Mbunge wa Sengerema, William Ngeleja amehojiwa kwa saa moja katika Ofisi ya Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai (DCI), jijini Dar es Salaam leo Jumatatu Septemba 11.
Ngeleja ambaye pia amewahi kuwa Waziri wa Nishati na Madini wa awamu ya nne, aliwasili katika ofisi hiyo saa nne asubuhi akiwa peke yake ambapo alikutana na DCI saa tano na kuondoka saa sita na nusu mchana bila kusema alichohojiwa.
Hatua ya Ngeleja kufika ofisini hapo ni kuitikia wito wa Mkuu wa Jeshi La Polisi (IGP), Simon Sirro ambaye aliwataka watuhumiwa waliotajwa katika ripoti ya Tanzanite na Almasi kuripoti kwenye ofisi hiyo kwa ajili ya mahojiano wakati uchunguzi ukiendelea
Katika hatua nyingine, baada ya Ngeleja kuondoka Katibu Mkuu wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Dk Vincent Mashinji naye aliingia kuhojiwa kuhusiana na taarifa za kupigwa risasi kwa Mwanasheria Mkuu wa chama hicho, Tundu Lissu.
Kwa upande wake Mashinji, ameitikia wito wa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, Gilles Muroto ambaye alimtaka kiongozi huyo kufika kwenye Ofisi ya Polisi ya Mkoa wa Dodoma au Ofisi ya DCI kwa ajili ya kuhojiwa.
Katika wito wake huo, Muroto pia alimtaka dreva wa Lissu, Simon Bakari kuisaidia polisi kuhusiana na tukio hilo la kupigwa risasi kwa Lissu, Septemba 7, mwaka huu mjini Dodoma.