24.7 C
Dar es Salaam
Sunday, November 17, 2024

Contact us: [email protected]

NGUVU ZA WANAWAKE, VISA, MIKASA NA BIASHARA

Na Markus Mpangala,

ULIMWENGU wa fasihi umeshuhudia vitabu mbalimbali vikitolewa na kuvuta hadhira kwa kiwango kikubwa. Miongoni mwake ni simulizi za Alfu Lela U Lela, ambapo hutafsiriwa kuwa Siku Elfu na Moja. Vitabu vyenye simulizi hizo vimekuwa vikichapwa katika matoleo tofauti.

Alfu Lela U Lela ni vitabu vyenye mfululizo wa mikasa na visa mbalimbali. Vinauzwa katika duka la vitabu la Tanzania Publishers Bookshop (TPH) jijini Dar es Salaam.

Mathalani kuna vitabu vilitungwa karne nyingi zilizopita lakini vikawafikia kwa wingi wasomaji katika karne ya 20 na karne ya 21 vikasambaa zaidi. Kutokana na mabadiliko ya teknolojia yamewezesha baadhi ya simulizi kuwekwa kwenye vitabu.

 MANDHARI

Katika bashraf ya kitabu hiki ni kwambaAlfu Lela U Lela’ ni mkusanyiko wa fasihi katika muundo wa visa kutoka Mashariki ya Kati.  Visa hivi vinatokana na kitabu cha zamani cha Kiajemi kiitwacho Hazar Afsana (Visa vya Ngano Elfu Moja). Inaaminika kuwa mtu aliyekusanya visa hivi na kutafsiri kwa Kiarabu ni mwandishi maarufu wa hadithi Abu abd-Allah Muhammed el-Gahshigar, ambapo alifanya kazi hiyo katika karne ya 14.

Tafsiri ya kwanza ya Kiarabu ya kisasa ilichapwa mjini Cairo, Misri mwaka 1835. Inasadikika kuwa visa hivi vilianza kukusanywa wakati Baghdad ilipokuwa kitovu cha biashara na siasa katika eneo la Mashariki ya Kati.

Wafanyabiashara toka ghuba ya Uajemi (Persia), China, India, Afrika, na Ulaya walikuwa wakitembelea mji wa Baghdad kwa ajili ya biashara na mambo mbalimbali ya kiuchumi.

 MAUDHUI

Visa vilivyoko kwenye vitabu hivi ni mkusanyiko wa mapenzi, misiba, ucheshi, mashairi, pamoja na visa vya dini ya Kiislamu. Tunaonyeshwa wanamazingaombwe na majini, huku visa maarufu zaidi vikiwa vya Taa ya Alladin, Baharia Sindbad, Ali Baba na Wezi Arobaini.

Kuna majina kama Khalifa Harun ar-Rashid na mshairi Abu Nuwas. Inaaminika kuwa visa vya Alladin na Ali Baba viliingizwa katika mkusanyiko huo karne ya 18 na Antoine Galland ambaye aliwahi kuvisikia visa hivyo kutoka kwa mtunzi wa hadithi wa Kimaroni kutoka nchini Syria.

Simulizi nyingi zinatoka katika jamii za watu wa India, Wayahudi, Iran, Ugiriki na Uturuki, ambavyo vinakifanya kitabu kizima kiwe cha kusisimua.

Mwanzo wa visa hivi ni kuudhiwa kwa mfalme Shahryar wa Kisiwa kilichoko kati ya India na China, baada ya kitendo cha mke wake kuwa na uhusiano wa kimapenzi nje ya ndoa.

Shahryar aliamua kumuua mke wake kama adhabu pekee iliyomfaa mke huyo. Kwa kuamini kuwa wanawake wote wako kama mke wake aliyemuua yaani si waaminifu alimwaamuru mtumishi wake awe anampatia mke kila usiku.

Baada ya kulala na mke wake mpya usiku, kunapokucha anawaamuru watumishi wake wamuue mke huyo.

Hali hii inaendelea hadi pale binti wa huyo mtumishi wake anapounda mbinu maalumu na kuamua kujitolea kuwa mke wa mfalme. Binti huyo jina lake ni Shahrazad, ambaye anatajwa pia kama Scheherazade au Shahrastini katika vitabu vya Kiingereza vya simulizi hizo.

Kila usiku baada ya ndoa yao, binti huyo anatumia saa kadhaa kumsimulia mfalme visa vitamu na vya kusisimua ambapo utamu wake unakuwa umekolea inapofika alfajiri, ambapo ni wakati wa kuuawa kwa mke wa mfalme baada ya kulala naye.

Kwa nia ya kujua mwisho wa kisa, mfalme alikuwa akiahirisha mauaji ya Shahrazad. Aliendelea kuahirisha kuuawa kwa mke wake hadi akapata naye watoto watatu! Ulipofika wakati huo aliamini kuwa mke wake huyo ni mwaminifu hivyo akabadili uamuzi wa kuua wake zake.

 DHAMIRA

Kulingana na hii ni sehemu fupi ya simulizi za Alfu Lela Ulela ambazo zilianza karne ya 14 mpaka kizazi cha sasa kinapofurahia hadithi hiyo. Ni kumbukumbu nzuri ambayo kizazi kipya kinatakiwa kujifunza maisha kwa ujumla.

Lakini jambo kubwa zaidi, mwandishi anatuonyesha namna gani jamii yetu imetawaliwa na ukandamizaji. Hukumu aliyopitisha mfalme dhidi ya tabia za wanawake haikuwa sahihi kwani si wote kwamba hawaaminiki katika maisha ya ndoa.

Mfalme amechorwa kama alama ya baadhi ya wanajamii ambao wanawatumia wanawake kama chombo cha starehe. Jambo hili mwandishi anaonekana kulikemea kwa njia ya kichekesho pale binti wa mtumishi anapokubali kuolewa kwa mfalme na kumsimulia visa mbalimbali.

Binti huyo amechorwa kama mwanamke asiye na nguvu wala mamlaka katika jamii, lakini ana uwezo wa kuwasilisha hisia zake na kutafuta ufumbuzi wa matatizo yanayoikabili jamii zetu.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles