Na Andrew Msechu – dar es salaam
RIPOTI ya Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali (CAG) kwa mwaka wa fedha 2017/18, inaonesha Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) lipo hatarini kupata hasara ya mabilioni ya fedha kutokana na miradi yake ambayo kwa sasa imesimama.
Inasema NHC ilianzisha mradi wa nyumba wa Golden Premier Residence (711-2) uliopo Kawe, Dar es Salaam Kitalu Na. 711/2 Oktoba 16, 2013 ambao hauendelei vizuri.
Ripoti hiyo inasema iwapo NHC haitapata kibali cha kukopa kutoka Wizara ya Fedha na Mipango kutokana na kufikia ukomo wake wa kukopa, itapaswa kuwalipa wakandarasi Sh bilioni 99.99 kwa kuvunja mikataba.
Pia, shirika hilo litatakiwa kurejesha Sh bilioni 2.6 kwa wateja waliokwishaanza kulipia malipo ya awali ya ununuzi wa nyumba hizo.
CAG Profesa Mussa Assad alisema katika mapitio yake, alibaini mradi huo ulisimama tangu mwanzo wa mwaka 2017 kutokana na ukosefu wa fedha.
“Hadi unasimama, mradi ulikuwa umekamilika kwa asilimia 30 na umetumia jumla ya Sh bilioni 34.87, ambapo vyanzo vya ndani vilichangia kiasi cha Sh bilioni 11.64 na mkopo kutoka Benki ya Uwekezaji Tanzania (TIB) ulikuwa ni Sh bilioni 23.23.
“Shirika la Nyumba la Taifa lilitakiwa kuanza kulipa marejesho ya mkopo kuanzia Julai 2018. Hivyo, Shirika linatumia fedha kutoka vyanzo vingine kulipa mkopo huo huku mradi ukiwa haujakamilika,” inasema ripoti hiyo.
Inasema mradi uliopo katika kitalu Na 711 Kawe, Kinondoni, Dar es Salaam ulianza Aprili 4, 2014 baada ya NHC kuingia mkataba na Estim Construction Company Limited wenye thamani ya Sh bilioni 105.11 pamoja na VAT kwa ajili ya usanifu na ujenzi kupitia zabuni namba PA/066/2011-2012/HQ/W/03 kwa muda wa wiki 156 toka siku ya kwanza ya ujenzi.
Ripoti hiyo inasema kufikia Novemba 4, 2014, NHC na Estim Construction Company Limited waliingia mkataba wa nyongeza kwa ajili ya kuhamisha mradi huo kutoka sehemu ya awali ulipokuwa umepangwa kutekelezwa katika eneo la Ngano kitalu namba 79-82 na kupelekwa kitalu namba 711-1 Kawe.
“Upembuzi yakinifu wa mradi huu ulifanywa Juni 2014; miezi miwili baadaye baada ya kusaini mkataba. Hii inaonesha kwamba mkataba ulisainiwa kabla hata ya kufanya upembuzi yakinifu kwenye mradi huo.
“Matokeo ya upembuzi yakinifu ni pamoja na gharama za ujenzi zilizokisiwa kuwa ni Dola milioni 69.43, sawa na Sh bilioni 114.4, muda wa ujenzi ulikadiriwa kuwa ni miaka mitatu hadi 2017, uliainisha vyanzo vya fedha za mradi, ambapo vyanzo vya ndani vitachangia asilimia 35 na mikopo itachangia asilimia 65,” inasema ripoti hiyo.
Inasema hadi Septemba 2017, NHC walibadili andiko la kibiashara na kuainisha kuwa gharama za mradi zitaongezeka hadi Sh bilioni 142.55, mradi utaisha baada ya miaka miwili, yaani mwaka 2019, na vyanzo vya fedha za mradi vitabadilika na kuwa vyanzo vya ndani vitachangia asilimia 37 na mikopo itachangia asilimia 63.
Ripoti hiyo inasema mradi ulisimama tangu mwanzoni mwa mwaka 2017 kutokana na ukosefu wa fedha na kwamba hadi wakati huo, ulikuwa umekamilika kwa asilimia 20 tu na ulishatumia Sh bilioni 26.31 kutoka katika vyanzo vya ndani.
“Kwa mujibu wa upembuzi yakinifu, NHC ilikuwa na uhakika wa kupata fedha kwa ajili ya mradi, lakini mpaka sasa imeshindwa kukopa kwa ajili ya ujenzi huo,” alisema CAG Assad.
Alieleza kuwa mkopo wa TIB uliochukuliwa Julai 6, 2015 ulitakiwa uanze kulipwa baada ya miezi 36 (Julai 2018), ikimaanisha kwamba kwa sasa NHC inatumia fedha kutoka vyanzo vingine kulipa mkopo huo, hivyo wakati wa kulipwa mkopo huo tayari ulishafika na ujenzi bado haujakamilika.
Ripoti hiyo inaeleza kuwa NHC imeshindwa kukopa benki baada ya kufika ukomo wa kukopa wa Sh bilioni 300, na wameomba kibali cha kuongeza mkopo toka Wizara ya Fedha na Mipango bila ya mafanikio.