Na Aziza Masoud na Ferdnanda Mbamla, Dar es Salaam
ENEO la Riverside Ubungo jijini Dar es Salaam, jana liligeuka uwanja wa mapambano baada ya polisi kutumia risasi za moto na mabomu ya machozi ili kunusuru hafla ya kuapishwa wenyeviti wa Serikali za Mitaa katika Wilaya ya Kinondoni.
Dalili za kuibuka kwa fujo zilianza kuonekana kwa wananchi waliokuwa wamekusanyika nje ya hoteli ya Land Mark ambako hafla hiyo ilipangwa kufanyika, waliokuwa wakipinga kuapishwa kwa waliokuwa wagombea uenyekiti kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) waliodai walishindwa katika uchaguzi huo.
Wananchi hao ambao wengi wao wanatoka mitaa ya Msisiri ‘A’, Kawe Ukwamani, Kata ya Saranga, Kimara King’ong’o na Mtaa wa Temboni, Kata ya Msigani, walidai katika maeneo yao, wagombea wa CCM walipewa ushindi kinyume na matokeo halali.
Walidai kuwa katika uchaguzi huo, wagombea halali walioshinda wanatoka Chama cha Wananchi (CUF), lakini matokeo yalibadilishwa siku ya pili baada ya kutangazwa.
MABOMU NA RISASI
Katika tukio hilo, polisi walilazimika kupiga mabomu ya machozi na kurusha juu risasi za moto, huku wakiwataka wananchi kuondoka eneo hilo baada ya kuona fujo zinaweza kuwa kubwa.
Wakati risasi zikirushwa, wananchi hao walikuwa wakiimba kwa kutaja neno “Ukawa, Ukawa…” na wengine walikuwa wakisikika wakisema “zipigwe risasi nyingine” ndipo polisi walipoanza kupiga mabomu ya machozi.
Pamoja na mabomu kupigwa, wananchi waliamua kuhamia upande wa pili wa hoteli hiyo.
Hali ilikuwa ngumu katika geti la kuingia hotelini hapo ambapo muda wote lilionekana limezingirwa.
NDANI YA MTARO
Mambo yalibadilika zaidi, baada ya aliyekuwa mgombea kutoka Mtaa wa Msisiri ‘A’, Juma Mbena (CCM) kushindwa kuingia ndani, baada ya kuzuiwa na wananchi.
Inadaiwa katika mtaa huo, matokeo halali yalibadilishwa, licha ya kuonyesha mgombea wa CUF, Gasper Chambembe ni mshindi kwa kupata kura 497 dhidi ya 450 za Mbena.
Muda wote wananchi walikuwa wakimtaka Mbena kuondoka eneo hilo, huku wakimvuta shati lake hadi kuchanika wakidai si kiongozi wao halali.
Baada ya kuona amezidiwa, Mbena alikimbia na kwenda kujificha ndani ya mtaro wa maji machafu.
“Huyu kiongozi aliyekuja kuapishwa hapa tutahakikisha haingii kwa kuwa si chaguo letu, eneo letu alishinda mgombea wa CUF, tuliamka asubuhi lakini ilipofika saa 4 matokeo yalibadilishwa na ofisa mtendaji kwa kufutwafutwa kwa kalamu ya wino na kumpa ushindi mgombea wa CCM ambaye alishindwa katika uchaguzi,” alisema mmoja wa wananchi hao aliyefahamika kwa jina moja la Nassoro.
Wananchi kutoka eneo la Kawe Ukwamani walifika kwenye hoteli hiyo wakiwa na aliyekuwa mgombea wao wa uenyekiti, Nasri Mohamed (CUF), lakini alizuiwa kuingia ndani kwa kile kichodaiwa hakuwa na barua ya mwaliko kutoka Manispaa ya Kinondoni.
“Mimi nimeingia ndani nikatolewa, amebaki mwenzangu wa CCM ambaye katika uchaguzi ule nilimshinda,” alisema Mohamed.
Alisema katika uchaguzi huo alishinda kwa kupata kura 568 dhidi ya aliyekuwa mgombea wa CCM, Suleiman Jeta aliyepata kura 560.
MKURUGENZI WA MANISPAA
Mkurugenzi wa Manispaa ya Kinondoni, Mussa Nati, alisema wenyeviti 154 waliapishwa kati ya 191.
“Tumeapisha wenyeviti 154 kati ya 191. Kutokana na sababu mbalimbali zikiwamo ugonjwa na dharura nyingine wengine wameshindwa kufika,” alisema Nati.
Alipoulizwa kuhusu malalamiko ya wananchi na kuhusishwa kuvuruga uchaguzi huo, alisema hana jibu kwakuwa alikuwa akipata majina ya washindi kutoka kwa watendaji wa mitaa na kata.
Wenyeviti hao waliapishwa na Mwanasheria wa Manispaa hiyo, Burton Mahenge.
KAMANDA WA POLISI
Akizungumzia vurugu hizo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Camillus Wambura, alikiri kutokea na kusema hadi jana walikuwa wanashikilia watu saba.
Aliwataja watuhumiwa hao kuwa ni Kinyaiya Shiriri, Fadhili Ally, Wilfred Ngowi, Stanley Hurio, Prisan Clement, Joseph Samki na Zito Fabiani.
Alisema wanaendelea kuwahoji na uchunguzi utakapokamilika jalada lao litapelekwa kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali ili sheria ichukue mkondo wake.