Renatha Kipaka,Muleba
MKUU Wilaya ya Muleba, mkoani Kagera Toba Nguvila ameunda kamati ya kuchunguza migogoro ya ardhi katika Kijiji cha Ilemela Kata ya Gwasnseli, huku akiwataka viongozi wa Serikali ya kijiji hicho kuacha mara moja kugawa ardhi.
Akizungumza katika mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye Uwanja wa Ofisi ya Kijiji cha Ilemela leo Novemba 8,2021 Nguvila amewataka pia wananchi kuacha kuvamia ardhi bila kufuata sheria.
Amesema kuwa kwa mujibu wa sheria ya ardhi mwananchi hatakiwi kumiliki zaidi ya eneo la ekari 50, Serikali ya kijiji kupitia vikao na mkutano mkuu wa kijiji wana mamlaka ya kumpa mtu aliyeomba ardhi ekari chini ya 50.
“Katika kero zilizotolewa na wananchi wametajwa watu wengi waliojichukulia maeneo bila kufuata utaratibu. Sasa naunda kamati ya uchunguzi ili ije hapa kufanya uchunguzi kwa muda wa wiki mbili kuanzia tarehe 08.11.2021 na kamati hiyo itakuwa na mtu wa TAKUKURU kwa sababu kutokana na maelezo ya wananchi inaonekana harufu ya rushwa.
“Pia kamati itakuwa na mtaalam wa ardhi ambaye ataongoza, atasanifu na kuhakiki taratibu zote kama zilifuatwa za utoaji wa ardhi.
“Ndani ya kamati kutakuwa na mjumbe kutoka jeshi la Polisi, Afisa wa Usalama, Afisa Utumishi, Afisa Tarafa, Mtendaji wa Kata pamoja na Diwani kwa ajili ya kutoa ushirikiano.
“Baada ya uchunguzi kamati hiyo itasoma taarifa ya uchunguzi kwenye mkutano wa hadhara kama huu,” amesema Nguvila.
Aidha amesema ili kujikwamua kiuchumi wananchi wa kijiji hicho wanatakiwa kuchangamkia fursa ya kilimo hasa kwa kupanda mibuni pamoja na kilimo cha parachichi.
Amemuagiza Mtendaji wa Kijiji hicho kuhakikisha anaandaa taarifa ya mapato na matumizi na kuitisha mkutano wa hadhara wa kijiji ili wananchi waweze kusomewa taarifa ya mapato na matumizi ya kijiji chao.