CATALUNYA, Hispania
IKIWA ni siku chache zimepita tangu klabu ya PSG kutangaza kuwa ilikuwa tayari kumpa ndege staa, Neymar ikiwa angekubali kutua klabuni hapo nyota huyo ameibuka na mapya.
Kwa mujibu wa kauli iliyotolewa na mpachikaji mabao huyo, hakuna kitakachomfanya kuikacha klabu yake ya sasa ya Barcelona.
Straika huyo amedai kuwa hapati picha ni kitu gani kitakachosababisha aachane na mabingwa hao wa Ulaya na kutimkia katika klabu nyingine.
Itakumbukwa kuwa baada ya kuwaniwa na klabu kadhaa wakati wa dirisha la usajili la Januari, fowadi huyo wa kimataifa wa Brazil alisaini mkataba mpya wa kuendelea kukipiga katika kikosi cha Wacatalunya hao.
Juni mwaka huu, Neymar alisaini mkataba wa miaka mitano ambao utamweka klabuni hapo mpaka mwaka 2021.
Akizungumzia uwezekano wa kukipiga kwingineko, Neymar amesema imekuwa ngumu kila anapojaribu kufikiria kuvaa jezi za timu nyingine.
“Sioni uwezekano wa kuwa nje ya Barca. Bado sijafikiria kabisa kuhusu hilo,” alisema Neymar.
“Najiona kama sehemu muhimu ya timu na nadhani naweza kusaidia zaidi na zaidi.”
Alipoulizwa juu ya tetesi za kutakiwa na matajiri wa PSG kwa dau lililotajwa kuwa lingevunja rekodi, staa huyo alikataa kulizungumzia suala hilo.
“Siwezi kuthibitisha kuhusu hilo kwa sababu sipendi kuzungumzia kuhusu fedha. Nimeshawahi kusema nilikuwa na mazungumzo na klabu nyingi na nilichagua kubaki hapa sehemu ambayo huwa nahisi ni nyumbani.”
“Kama nilivyosema, mimi ni mali ya Barca na ninafurahia maisha ya hapa.”
Mbali na hilo, Neymar alizungumzia kichapo cha mabao 7-1 walichokipata Brazil kutoka kwa Ujerumani katika mchezo wa hatua ya nusu fainali ya Kombe la Dunia ya mwaka 2015.
Alisema hana shaka kuwa hilo halitatokea tena kwani kikosi chao cha sasa kina morali ya hali ya juu tofauti na miaka kadhaa iliyopita.
Kinachomtia jeuri nyota huyo mwenye umri wa miaka 24 ni kitendo cha Brazil kushinda michezo yake miwili ya kuwania kufuzu fainali za Kombe la Dunia za mwaka 2018.
Wakiwa na kocha Tite aliyechukua nafasi ya Carlos Dunga, Brazil walishinda mchezo wa kwanza dhidi ya Ecuador kabla ya kuwasambaratisha Colombia.
Matokeo hayo yamewafanya kuingia ‘top five’ ya viwango vya Shirikisho la Soka Ulimwenguni (FIFA).
“Mara kwa mara Brazil imekuwa na wachezaji wenye viwango. Hatukushinda fainali za Kombe la Dunia na hata hivyo kulikuwa na presha kubwa kwenye kundi letu. Tuna timu kubwa na kocha mwenye heshima kubwa pia,” alisema.