa ndipo anapoona umuhimu wa kuwa na bima wakati angeweza kuwa nayo kabla,” alisema Mwakababu